Binadamu sisi ni viumbe wa kijamii, tunapenda kuwa sehemu ya jamii na ili kuwa sehemu ya jamii tunalazimika kufanya yale ambayo jamii imezoea kufanya.

Katika hali hii tunajikuta tunalazimika kufanya kitu sio kwa sababu tunapenda, au kwa sababu tunajua maana yake ila tu kwa sababu kila mtu anafanya.

Sasa hakuna kitu kinachokurudisha nyuma kama kufanya kitu kwa sababu kila mtu anafanya. Kwa sababu hapa unajizuia kukua, unajizuia kuhoji na unajizuia kujua zaidi. Unalazimika kufanya vitu ambavyo siyo muhimu kwako na wala havina mchango wowote kwenye mafanikio yako.

Na mbaya zaidi vile vitu ambavyo vinafanywa na kila mtu, huwa havina thamani kubwa na mara nyingi huwa siyo vitu sahihi, hasa kwako wewe ambaye unataka kuwa na maisha bora na ya mafanikio.

Ufanye nini?

Usifanye kitu chochote kwa sababu tu kila mtu anafanya, fanya kile ambacho ni muhimu kwako. Hoji kila kitu mpaka upate ukweli halisi kwa nini watu wanafanya na kwa nini na wewe pia ufanye.

Na pia usiogope kwamba kama utafanya tofauti na wengine basi utakosa watu wa kukuunga mkono kwenye jamii. Kuna wenye mtizamo kama wako ila tu hawajapata wengine wenye mtazamo huo. Anza kufanya kile ambacho ni muhimu kwako na utapata waliomuhimu wa kuambatana nao.

SOMA; Habari Za Kusikitisha; Kila Kitu Kinabadilika…

TAMKO LANGU;

Nimejifunza ya kwamba mambo mengi ninayofanya ni kwa sababu kila mtu anafanya na haya siyo mazuri kwangu kufanya. Kuanzia sasa nitaanza kuhoji chochote ninachofanya, ili nijue ni kwa nini hasa nafanya na ninafaidika vipi kwa kufanya, na sio kufanya tu kwa mazoea.

NENO LA LEO.

“Because everyone is doing it doesn’t make it right and because you stand out doesn’t make it wrong. Just find a path that you can defend.”

― Temi ‘T Quest’ Sholeye

Kwa sababu kila mtu anafanya, haifanyi kitu kuwa sahihi, na kwa sababu wewe unatofautiana na wengine haifanyi kitu kutokuwa sahihi. Tafuta njia ambayo unaweza kuitetea.

Usikubali kufanya kitu kwa sababu kila mtu anafanya, fanya kile ambacho unajua ni muhimu kwako na wanaokuzunguka. Hoji kila unachofanya.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.