Nazifunga Tena Makala Zote, Na Ombi Muhimu Kwako Wewe Rafiki Yangu.

Habari za wakati huu rafiki?
Naamini unaendelea vizuri na kuyafanya maisha yako kuwa bora kila siku. Hii ndiyo habari ninayotaka kuisikia kutoka kwako kwa sababu dhumuni langu kwenye maisha ni kuwa sehemu ya mabadiliko chanya kwenye maisha ya wengine. Kupitia chochote ninachofanya, napenda kuona maisha ya wengine yakibadilika na kuwa bora zaidi. Ninaamini sana kwenye hili kwa sababu najua inawezekana kwa kila mtu kuwa na maisha bora zaidi ya aliyonayo sasa. Na ukilinganisha na uwezo ulio ndani yetu, tunatumia kiasi kidogo sana.
Wakati naanzisha mtandao wa AMKA MTANZANIA hakukuwa na mitandao mingi inayotoa maarifa ya kuboresha maisha kwa kipindi kile, na hivyo ilikuwa kazi ngumu sana kuwafikia watu. Ilikuwa bado ni kitu kigeni na wengi hawakuwa wakielewa achilia mbali kuamini kwamba jukumu la kuboresha maisha yao ni lao wenyewe, na wanaweza kufanya hivyo kama wataamua. Tumekwenda na safari hii na angalau sasa kuna mwamko mkubwa wa watu kuchukua hatua. Watu wanaboresha kazi zao, watu wanaanzisha biashara, watu wanaingia kwenye kilimo na watu wengi zaidi wanaondoka kwenye madeni na kuweza kuweka akiba na hata kuwekeza.
Hii ni kazi kubwa sana ambayo tumeifanya kwa pamoja, na wewe umeweka juhudi kubwa sana na umeona zinakusaidia ndio maana mpaka sasa tupo pamoja hapa.
Wakati naanzisha AMKA MTANZANIA na watu wakaanza kuelewa kulitokea wimbi kubwa la watu kunakili makala kutoka kwenye AMKA MTANZANIA na kuzisambaza kwa kuweka majina yao kwamba wao ni waandishi. Hali ile ilinifanya kuzifunga makala kwenye AMKA MTANZANIA hivyo ikawa haiwezekani watu kunakili. Baadae nilikuja kuondoa kifungo kile na kuruhusu mtu yeyote aweze kunakili makala na kuzisambaza kwa wengine. Kwa sababu ninaamini maarifa haya yanatakiwa kuwafikia wengi zaidi na njia ya kufanya hivyo ni kwa kila msomaji kuwa balozi wa kusambaza maarifa haya mazuri. Na niliomba yeyote anayenakili, hata kama hatotaka kuandika jina la mwandishi, basi angalau aseme makala imetoka AMKA MTANZANIA.
Tumekwenda na hali hiyo mpaka siku za hivi karibuni, tangu mwaka jana 2015, kumekuwa na wimbi kubwa sana la kunakili makala kwenye AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA na mbaya zaidi watu wanazitumia kujinufaisha wao binafsi. Kuna watu wameanzisha blog zao kabisa na wanachukua makala na kuziweka kwenye hizo blog kama ni makala zao wameandika. Nimekuwa napata taarifa na kuwasiliana na watu hawa lakini wamekuwa hawaoneshi mwitikio chanya. Nakumbuka kuna mtu alianzisha blog akawa anaweka kila ninachoandika, ila chini ya makala anaondoa jina langu anaweka lake. Nikiandaa semina anachukua maelezo yale yale na chini anaweka taarifa zake na namba zake za malipo. Nilimtafuta kumweleza kwamba anajipoteza yeye mwenyewe, kwa sababu mambo sio rahisi kama anavyofikiri. Na kweli hakuweza kwenda mbali.
Watu wengi sasa wamekuwa wanachukua makala, kama ilivyo na chini wanaondoa jina na kuweka jina lake na kisha kusambaza kwa njia mbalimbali. Kuna watu wamejizolea umaarufu kwenye makundi mbalimbali ya facebook na wasap kwa makala nzuri wanazowapa watu, kumbe wamezinakili kutoka AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA.
Ni kutokana na hali hii nimefikia maamuzi ya kuzifunga tena makala zote kwenye AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA. Kwa sasa hutaweza kunakili maelezo ya makala na kusambaza kwa njia hiyo. Bali njia pekee unayoweza kusambaza ni kuchukua link na kuisambaza, au kubonyeza vitufe vya share kwa mitandao mbalimbali ya kijamii.
Na hata ikitokea ukaweza kunakili kwa mbinu za kiteknolojia, napenda ujue kwamba siruhusu hilo.
Naomba niweke wazi kwamba sizuii mtu kuandika, wala sina tatizo na mtu yeyote anayeandika hata kama ataandika kama ninachoandika mimi. Kwanza napenda sana watu wanaoandika, na mara nyingi nimekuwa nawasiliana nao na kuwapa moyo, kwa sababu hii sio kazi rahisi. Ninachozuia hapa ni wale wavivu ambao hawataki kujishughulisha ila wanataka kupakua chakula kilichoiva na kula, hii sio tabia nzuri na inakwenda kinyume kabisa na falsafa yangu ya maisha.
Ombi muhimu kwako wewe rafiki yangu.
Nakuomba sana wewe rafiki yangu tusaidiane kufanya makala hizi nzuri ziwafikie watu wengi zaidi. Ukilinganisha na idadi ya watu wanaohitaji huduma hizi, ni wachache sana ambao tumeshawafikia. Kama wewe unazifurahia hizi huduma na unaona zina msaada kwako, basi fikiria watu watano ambao nao wanaweza kunufaika na watumie link ya makala unazozisoma kwenye AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA.
Kila siku nakazana kuhakikisha unapata huduma iliyo bora sana, ya kukuwezesha wewe kuwa na maisha bora kila siku mpya unayoianza. Na hili ni jukumu nililochagua kufanya kwa maisha yangu yote, bila kujali nitakuwa napitia nini. Hivyo napenda kukuhakikishia kwamba nipo hapa kwa muda mrefu, na ninapokwambia TUPO PAMOJA, basi jua tupo pamoja kweli.
Asante sana rafiki yangu kwa kuendelea kuwa pamoja na mimi katika safari hii, tuendelee kuwa pamoja kwa sababu ukilinganisha na maarifa tunayopaswa kuwa nayo, tunajua kidogo sana. Yaani ni sawa na kusema hatujui chochote, ndio maana mara zote nakwambia kila siku ni lazima tujifunze.
Asante na karibu sana,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: