Pale biashara yako inapokua, unaanza kuona fursa nyingi zaidi za kukuza biashara hiyo. Haya ndiyo madhara mazuri ya kuendesha biashara yako kitaalamu. Na unapofika wakati wa kuikuza zaidi biashara yako, kufungua matawi sehemu mpya ni moja ya sehemu za ukuaji wa biashara yako. pamoja na kufanikiwa sana kwa biashara kwenye eneo moja, haimaanishi moja kwa moja utafanikiwa kwenye eneo jingine. Hivyo ni muhimu sana kujiandaa kabla hujaanzisha biashara yako kwenye eneo jingine ili uweze kuikuza biashara yako zaidi hata kule utakapofungua tawi.
Leo kupitia makala hii ya kona ya mjasiriamali tunakwenda kuangalia mambo muhimu ya kuzingatia pale unapoikuza biashara yako kwa kufungua tawi kwenye eneo jingine. Karibu sana tujifunze na uyafanyie kazi.
Kitu muhimu kabisa kuzingatia ni kwenda kufanya biashara unayofanya sasa. Kuna wafanyabiashara wengi ambao huwa wanafikiri kufanikiwa kwenye biashara moja basi ni tiketi ya kufanikiwa biashara yoyote. Sio kweli, biashara yoyote utakayoingia mpya, kuna kipindi cha kujifunza. Hivyo kama hutaki kupitia kipindi hiki, ni vyema ukaenda kufanya biashara unayofanya sasa. Hii ni kwa sababu biashara hii unaifahamu vizuri kuanzia upatikanaji wa bidhaa au huduma mpaka usambazaji wake. Unajuana na watu muhimu waliopo kwenye mtandao huo na pia unazijua tabia za wateja katika aina hiyo ya biashara. Hivyo zingatia hili, kafanye biashara ambayo unafanya sasa.
Kitu kingine muhimu sana kuzingatia ni kuangalia soko la eneo hilo jipya likoje. Kujua washindani wako wanafanyaje biashara hiyo. Kwa kifupi unahitaji kujua kila kitu kuhusu biashara unayokwenda kufanya kwenye eneo hilo. Jua washindani wako ni wakina nani, jua nguvu yao, jua madhaifu yao na jua ni maeneo gani ambayo bado hawajayafikia vizuri. Jiangalie na wewe mwenyewe unapokwenda pale unapeleka kitu gani cha tofauti, kitu gani ambacho watu kwa sasa hawakipati. Na hata kama utakwenda kufanya biashara ambayo inafanana na wengine, basi hakikisha huduma unazozitoa ni bora sana kiasi kwamba mteja atakuwa tayari kumwambia mwingine na mwingine.
Pia zingatia sana ufanano wa biashara yako kwa ulipo sasa na kule unakokwenda. Ni vyema viwango vikawa sawa. Hata kama biashara utakayokwenda kuanza haitakuwa inaingiza biashara kwa sasa, usikubali kuiendesha kwa viwango vya chini ukilinganisha na biashara yako kuu. Nenda na viwango vile vile ambavyo unavyo kwenye biashara yako. hii itakusaidia kutengeneza jina la biashara yako. kwa njia hii mtu anakuwa na uhakika popote anapokutana na biashara yako basi anapata ubora wa hali ya juu sana. Usiangushe matarajio ya wateja wako.
Unahitaji kuzingatia mpangilio na matumizi mazuri ya muda wako. Kwa sasa kama unafanya biashara moja, ina maana muda wako mwingi umeweka pale. Sasa utakapofungua biashara ya pili ina maana unahitaji kupangilia muda wako vizuri, maana kwa sasa unahitaji kusimamia biashara mbili na sio moja kama ulivyokuwa umezoea. Wafanyabiashara wengi huwa wanashindwa kujipanga vizuri na hivyo usimamizi kuwa mbovu. Mwishowe kuanzisha biashara mpya kunaishia kuua biashara ambayo ilikuwa na mafanikio. Usikubali kuanzisha biashara mpya kuwe chanzo cha biashara yako nzuri kuzorota, jipange vizuri ili uwe na usimamizi wa uhakika kwenye biashara zako zote.
Kitu cha mwisho cha kuzingatia ni kutafuta wasaidizi wazuri kwenye biashara yako. ni jambo lililo wazi kwamba hutaweza kuwepo kwenye biashara zako zote kwa wakati mmoja na hivyo unahitaji kuwa na wasaidizi bora sana kwenye biashara yako. kwenye biashara ambayo ndiyo umeanza nayo, unahitaji uwe ulishamwandaa mtu wa kuendelea kuwepo pale. Mtu huyo anatakiwa kuwa anaijua biashara vizuri na anaujua utaratibu wako w akuendesha biashara na jinsi ya kufikia maamuzi kunapokuwa na changamoto. Na unapokwenda kwenye biashara mpya unahitaji kutengeneza mtu mwingine pale pia. Au unaweza kumpeleka msaidizi uliyekuwa naye kwenye biashara uliyokuwa nayo awali. Kwa vyovyote vile hakikisha unaweka muda wa kutosha kwenye biashara mpya unayokwenda kuanzisha kwa sababu inakuhitaji sana, hasa mwanzoni.
Kuza biashara yako kwa kufungua matawi mapya ya biashara ile ambayo unafanya sasa. Na zingatia haya tuliyojadili hapa katika kuhakikisha unakuza biashara yako vizuri. Kila la kheri.