Moja ya misingi muhimu sana ambayo tumejifunza kwenye FALSAFA YETU MPYA YA MAISHA ni upendo. Upendo ni msingi muhimu sana na ndio kitu pekee kinachoweza kutuvusha na kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi. Bila ya upendo maisha hayawezi kuwepo, na matatizo mengi tunayopitia sasa kama dunia yanatokana na ukosefu wa upendo.
Upendo unaanzia ngazi ya chini kabisa kati ya mtu mmoja na mwingine, kisha unakwenda ngazi ya familia moja na nyingine, jamii moja na nyingine, kikundi kimoja na kingine, na hatimaye taifa moja na jingine.
Leo katika makala yetu hii ya FALSAFA MPYA YA MAISHA tutajadili njia bora sana ya kujenga upendo baina ya watu wawili, fanilia mbili, makundi mawili na hata mataifa mawili na hata zaidi ya pande mbili. Kwa njia hii tutaona ni jinsi gani nguvu ya upendo ipo ndani ya kila mmoja wetu na ni uamuzi wetu tu kuitumia nguvu hii.
Njia bora sana ya kujenga upendo wako kwa wengine ni kuwakubali kama walivyo. Ili kuwapenda watu kweli unahitaji kuwakubali kama walivyo.
Wote tunajua ya kwamba watu tunatofautiana, hata mapacha wa kufanana bado wanatofautiana. Tofauti zetu zinatokana na tabia zetu, vipaji vyetu, malezi yetu, dini zetu, rangi zetu na hata maeneo tunayoishi. Hizi ni tofauti za juu sana kwani haziathiri ule utu wetu.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Nguvu Moja Unayomiliki Yenye Uwezo Wa Kuibadili Dunia.
Lakini tofauti hizi zimekuwa zikitumika kutugawa. Kwamba huyu ni wa dini fulani hawezi kuwa sawa na sisi, huyu ni wa rangi fulani hawezi kuwa sawa na sisi na kwa njia hii upendo unavunjika.
Ili kujenga upendo, ni lazima tuzione tofauti hizi zilizopo baina yetu, na kuendelea kuwa pamoja licha ya tofauti hizi. Hatujaribu kuziondoa tofauti, kwa sababu kufanya hivyo ni kuharibu zaidi, badala yake tunazielewa tofauti hizi na kuweza kuishi licha ya kuwa na tofauti hizi.
Tunawezaje kuwakubali wengine kama walivyo?
Hii siyo kazi rahisi hasa kwa dunia ambayo tunaishi, kwa sababu tumekuzwa kwenye mazingira ya kuzionesha wazi tofauti zetu, na wakati mwingine kutumia tofauti hizi kujiona kwamba ni bora kuliko wengine, au ni hovyo kuliko wengine.
Kwa mfano tukiangalia kwa upande wa rangi, tayari tumejengewa kwenye akili zetu kwamba wenye rangi nyeupe ni bora kuliko wenye rangi nyeusi. Tofauti hii inavunja upendo kati ya makundi haya na hivyo kukosa hali ya kuaminiana na kuweza kufurahia maisha kwa usawa.
Tukiangalia upande wa dini pia, kumekuwa na mgawanyiko mkubwa sana, wa dini moja anajiona ni bora zaidi na yupo sahihi zaidi wa yule anayeamini dini tofauti. Kwa mtazamo huu dini zimeleta mgawanyiko mkubwa na kuzuia baadhi ya watu kuweza kushirikiana pamoja kwa upendo.
Pamoja na kupitia mazingira haya ya kujenga tofauti, bado tunaweza kuziondoa tofauti hizi na kuwakubali watu kama walivyo. Haya hapa ni mambo muhimu kwa kila mmoja wetu kufanya ili kuweza kuwakubali wengine kama walivyo.
1. Elewa kwamba tofauti zipo na zitaendelea kuwepo.
Hata kama kungekuwa na watu wa rangi moja tu duniani, bado tofauti zingekuwepo baina ya watu hawa. Hata kama ingepitishwa amri kwamba dini inapaswa kuwa moja tu duniani, bado kungekuwa na tofauti ndani ya dini hiyo moja. Hivyo badala ya kukazana kupinga tofauti, ni vyema wote tukaelewa kwamba tofauti zipo na zitaendelea kuwepo.
Haiwezi kutokea wote tukafikiri na kutenda sawa, haiwezi kutokea kamwe. Tunaelewa tofauti, tunapendelea vitu tofauti na tuna mitazamo tofauti. Kubali hili kwa wengine na maisha yatakuwa rahisi sana.
2. Jikubali wewe mwenyewe kwanza.
Njia nyingine ya kuwakubali wengine kama walivyo ni kwa kuanza kujikubali wewe kwanza. Turudi kwenye uhalisia wa maisha, wengi tumekuwa tunakazana kuishi maisha ya maigizo, kufanya kile ambacho labda wengine watafurahia lakini ndani yetu siyo tunachotaka kufanya.
Unapokuwa na maisha haya ya maigizo na wewe unategemea wengine pia waigize na wanaposhindwa kufanya hivyo utaishia kupata hasira na kuvunjika kwa upendo. Lakini utakapojikubali wewe mwenyewe kwa kufanya yale ambayo ni muhimu kwako, unafurahia na kwa njia hii utawapa wengine uhuru wa kufanya kile ambacho wanakipenda.
Kama wewe mwenyewe hujajikubali, huwezi kuwakubali wengine. Kama wewe mwenyewe hujajipenda, huwezi kuwapenda wengine. Na unapojikubali ndiyo hatua ya kwanza kabisa ya upendo.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Upacha wa dunia na jinsi ya kuutumia kuwa na maisha bora.
3. Angalia upande chanya.
Katika kila anachofanya mwingine, hata kama hukubaliani nacho, kuna upande chanya na upande hasi. Ni vyema wewe ukaangalia zaidi ule upande chanya, hii itakupelekea kukubali na hata wao watasisitiza zaidi kwenye ule upande chanya.
Kwa mfano wote tunajua dini tofauti zina falsafa tofauti na katika falsafa hizi kuna mambo mazuri na mambo mabaya zaidi. Badala ya kukazana na yale mabaya, ingekuwa bora sana kama tungewaangalia wengine kwa yale mazuri waliyonayo na hapa tungejikuta tunakutana kwa falsafa ambayo ni bora zaidi kwetu.
Hakuna kitu ambacho ni kibaya tuu au kizuri tuu, bali mtazamo wetu wenyewe, kwa kile tunachowekea mkazo ndio tunachagua uzuri au ubaya.
4. Usihukumu.
Huenda hili ni gumu kuliko yote, lakini kama umechagua kuishi maisha haya ya falsafa, basi huna budi kufanya yaliyo magumu.
Nasema hili ni gumu kwa sababu sisi binadamu ni viumbe wa kuhukumu. Tunahukumu kila kitu na kila wakati. Tunahukumu mtu kabla hata hatujapata taarifa kamili. Tunahukumu mtu kwa kumwangalia tu hata kabla hajazungumza chochote. Tunahukumu kwa kusikia tu. Na mbaya zaidi tunahukumu watu ambao hata hatuwajui, hatujawahi kuwaona, hatujui wanapitia nini, lakini kwa kuwa tumesikia kitu kimoja tu walichofanya, tayari tunakuja na hukumu zetu.
Ili kuweza kuwakubali watu kama walivyo, ni lazima uache kuhukumu. Angalia mambo kama yalivyo, kuwa mtu wa kujifunza na usikimbilie kuchukua upande wowote. Na kama unahitaji kuchukua upande basi jiridhishe kwanza kwa taarifa sahihi kisha kuchukua maamuzi.
Unapokuwa mtu wa kuhukumu, hasa kwa kasi ambayo kila mtu anatumia kuhukumu, huwezi kuwakubali watu kama walivyo.
5. Ishi sasa.
Hii ni dawa kwenye changamoto yoyote unayopitia kwenye maisha yako. ISHI SASA. Sasa hivi hapo ulipo, kwa kile unachofanya, ndiyo muhimu zaidi. Mtu unayekutana naye sasa, kwa kile anachofanya sasa au mnachofanya sasa ndiyo muhimu. Usianze kuja na hadithi zako za miaka iliyopita kwamba huyu alifanya hivi na hivi na hivyo hafai kabisa. Una uhakika gani? Unajuaje kama kweli hajabadilika? Kwa kuishi sasa, unampa mtu nafasi ya kutoa kile bora alichonacho sasa. Lakini utakapoanza kumhukumu kwa yaliyopita, utamzuia kutoa alichonacho na pia utaondoa upendo.
Na katika kuishi sasa pia epuka kusumbuliwa na hofu za baadaye. Ile hali kwamba labda mtu atakugeuka, labda mambo hayatakwenda vizuri kama unavyotegemea. Kwa hofu hizi za mambo ambayo hata bado hayajatokea zinakuzuia wewe kuwa na mahusiano bora na wengine na kuondoa upendo baina yako na wengine.
Upendo ndiyo nguzo kuu inayofanya dunia iendelee kuwepo. Tunajikuta kwenye migogoro mingi pale tunapokuwa na makundi yanayokuza tofauti zetu. Njia bora kabisa kwa sisi kuendelea kuwa na upendo ni kuzielewa tofauti zetu na kukubaliana kama tulivyo. Wakubali watu kwa vile walivyo na upendo utajengeka baina yako na wengine.
Tutumie msingi huu kuboresha maisha yetu, kama lilivyo lengo la FALSAFA MPYA YA MAISHA, kuwa na maisha bora, ya furaha na mafanikio makubwa. na haya yote yanaanzia ndani yetu.
Rafiki na Kocha wetu,
Makirita Amani,