Kwenye makala iliyopita ya BISHARA LEO, tuliona ni muhimu sana kuepuka kuweka bei kubwa ili wateja watakapotaka kupunguziwa ndiyo unampunguzia kufikia bei ya kawaida. Tukaona ni muhimu uwe na bei moja ambayo haipungui na kila mteja ataambiwa bei hiyo. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala ile bonyeza maandishi haya kuisoma; Jambo Muhimu Kuzingatia Kwenye Bei Ya Bidhaa Au Huduma Unazotoa.

Changamoto inakuja kwamba wateja wengi wameshazoea kupunguziwa bei, na hivyo wanategemea kila kitu kipungue bei. Je unafanya nini pale ambapo mteja anataka umpunguzie bei kupitiliza kiwango chako wewe ulichoweka?

Suluhisho hapa siyo wewe kukubaliana na mteja na kushusha bei, unachotaka ni mteja kununua kwa bei uliyopanga, na hapa ndipo unapohitaji ushawishi mzuri utakaomfanya mteja kununua huku akiendelea kujenga uaminifu mkubwa kwako.

Mteja anapotaka kupunguziwa bei zaidi, usikazane kubisha bei, bali mpe faida zaidi za kununua kitu hiko kwa bei hiyo uliyomtajia. Mwoneshe ni faida gani anazipata kwa kununua kwako. Labda ni uhakika, kwamba akikuta kina matatizo anaweza kurudisha, au atapata huduma bora na vingine vingi.

Na ikiwa mteja atasisitiza bei ya chini zaidi, kwamba kuna wengine wanauza chini, endelea kumuonesha ni jinsi gani kununua kwako kutakuwa na faida zaidi kwake. Kumbuka unapofanya yote haya uwe na bidhaa au huduma ambayo ni bora kweli na unaamini kabisa itakwenda kumsaidia mteja wako.

Iongelee biashara yako kwa minajili ya mteja ananufaikaje, na sio kukazania bei kubwa au ndogo. Ukiweza kulijua tatizo la mteja na jinsi bidhaa au huduma yako inaweza kumsaidia, bei haiwezi kuwa tena tatizo.

Kila la kheri.

MUHIMU; Kama una swali, maoni au changamoto yoyote ya kibiashara, weka kwenye maoni hapo chini na tutajadiliana zaidi na kama itahitajika nitaandaa makala ya kuhusu jambo hilo kwenye makala zijazo.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz