Tunaishi kwenye dunia ambayo mabadiliko yanatokea kwa kasi kuliko kipindi chochote kuwahi kutokea. Ukiangalia tangu zama za mawe, ilichukua muda mrefu sana kufikia zama za chuma, na baadaye mapinduzi ya viwanda. Lakini tangu tumeingia kwenye zama hizi za taarifa, kugunduliwa kwa mtandao wa intaneti kumeleta mabadiliko makubwa na ya haraka sana.
Kwa maisha haya yenye mabadiliko yaendayo kwa kasi, njia pekee ya kuhakikisha unakuwa bora na kufikia mafanikio makubwa ni kuwa mvumbuzi. Kuwa mvumbuzi kwenye kazi unayofanya na kuwa mvumbuzi kwenye biashara yako. bila ya uvumbuzi huwezi kuwa na mabadiliko na bila ya mabadiliko huna cha kukutofautisha na wengine, hivyo utapotea.
Wiki hii tumesoma kitabu The truth about innovation ambacho kimeandikwa na mwandishi Mac McKeown. Mwandishi ametupa ukweli kuhusu uvumbuzi kwenye maisha yetu ya kila siku. Ametuonesha ni kwa jinsi gani uvumbuzi sio mgumu kama wengi tunavyofikiri na ametupa mbinu za kuweza kufikia uvumbuzi kwa urahisi kwenye chochote tunachofanya.
Karibu tuungane katika mambo haya 20 niliyojifunza kwenye kitabu hiki, kuna mengi unaweza kujifunza na kufanyia kazi.
1. Uvumbuzi ni pale unapokuja na kitu kipya na ambacho kina matumizi mazuri kwa wengine. Na upya wa kitu sio lazima kiwe kipya kabisa, bali inawezekana ni kitu kile kile ila kimeongezwa ubora zaidi. Na matumizi mazuri ya kitu ni kutokana na mahitaji ya yule anayekwenda kutumia kitu hiko. Hivyo unapofikiria kufanya uvumbuzi kwenye kazi au biashara yako, angalia ni kitu gani unaweza kuboresha na kikawa na matumizi mazuri kwa wateja wako.
2. Kuna misukumo mikubwa miwili inayochochea watu kufanya uvumbuzi.
Msukumo wa kwanza ni watu wanatafuta ufumbuzi wa changamoto wanazopitia wao. Na hapo wanakuwa wametafuta suluhisho na hawajalipata iwe ni kutokana na kutokuwepo kabisa, au kuwepo ila gharama kubwa, au suluhisho kuwepo lakini sio rahisi kutumia.
Msukumo wa pili ni kutaka kutafuta suluhisho la matatizo ya watu wengine. Hapa mtu anaiona fursa na kuitumia kwa kuleta suluhisho la changamoto inayowasumbua wengine, ambayo bado haijatatuliwa.
Haya ni maeneo mawili muhimu sana kwako kuyaangalia na kuona ni jinsi gani kazi yako au biashara yako inaweza kutatua matatizo uliyonayo au waliyonayo wengine, na suluhisho lako liwe bora kuliko yaliyopo sasa.
3. Kila uvumbuzi ni mpya, ila uvumbuzi unatofautiana kwa viwango vya upya. Hapa kuna viwango vitatu vya upya wa uvumbuzi;
Kwanza ni upya unaoongezwa kidogo kidogo. Hapa mtu anaanza na huduma au bidhaa na kadiri siku zinavyokwenda marekebisho madogo madogo yanafanyika na hatimaye inakuwa bidhaa au huduma ya tofauti kabisa na ilipoanza.
Pili ni mabadiliko makubwa sana yanayofanyika mara moja kwenye bidhaa au huduma. Hapa kitu kipya kabisa kinazaliwa ambacho ni bora zaidi.
Tatu ni mapinduzi ambapo uvumbuzi mwingi unaohusiana unakuja pamoja na kuleta mabadiliko makubwa sana. Mfano mapinduzi ya viwanda, mapinduzi ya teknolojia.
4. Uvumbuzi pia unaweza kutokea kwenye maeneo matatu muhimu sana.
Eneo la kwanza ni kwenye bidhaa au huduma. Hapa mabadiliko yanafanywa kwenye bidhaa au huduma inayotolewa na hivyo kuifanya kuwa bora zaidi kwa mtumiaji.
Eneo la pili ni mchakato, hapa mabadiliko yanafanyika kwenye mchakato wa kuzalisha na kutoa bidhaa au huduma. Hapa watu wanavumbua njia mpya ya kufanya kitu, na hivyo kitu kufanyika kwa ubora zaidi.
Eneo la tatu ni uvumbuzi kwenye uongozi, hapa mabadiliko yanafanyika kwenye muundo wa uongozi na usimamizi wa watu. Hapa uongozi unaboreshwa kama kuondoa urasimu na kujenga timu nzuri kwa ufanyaji wa kazi.
5. Hakuna kitu kama wazo kamili la biashara, kwamba kuna wazo moja ukishalipata tu basi biashara yako inakwenda vizuri sana, hakuna. Badala yake kuna mawazo mazuri ya bishara ambayo yanaweza kuleta faida. Ila kadiri muda unavyokwenda, mawazo haya ya biashara yanahitaji kuboreshwa zaidi ili kuendana na mabadiliko yanayoendelea kutokea. Kitu chochote kizuri kinaweza kufanywa kuwa kizuri zaidi, na hivi ndivyo ilivyo kwenye biashara. Hivyo badala ya kusubiri upate wazo la kipekee la biashara, anza na wazo lolote linaloweza kuleta faida, kisha nenda ukiboresha kila siku.
6. Wazo lolote la biashara au uvumbuzi ambalo lina nguvu kubwa ya kuleta mabadiliko makubwa haliwezi kuzuiwa na kitu chochote. Hii ni kwa sababu wavumbuzi wanakuwa na kiu kubwa ya kutoa kitu bora sana kwa wale wanaokitegemea na watu pia wana kiu ya kupata kitu ambacho ni bora zaidi. Kwa njia hii mawazo haya ya uvumbuzi yanaleta matokeo makubwa. uvumbuzi wowote unasukumwa na vitu hivyo viwili, kujitoa kwa mvumbuzi, na hitaji la wateja. Hivyo na wewe unaweza kuangalia ni eneo gani upo tayari kujitoa na soko linataka nini. Na weka juhudi.
7. Hakuna wazo lolote unaloweza kulilinda, hasa kwa ulimwengu wa sasa ambapo kila mtu anatafuta mawazo mazuri ya kufanyia kazi. Na pia kitakachokufanya ushindwe kulinda ni kwamba hakuna wazo lililokamilika, hivyo mtu yeyote anaweza kuchukua wazo lako na kuliboresha zaidi. Hivyo unapopata wazo, lifanyie kazi na kila siku liboreshe, hapo ndio utajipa uhakika wa kulifaidi wazo hilo.
8. Kuna maeneo matatu unayoweza kuangalia ili kupata mawazo ya uvumbuzi kwenye kazi yako au biashara yako.
Moja, angalia nyuma au ulikotoka. Angalia ni hatari gani zilitishia kuua kazi yako au biashara yako. ni kitu gani kimeua biashara za wengine huko nyuma? Ni hatari gani imekuwepo kwenye aina ya biashara au kazi unayofanya.
Pili, angalia kesho au siku zijazo. Jiulize ni hatari gani inaweza kuikumba biashara yako siku za mbeleni? Ni bidhaa gani washindani wako wanaweza kuja nazo? Ni sheria gani mpya zinaweza kuathiri biashara yako? je kutakuwa na mabadiliko gani ya wateja?
Tatu, angalia sasa, wakati huu tuliopo. Ni mambo gani yanaendelea sasa kwenye biashara au kazi uliyopo, ni maeneo gani yanahitaji kuboreshwa zaidi? Ni mambo gani unaweza kujifunza kwenye kushinda na kushindwa kwa wengine?
9. Katika uvumbuzi, usitafute njia ya kufanya kimoja na kuacha kingine, bali tafuta njia ya kuweza kufanya vyote kwa pamoja na kwa ubora. Kwenye maisha watu wengi wanalazimika kuchagua moja kati ya vitu au hali mbili. Wavumbuzi wazuri wanawapatia watu uwezo wa kuchagua vyote viwili na maisha yao kuwa bora zaidi. Kwa mfano watu wanataka kitu cha bei rahisi na ambacho ni bora. Na mara nyingi vitu bora ni bei ghali, na vitu vya bei rahisi sio bora. Sasa wewe tumia uvumbuzi wako kuja na kitu ambacho watu wanakihitaji na ni bei rahisi na kina ubora wa hali ya juu.
10. Kuna maswali mawili ambayo yanachokoza fikra za kivumbuzi. Maswali hayo ni KWA NINI, na KWA NINI ISIWE. Jambo lolote unalofanya sasa jiulize kwa nini unafanya, na ukishajiuliza kwa nini, jiulize kwa nini isiwe hivi. Ukijiuliza maswali hayo mara nyingi uwezavyo kwenye kila unachofanya, ni lazima utakuja na mawazo mengi sana ya kuboresha unachofanya.
11. Hakuna kitu kinachozaliwa kipya kabia, hata binadamu. Wewe ulizaliwa na chembechembe ulizorithi kwa wazazi wako, ambao na wao walirithi kutoka kwa wazazi wao. Hivyo hata kwenye uvumbuzi, hutakuja na kitu kipya kabisa, bali utakuja na kitui chenye chembechembe za vitu vinavyofanyika sasa. Hivyo angalia sana unavyofanya sasa, angalia sana wengine wanavyofanya, kisha njoo na njia nyingine bora ya kufanya, ikiwa na chembechembe za inavyofanyika sasa.
12. Mawazo yote makubwa tunayoona sasa, yanatokana na mawazo ambayo yalikuwepo zamani sana. Hivyo hata mawazo yako makubwa, yatatokana na mawazo yaliyopo sasa. Je unayapataje mawazo yaliyopo sasa na ya zamani? Ni lazima uwe mchunguzi, lazima uwe mtu wa kuhoji, na lazima uwe mtu wa kujifunza kwa kujisomea. Soma vitabu ambavyo havihusiki hata na taaluma yako, soma vitabu vya aina mbalimbali, soma historia, soma kuhusu vita, soma kuhusu falsafa na utaona jinsi gani mawazo unayopata yanaweza kuboresha mawazo yako na ukaja na kitu bora kabisa.
13. Katika uvumbuzi, unaweza kufanya badiliko moja kubwa na ukaleta uvumbuzi mkubwa, au unaweza kufanya mabadiliko mengi madogo madogo na ukaweza kufikia uvumbuzi mkubwa. Kwenye uvumbuzi mmoja mkubwa ni kama ukipata unapata kweli, na ukikosa umekwisha. Lakini kwenye uvumbuzi mdogo mdogo, kuna vingi vitashindwa ila pia kuna vingi vitakavyoshindwa. Hivyo ni bora kufanya kidogo kidogo.
14. Ni bora kuomba samahani kuliko kuomba ruhusa. Na mawa zote kwenye uvumbuzi, ukiomba ruhusa hakuna atakayekupa, ila ukifanya bila ya ruhusa, ni rahisi kuomba samahani baadaye. Na kama uvumbuzi wako umefanikiwa, huna hata haja ya kuomba samahani. Hii ni kwa wote iwe umeajiriwa au unafanya biashara, kuwa na utayari wa kufanya kitu ambacho hakijazoeleka ila wewe unaamini kitaleta matokeo bora sana/ hivi ndivyo mabadiliko yanavyotokea.
15. Ubunifu ni mchakato na sio ajali. Kuna watu huwa wanoana kama kuna watu fulani wamezaliwa wakiwa wabunifu, au kuna wakati ubunifu unamjia mtu kama ajali. Hii sio kweli, ubunifu ni mchakato, na ni mchakato mrefu na unaoumiza. Mpaka unaona mtu kaja na wazo moja bora, jua kuna mawazo mengi sana ambayo hayakuwa mazuri alishayapitia. Hivyo ingia kwenye mchakato wa kuja na mawazo mapya kila siku, na katika mchakato huu utakutana na ubunifu ambao utapelekea kuja na uvumbuzi.
16. Watu wote wabunifu wanapenda mawazo mapya. Wanakusanya mawazo na kuyafuatilia zaidi. Wanapitia mawazo mengi na kujaribu kuyaunganisha au kuyaboresha zaidi. Kwa njia hii wanatoka na wazo ambalo ni bora. Watu hawa wanakusanya mawazo kutoka sehemu mbalimbali ambazo zinaweza kuwa hazina uhusiano na kila wanachofanya. Kwa kuleta mawazo haya pamoja wanaona njia inayoweza kuwa bora kwa kile wanachofanya wao.
17. Ubunifu ndio zawadi ya ubunifu. Watu wana misukumo ya aina mbili kwenye kufanya kitu, kuna msukumo wa nje na msukumo wa ndani. Msukumo wa nje ni ule wa vitu mtu anapewa, msukumo wa ndani ni vile mtu anavyojisikia kwa kufanya kile anachofanya. Msukumo wa ndani ndio bora zaidi. Na msukumo huu huleta ubunifu ambayo ndio zawadi inayochochea mtu kujituma zaidi. Hakikisha kile unachofanya unapata msukumo kutoka ndani yako.
18. Wakati mwingine unaweza kupata mawazo mazuri na ya kibunifu kutoka kwenye kundi la watu. Hapa unaweza kuwakusanya watu kwa pamoja na kila mtu akatoa mawazo yake kulingana na hali iliyopo. Watu hawa wanaweza kuwa wafanyakazi au pia wanaweza kuwa wateja wa bidhaa husika. Usisahau makundi unayohusika nayo wakati unapotafuta uvumbuzi.
19. Katika uvumbuzi pia usiwe na haraka sana, na usikamie sana kitu. Mawazo makubwa kuwahi kutokea duniani, yalitokea wakati wavumbuzi hao wakiwa wamepumzika, au wakiwa wanafanya kitu ambacho hakihusiani kabisa na kile walichokuwa wanafanyia kazi. Kuna usemi kwamba mwanasayansi Newton aligundua nguvu ya mvutano ya dunia akiwa amekaa chini ya mti na kuona tunda linadondoka chini. Hivyo jipe nafasi na mawazo ya kiuvumbuzi yanaweza kukujia muda wowote na popote ulipo.
20. Katika ushindani wa kibiashara, fanya kile ambacho mshindani wako hafanyi. Hii ndio njia bora kabisa ya kushindana ambayo haitakuumiza kabisa wewe. Lakini ukishindana moja kwa moja, mtaishia kugombea kitu kimoja ambapo wote mtaumia. Kuna njia tatu za kufanya kile ambacho mshindani wako hafanyi.
Moja, fanya kile ambacho hawezi kufanya. Mshindani wako kuna vitu vingi ambavyo hawezi kufanya, vijue na wewe vifanye kwa ubora sana.
Pili fanya vile ambavyo mshindani wako hawezi kuelewa. Hapa unakuja na kitu ambacho mshindani wako haelewi unafanyaje, hapa pia utapata nafasi kubwa ya kutengeneza wateja.
Tatu fanya kile ambacho mshindani wako hayupo tayari kufanya. Kuna maeneo mengi ya biashara yako ambayo mshindani wako ameamua kuachana nayo, hataki kuyawekea uzito, yajue na yawekee uzito wewe.
Ni muhimu sana kwa kila mmoja wetu kuwa mvumbuzi kwa sababu tunaishi kwenye dunia yenye mabadiliko mengi na ushindani umekuwa mkubwa sana. Na uvumbuzi unaanza na mawazo ambayo sio lazima yawe mazuri. Kuwa na mawazo mengi na yachunguze na kuhoji zaidi, ni lazima utakuja na amwazo bora sana kwa kazi yako au biashara yako.
Kila la kheri.
asante kocha
LikeLike
Karibu sana.
LikeLike