Tangu kuwepo kwa mfumo rasmi wa elimu, elimu ya darasani imekuwa inapewa kipaumbele kikubwa sana kwenye jamii zetu. Imekuwa ikizoeleka sana, wale ambao wanapata elimu rasmi ya darasani ndio pekee wanaopata nafasi za kuajiriwa na kuwa na maisha bora. Ila kwa sasa mambo yamebadilika sana, elimu ya darasani karibu kila mtu anayo na bado mambo siyo mazuri. Hapa ndipo inapokuja elimu binafsi, elimu ya kujifunza wewe mwenyewe bila ya kwenda darasani.

Katika kitabu hiki cha Don’t go back to school, mwandishi Kio Stark ameonesha kwa mifano watu ambao wameweza kufikia mafanikio makubwa sana kwneye maisha yao licha ya kuwa hawakupata elimu ya juu. Kio amefanya mahojiani na waandishi, wanasayansi, wajasiriamali, wasanii na kada nyingine ambapo watu wamepata mafanikio makubwa licha ya kukosa degree kama wengi wanavyoamini degree ni kila kitu.

Kio anatushirikisha mbinu za kujifunza kitu chochote unachotaka kwenye maisha yako, wewe mwenyewe bila ya kurudi darasani. Na uzuri wa kujifunza mwenyewe ni kwamba kwanza unapenda kile unachojifunza, tofauti na shuleni ambapo ni lazima usome hata kama hupendi, na pili unachagua kipi cha kusoma na kipi cha kuacha, shuleni lazima usome vyote la sivyo utafeli mtihani.

Kitabu hiki ni kizuri sana na muhimu hasa kwa wakati huu ambapo wasomi ni wengi na nafasi za ajira ni chache. Ni muhimu kuwa na kitu ambacho kitakutofautisha na wewe, na kitu hiki unaweza kujifunza mwenyewe. Karibu twende pamoja na hapa nitakushirikisha mambo 20 muhimu sana niliyojifunza kwenye kitabu hiki.

1. Mfumo rasmi wa elimu una mapungufu mengi sana, na kila mtu anajua hili. Kuanzia shule ya awali mpaka vyuo vikuu, mambo yamekuwa mabovu kadiri miaka inavyozidi kwenda. Ufaulu unakwenda ukipungua kila siku, wasomi wanaozalishwa wanakuwa na uwezo mdogo wa kuzalisha. Na mbaya zaidi wanafunzi wanamaliza wakiwa na madeni makubwa ya kulipa huku wakiwa hawana uhakika wa ajira.

2. Njia ambayo inapata umaarufu sasa kwenye kujifunza ni kujifunza mwenyewe, hapa mtu anachagua kitu anachopenda kufanya, au anachopenda kujua kisha anachagua njia za kujifunza kitu hiko. Kuna ambao wanajifunza kwa kusoma vitabu hisika na kisha kufanya. Kuna ambao wanajifunza kwa kuangalia video za mafunzo na kuna ambao wanajifunza kwa kufanya na kukosea, na kuuliza wale ambao wamefanikiwa kwenye kitu wanachotaka kufanya.

3. Ukiacha fani kama udaktari na uanasheria, ambazo zinahitaji leseni za bodi maalumu ndio uweze kufanyia kazi unachojifunza, fani nyingine zote huhitaji degree ndio uwe mbobevu. Unachohitaji ni kupenda sana kile ambacho unafanya au unataka kufanya, na kujifunza kwa vitendo. Unaweza kujifunza na kuweza kufanya kwa ubora wa hali ya juu sana kuliko hata aliyekaa darasani na kusoma mpaka kufikia shahada za uzamivu. Kiu yako ya kujifunza, shauku yako ya kutaka kujua zaidi na juhudi zako za kufanyia kazi yale unayojifunza, vitakufikisha popote unapotaka kufika, na siyo degree kama wengi walivyokariri.

4. Tulipokuwa watoto wadogo tulikuwa tukishangazwa na kila kitu, tukiuliza maswali na kutaka kujua zaidi. Lakini kadiri tulivyokuwa tunakua jamii ilitubadili, na kutufanya tuache kuwa wadadisi na badala yake kupokea kila kinachokuja. Hali hii imeondoa kabisa ile shauku ya kujifunza ambayo inamsukuma mtu kujua zaidi anachotaka kujua bila hata ya kwenda shuleni.

5. Changamoto kubwa ya elimu rasmi ya darasani ni kwamba mkazo unawekwa kwenye kufaulu mtihani. Hivyo mwanafunzi atakazana kusoma sio apate utaalamu, badala yake afaulu mtihani. Hali hii inapelekea mtu anahitimu hana utaalamu wa kuionesha dunia, zaidi ya vyeti. Elimu binafsi ya kujifunza mwenyewe, unachagua kile unachopenda kujifunza na unaweka juhudi zako katika kujifunza na kufanyia kazi. Bila hata ya kuwa na cheti, dunia inaona matokeo yako mazuri.

6. Kadiri siku zinavyokwenda ndivyo umuhimu wa vyeti kwenye ajira unapungua. Sasa hivi makampuni mengi hayaangalii tu cheti alichonacho anayeomba kazi, bali wanaangalia uwezo wake binafsi, anaweza kufanya nini, ni thamani gani analeta kwenye kampuni. Tatizo ni kwamba thamani hii haifundishi kwenye mfumo rasmi wa elimu.

7. Katika kujifunza, kuna msukumo kutoka ndani na msukumo kutoka nje. Msukumo kutoka ndani ni kutaka kujua zaidi, kutaka kuwa bora zaidi na kutaka kufanya makubwa. msukumo huu unamfanya mtu ajifunze yeye mwenyewe na pia unamletea furaha kubwa. Msukumo kutoka nje ni kama zawadi ya ufaulu, cheti, kupata kazi na vingine. Msukumo huu unamfanya mtu kuwa kwenye hali ya kushindana na wengine na hivyo kumnyima furaha.

8. Pamoja na kwamba elimu ya kujifunza mwenyewe ndiyo bora, bado hatusemi elimu rasmi haina maana kabisa. Elimu rasmi bado ni muhimu kwa kuendelea kutengeneza mifumo ya kujifunza kama tafiti na hata mitaala. Kwa sababu hata wanaojifunza wenyewe bado wanahitaji mitaala na vitabu ambavyo vimepitishwa na mifumo rasmi ya elimu. Pia elimu rasmi inatengeneza jumuia ambazo watu mbalimbali mnakutana, kujifunza pamoja na baadae kuweza kufanya kazi pamoja. Lakini pamoja na elimu hii rasmi, ni lazima uchague kujifunza mwenyewe pia, hasa kwa yale ambayo ni muhimu sana kwako.

9. Njia nzuri sana ya kujifunza wewe mwenyewe ni kujifunza huku unafanya, hivyo yale unayojifunza yanakaa kwa muda mrefu. Na pia unaweza kuchagua kuwafundisha wengine kile ambacho umejifunza. Kwa njia hii unaelewa zaidi na unaweza kufanyia kazi kile ulichojifunza. Hivyo angalia njia bora kwako ni ipi, usiishie tu kusoma, soma na fanyia kazi, au soma na fundisha wengine.

10. Maisha yanabadilika kwa kasi sana, hivyo kujifunza vitu vipya kuhusu kazi au biashara yako ni hitaji la msingi. Hata kama una elimu kubwa kiasi gani, kama utaacha kujifunza, hutabaki kama ulivyo, badala yake utapotea. Ni muhimu sana kujifunza wewe mwenyewe. Chagua eneo lolote unalotaka kubobea, eneo unalotaka kuwa mtaalamu sana na anza kujifunza. Ni njia zipi za kujifunza tutaziona mbeleni.

11. Kitu chochote unachotaka kujifunza au kubobea, kuna watu wengine ambao tayari wamebobea. Na hivyo kazi yako kubwa ni kuwajua watu hawa na kujifunza kutoka kwao. Angali wamefikaje walipo, walipitia vitu gani, waliwezaje kuvuka changamoto na mengine mengi. Na mara nyingi watu hawa wako tayari kuwashirikisha wanaotaka kujifunza. Sema watu wengi hawapo tayari kuuliza na kujifunza. Uliza na jifunze, utapata chochote unachotaka.

12. Kitu chochote ambacho kinakupa changamoto kwenye kazi yako au biashara yako kwa sasa, unaweza kuondokana na changamoto hiyo kama utajifunza zaidi. Hakuna kitu ambacho hakijafundishwa au kuelezewa mpaka sasa katika mazingira ya kawaida ya kazi. Chagua kujifunza mwenyewe kuwa sehemu ya maisha yako, na utajikuta kila siku unabobea kwenye kile unachokifanya. JIFUNZE.

13. Unachohitaji kutoka nacho kwenye elimu yoyote ni utaalamu na ubobevu, sio cheti na deni. Elimu rasmi inawaandaa watu kuondoka na vyeti na madeni. Elimu isiyo rasmi inampa nafasi mtu ya kujifunza kile ambacho kitamwongezea ujuzi na ubobevu zaidi. Jifunze wewe mwenyewe, na hakuna kitakachokushinda.

14. Katika elimu yoyote ile, hata uwe na mwalimu mzuri kiasi gani, bado hataingiza maarifa kwenye kichwa chako moja kwa moja, ni lazima wewe mwenyewe uweke juhudi kwenye kujifunza, usome vitabu, usikilize mwalimu anapofunzisha kwa umakini na ufikiri kwa kina. Tofauti ya elimu rasmi na ya kujifunza mwenyewe ni, kwenye alimu rasmi utalazimika kusoma vitu ambavyo sio muhimu kwako, kwenye elimu isiyo rasmi unachagua kipi muhimu kwako kujifunza.

15. Njia nyingine bora sana ya kujifunza mwenyewe ni kuzungukwa na watu ambao wanajua, watu ambao wana ujuzi mkubwa kwenye kile wanachofanya. Kwa kuzungukwa na watu hawa, mara zote utapata nafasi ya kuuliza na kujibiwa, na pia utaona wanavyofanya mambo yao, kitu ambacho kitakuhamasisha zaidi. Ila kama utazungukwa na watu wenye uwezo mdogo, watu ambao wewe umewazidi ujuzi, ni rahisi sana kujisahau na kushindwa kujifunza makubwa zaidi.

16. Kama unataka kujifunza biashara, huna haja ya kupata shahada ya biashara, badala yake ni kujua maeneo gani ambayo ni muhimu sana kwenye biashara. Na haya ni kama usimamizi, fedha, rasilimali watu, huduma kwa wateja, mauzo na masoko. Sasa hapa wewe mwenyewe unachagua unajifunzaje maeneo hayo muhimu. Unaweza kujifunza kwa kujisomea vitabu, kusikiliza vitabu, kuhudhuria semina, kuangalia wafanyabiashara wengine wanavyofanya. Unachohitaji wewe ni kiu ya kujifunza na shauku ya kufanyia kazi unayojifunza.

17. Ujio wa kompyuta na ukuaji wa mtandao wa intaneti, umefanya kujifunza kuwe rahisi kuliko kipindi chochote tumewahi kupitia. Hakuna kitu unachotaka kujifunza ambacho utakitafuta kwenye mtandao ukose kabisa. Kila kitu kipo kwenye mtandao, watu walishafanya na wakashirikisha kwenye mtandao, ni wewe mwenyewe tu ugome kujifunza.

18. Ni njia zipi unaweza kuzitumia kujifunza wewe mwenyewe? Njia za kujifunza zipo nyingi sana, inategemea na wewe mwenyewe ni njia ipi unaipendelea ambayo unaelewa sana. Ya msingi kabisa ni kusoma vitabu na maandiko mengine yanayohusiana na kile unachotaka kujifunza. Njia nyingine ni kujifunza kupitia mtandao wa intaneti ambapo kwa sasa kuna mitandao inatoa mafunzo mengi kwa njia ya mtandao. Njia nyingine ni kuangalia video au kusikiliza vitabu vilivyosomwa. Pia unaweza kujifunza kwa kuangalia wengine wanafanya nini na wewe ukafanya. Na njia nyingine ambayo ni ndefu ni kufanya na kushindwa. Chagua njia ipi bora kwako na anza kujifunza.

19. Ukishachagua njia ya kujifunza unaanzia wapi? Hili ni swali muhimu sana. Ni lazima uwe na mahali pa kuanzia, ujue ni vitabu vipi muhimu kusoma, au kozi zipi muhimu kuzisoma. Na hapa unaweza kuanza kwa kutafuta kwenye mtandao wa google, tafuta kuhusu kile unachotaka kujifunza. Andika kwenye mtandao wa google kile unachotaka kujifunza na utapelekwa kwenye mitandao yenye maelezo zaidi. Pia unaweza kutafuta kwenye mtandao wa wikipedia, huu ni mtandao wenye taarifa nyingi sana hasa za kitaalamu. Hapa utapata kujua kuhusu kile unachotaka kujifunza. Pia unaweza kusoma machapisho ya tafiti zilizofanywa kwenye eneo unalotaka kujifunza. Ukishapata mwanga utajua ni hatua gani za kufuata.

20. Njia bora kabisa ya kuhakikisha unakuwa na hamasa ya kujifunza wakati wote ni kuwa na kikundi cha watu ambao unajifunza nao, ambao wote mnakwenda kwa kasi moja. Hapa utajisukuma kujifunza hata kama hujisikii ili usiwarudishe wengine nyuma.

Njia nyingine nzuri ni kufundisha kile unachojifunza. Na njia rahisi kufanya hivyo ni kuwa na blog ambapo unawashirikisha wengine yale unayojifunza. Hapa utajisukuma kujifunza zaidi kwa sababu unajua kuna watu wanasubiri kusikia kutoka kwako. Kama utataka kuwa na blog yako tuwasiliane.

Sasa tumeingia rasmi kwenye ulimwengu ambao kujifunza kila siku na kila mara ndio hitaji la msingi sana. Na kujifunza sio lazima urudi shuleni, bali kujifunza wewe mwenyewe ndiyo njia bora sana ya kujua chochote unachotaka kujua. Chukua hatua sasa ili uboreshe kazi yako na biashara yako pia.

Kila la kheri.