Kazi ndiyo msingi wa mafanikio, na sio kazi yoyote tu, bali kazi bora kwa yule mtu ambaye anaifanya. Na kama ilivyo kwa jambo lolote kwenye maisha, hakuna kazi au biashara ambayo ni bora kwa watu wote. Kazi ambayo ni bora kwako inaweza kuwa hovyo kwa mwingine.

Watu wote ambao wameweza kufikia mafanikio makubwa ni watu wa kufanya kazi au biashara zao kwa juhudi kubwa na maarifa pia. Kwa kuangalia kwa nje tunaweza kuona kama wanateseka na kuumia ila kwa ndani yao ni tofauti kabisa. Na pia watu wengi wamekuwa wakiweka juhudi kubwa kwenye kazi au biashara zao lakini hawaoni matokeo makubwa. hii inasababishwa na nini?

Kuna viungo vitatu muhimu sana vya kazi au biashara ambayo itamletea mtu mafanikio. Leo tutajifunza viungo hivi na unavyoweza kuvitumia kwenye kazi au biashara yako.

Kiungo cha kwanza ni raha unayoipata kwa kufanya kazi au biashara hiyo. Hiki ni kiungo muhimu sana kwa sababu kama kitu hakikupi raha kufanya, hutasukumwa kukifanya kwa muda mrefu. Binadamu wote tunapenda raha na tunapoweza kuipata kwenye kazi, tutaipenda sana kazi hiyo.

Kiungo cha pili ni dhumuni kubwa la wewe kufanya kazi au biashara hiyo. Kupata tu raha kutoka kwenye kazi unayofanya bado hakutoshi, unahitaji kuwa na dhumuni kubwa linalokusukuma kufanya kazi hiyo. Na dhumuni hili sio tu kupata fedha, bali kutoa mchango wako kwa wengine. Kuwasaidia wengine kuondokana na matatizo waliyonayo au kuwapatia kile ambacho wanakikosa. Ni muhimu utoe mchango mkubwa kwa wengine kupitia kile unachofanya na hii itakusukuma zaidi.

Kiungo cha tatu ni kubobea kwenye kazi au biashara unayoifanya. Kama kile unachokifanya unakijua vizuri basi utapata msukumo wa kuendelea kufanya kwa sababu unajua utatoa majibu mazuri. Lakini kama hujui vizuri utakuwa na shaka na hivyo kuogopa kufanya.

Hivyo ndivyo viungo vitatu vya kazi bora kwako, kupata raha wakati unaifanya, kuwa na dhumuni kubwa na kubobea kwenye kazi hiyo.

Je kazi au biashara unayofanya sasa inakupa viungo hivi vitatu? Kama jibu ni ndiyo kivipi na kama jibu siyo una mpango gani? Tushirikishane kwenye maoni hapo chini.

SOMA; Dakika 20 Kwa Siku Zinakutosha Kuwa Bora Duniani(WORLD CLASS)

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba hakuna kazi bora kwa watu wote. Na kazi bora kwangu ni ile ninayopata raha kwenye kuifanya, inaniwezesha kufikia dhumuni langu kubwa kwenye maisha, na nimebobea vizuri kwenye kuifanya.

NENO LA LEO.

“Nobody in life gets exactly what they thought they were going to get. But if you work really hard and you’re kind, amazing things will happen.” – Conan O’Brien

Hakuna mtu anayepata kila anachokitaka kwenye maisha. Lakini kama ukifanya kazi kwa juhudi kubwa na ukawa mwema, vitu vya kushangaza vitatokea kwenye maisha yako.

Kazi bora kwako kufanya ni ile inayokupa raha, inayokuwezesha kufikia dhumuni lako la maisha, na uliyobobea kuifanya.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.