Bado kuna watu wengi sana ambao wanashindwa kuingia kwenye biashara kwa sababu bado hawajapata wazo bora na la kipekee kwao.

Kama na wewe ni mmoja wa watu hawa naomba nikupe taarifa leo ya kwamba unajidanganya na unapoteza muda wako bure.

Huhitaji kuwa na wazo jipya kabisa na la kipekee ndio uweze kuingia kwenye biashara. Unahitaji kuanza na wazo lolote, hata ambalo tayari linafanyika na wewe upo tayari kuweka juhudi kubwa kwenye wazo lako.

Lakini pia unapochukua wazo ambalo tayari linafanyika usiige kila kitu, maana hapo napo utakuwa unajidanganya.

Ukweli ni kwamba watu hawapendi sana vitu ambavyo ni vipya kabisa, na wala hawajali sana kuhusu upya wa kitu. Wanachojali ni je kitawasaidia kukatua matatizo yao? Je kitawawezesha kupata kile wanachotaka?

Hivyo acha kupoteza muda kutafuta upya na badala yake wekeza nguvu zako kuanza na chochote na kukazana kukifanya kuwa bora zaidi.

Hii inafaa pia hata kama tayari upo kwenye biashara, usitake kuleta mapinduzi makubwa sana kwenye biashara yako, unachohitaji ni kuiboresha kila siku. Kila siku angalia ni jinsi gani ya kufanya maisha ya mteja wako kuwa bora zaidi kupitia biashara yako.

Na kila siku utapata wateja wengi, wapya kwa wa zamani.

Kila la kheri.

MUHIMU; Kama una swali, maoni au changamoto yoyote ya kibiashara, weka kwenye maoni hapo chini na tutajadiliana zaidi na kama itahitajika nitaandaa makala ya kuhusu jambo hilo kwenye makala zijazo.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz