Tumekuwa tunakutana na migogoro mingi sana kwenye maisha yetu, migogoro ya ngazi ya chini baina ya watu na hata migogoro ya ngazi za juu kabisa ambayo inapelekea mpaka vita.
Migogoro hii inakuwa hatari sana kwa maendeleo na mafanikio yetu kwa sababu inavuruga kabisa mahusiano yetu na kushirikiana kwetu na wengine. Na kama tunavyojua, maendeleo na mafanikio yetu yanategemea sana wengine.
Kuna sababu nyingi sana za migogoro kutokea, iwe ni baina yako na watu wako wa karibu au baina ya makundi mbalimbali au hata baina ya mataifa. Ila kuna chanzo kikuu cha migogoro yoyote inayotokea popote. Leo hapa tutajifunza chanzo hiki na jinsi ya kuondokana nacho ili kuepuka migogoro.
Chanzo kikuu cha migogoro yote ni mgawanyiko unaotokea baina ya watu, au baina ya makundi au baina ya mataifa. Kunapotokea mgawanyiko, kwamba mimi ni mimi na wewe ni wewe, au sisi ni sisi na nyinyi ni nyinyi, hapa lazima kuibuke mgogoro.
Katika mgawanyiko wowote, ndipo kila upande unapotaka kuonesha kwamba ni bora kuliko wengine, iwe ni watu wa wili, au dini mbili, au vikundi viwili au mataifa mawili. Na ili kudhibitisha ni nani aliye bora, basi mgogoro unaibuka na mapambano yanatokea.
Katika migogoro na mapambano haya, wote wanaishia kupata hasara au kuumia. Na hivyo hakuna anayenufaika.
Kitu muhimu sana cha kuzingatia ili kuepuka mgawanyiko, na migogoro pia ni kukubali kwamba sisi wote ni kitu kimoja. Tukubali kwamba tunatofautiana, lakini wote tuna lengo moja, la kufanya maisha yetu kuwa bora zaidi. Na hivyo tuwe tayari kubadilika na kurekebishana pale ambapo mienendo yetu inakuwa siyo mizuri katika kufanyia kazi malengo yetu.
SOMA; Matatizo Yote Kwenye Maisha Yako Yanatokana Na Kitu Hiki.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba migogoro inaanzia kwenye migawanyiko baina ya watu, vikundi au mataifa. Na njia bora ya kuepuka migogoro na migawanyiko, ni kujua kwamba sisi wote ni wamoja na wote tunapigania kuwa na maisha bora, na tunatofautiana katika hilo. Kukubali wengine kwa vile walivyo, na kila mmoja wetu kuwa tayari kubadilika, ni njia bora ya kuondokana na mgawanyiko na migogoro pia.
NENO LA LEO.
Peace is not absence of conflict, it is the ability to handle conflict by peaceful means.
Ronald Reagan
Amani sio kutokuwepo kabisa kwa migogoro, bali kuweza kuimaliza migogoro kwa njia za amani.
Migogoro inatokana na migawanyiko inayokuwepo baina ya watu. Kuweza kuondoa migawanyiko ni njia bora ya kuepuka au kutatua migogoro.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.