Unaposikia neno maamuzi unapata picha gani kwenye mawazo yako? maana kwa kila neno lazima kuna picha unaipata, je wewe ni picha ipi unaipata unaposikia neno maamuzi? Utatushirikisha kwa kuweka maoni yako hapo chini.

Pamoja na picha unayoipata iwe ni ya uhalisia au la, maana halisi ya maamuzi ni kwamba umelifikiria jambo kwa kina, umejua faida na hasara zake na umekubaliana na nafsi yako kwamba utachukua hatua fulani na upo tayari kwa lolote litakalotokea kutokana na hatua uliyochukua.

Je kwa kusikia hili picha yako ya maamuzi imebadilika? Kwa nafasi kubwa ni lazima ibadilike kwa sababu wengi tumekuwa tunafikiri maamuzi ni kuchagua tu kitu.

Kuanzia leo naamua sinywi tena pombe siku chache baadaye uko na marafiki zako na mnakunywa kwa pamoja.

Au kuanzia leo nimeamua sitopoteza tena muda wangu kwa mambo yasiyo muhimu, dakika chache baadae upo facebook kufuatilia maisha ya wengine ambayo hata siyo ya kweli.

Au kuanzia leo nimeamua sitaki tena mahusiano ya kimapenzi na mtu yeyote, miezi michache baadaye upo kwenye mapenzi motomoto na unamwambia umpendaye hakuna kama yeye.

Mara nyingi umekuwa unashindwa kufanya maamuzi imara na kuyasimamia kwa sababu unakuwa hujafikiri kwa kina, hujajua faida na madhara ya maamuzi yako, na hujajua utazivukaje changamoto utakazokutana nazo. Na mbaya zaidi unajikuta unafanya maamuzi ukiwa na hisia kazi za furaha, hofu, kuumizwa na nyingine.

Tatuzo kubwa kwenye kufanya maamuzi ni kwamba wengi wanakuwa hawajajipanga na hivyo kuchagua kimoja, na baadaye kurudi nyuma na kuchagua tena kingine.

Tukubaliane leo ya kwamba kabla hatujafanya maamuzi tutalifikiri jambo kwa kina, tutajua faida na hasara zake, tutajua changamoto tunazohitaji kuvuka na tutaamua tupo tayari kwa lolote litakalotokea.

Lakini usitumie kufikiri kama njia ya kutoroka kufanya maamuzi. Maana kuna wanaofikiri mpaka wanapotea kabisa kwenye kufanya maamuzi.

Na kumbuka mafanikio kwenye maisha yanaanza na maamuzi. Fanya maamuzi bora kwao na yasimamie mpaka utakapopata unachotaka.

SOMA; Usifanye Maamuzi Yako Kwa Kigezo Hiki, Utajuta Sana…

TAMKO LANGU;

Nimejikumbusha ya kwamba maamuzi siyo tu kuchagua kimoja kati ya vingi, bali kufikiri kwa kina kila chaguo, kujua faida na hasara za kila chaguo utakalofanya, kujua changamoto utakazokutana nazo na kuamua kufanya na kutokukubali kurudi nyuma.

NENO LA LEO.

A good decision is based on knowledge and not on numbers. – Plato

Maamuzi bora ni yale yanayofanyika kwenye msingi wa maarifa/ujuzi na siyo kwenye msingi wa namba.

Jua kwa hakika ni zipi faida na hasara, ni zipi changamoto kabla hujafanya maamuzi na ukishafanya maamuzi yasimamie mpaka mwisho.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.