Kwako rafiki yangu ambaye ni mwandishi kupitia mitandao hii ya kijamii.
Kwanza nikupe pongezi kubwa, kwa sababu kuandika, hasa kama unafanya mara kwa mara au kila siku, siyo kitu rahisi. Japo kuna ambao kwa nje wanaona ni rahisi sana. Lakini sio kitu rahisi ila unafanya kwa sababu unapenda wengine wanufaike na kile unachojua au ambacho una uzoefu nacho. Hongera sana kwa moyo wako huo mkuu.
Pili najua ya kwamba siyo rahisi kunufaika moja kwa moja kwa yale unayoandika kupitia mitandao hii ya kijamii. Lakini pia haikufanyi usinufaike kabisa na kazi zako. Kwa sababu usiponufaika wewe, kuna wenzako wananufaika sana kupitia kazi unayotolea jasho na kuumiza akili.
Hivyo basi, nimechukua nafasi hii nikukumbushe kwamba licha ya kuwashirikisha wengine maandiko yako kupitia mitandao ya kijamii kama facebook, wasap na mingine, hakikisha umejenga nyumba yako kwanza, ambapo vitu vyote vinaanzia hapo ndiyo vinaenda kwenye mitandao. Na nyumba ninayozungumzia hapa ni uwe na BLOG yako au hata TOVUTI. Hii itakuwa rahisi sana kwako kuendelea kutumia kazi zako za nyuma.
Kwenye mitandao ya kijamii kama facebook na wasap, leo huwezi kunionesha ulichopost mwaka mmoja uliopita na hata ukinionesha bado wengi hawawezi kukiona. Ila unapokuwa na blog au tovuti, unaweza kuchagua tu siku ya hata miaka mitatu iliyopita na ukanionesha ulipost nini na kwa wakati gani.
Kingine kuna watanzania wenzetu ambao wanakusubiri wewe upost, hawatalike, wala hawataweka komenti, ila watakachofanya wanaibeba kama ilivyo na kubadili jina lako kisha kuweka lake na kuanza kuisambaza. Yaani ndani ya dakika moja anajimilikisha kazi iliyokutumia muda kuandaa.
Lakini unapokuwa na nyumba yako, hata akikopi, bado wewe utabaki kuwa mmiliki. Kwa sababu mitandao inajua kuchuja habari imewekwa kwenye mtandao upi kwanza.
Hivyo nakusisitiza sana wewe kama rafiki yangu, kama unapenda kuandika, basi cha kwanza kuwa na BLOG na kama huna na hujui uanzie wapi tunaweza kuwasiliana na tukasaidiana kwenye hilo.
Kuandika ni kitu nilichochagua kufanya kila siku, kwa siku zote za maisha yangu. Napenda sana kila anayeandika, maana jamii yetu inakosa maarifa muhimu ya mtu kuweza kujikwamua.
Nikutakie kila la kheri.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,