Karibu tena rafiki kwenye kipengele chetu cha ushauri wa changamoto mbalimbali tunazokutana nazo kwenye safari yetu ya mafanikio. Changamoto ni sehemu ya maisha yetu na hivyo hatupaswi kuzikimbia bali kuzikaribisha na kuzitumia ili kufika kule tunakotaka.
Leo katika kipengele hiki cha ushauri tutaangalia changamoto moja ambayo inawazuia watu wengi sana kuweza kufikisha ujumbe, kushawishi au kuzitumia fursa zinazopatikana kupitia watu wengine.
Changamoto hii ni hofu ya kuongea mbele ya wengine. Kuna hofu nyingi sana, ila hofu ya kuongea mbele ya wengine ni hofu kubwa na inaathiri wengi, kuna watu wapo tayari wang’olewe jino bila ya ganzi kuliko kuongea mbele ya wengine. Wengine wapo tayari kuzikwa wakiwa hai lakini sio kuongea mbele ya wengine. Hii ni hofu kubwa sana na ina madhara makubwa.
Kama ambavyo wote tunajua, mafanikio yetu yanatokana na wengine. Chochote unachotaka sasa hivi kipo kwa mwingine. Na hivyo unavyoweza kuwasiliana vizuri na wengine, na kuweza kuwashawishi ni rahisi zaidi kwako kupata chochote unachotaka.
Sasa hofu inapokuwa kubwa unashindwa kuwasilisha kwa wengine kile ambacho ulitaka kuwasilisha na hivyo unakosa fursa kubwa.

http://www.amkamtanzania.com/p/kuwa-tajiri.html

 
Je ufanye nini ili kuondokana na hofu hii?
Kabla hatujaangalia hilo kwa undani, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili.

Changamoto yangu ni huwa najikuta kuwa Mimi ni mtu wa kukata tamaa na huwa na woga hata kumfuata MTU kumshirikisha ninachokifanya najikuta natetemeka sijui nini tatizo. Innocent P. J.

Kama ambavyo tumeona kwa msomaji mwenzetu hapa, na huenda imeshatokea kwako, unakosa kabisa kujiamini pale ambapo umepata fursa ya kumwambia mtu kile unachofanya. Labda ni mtu mwenye ushawishi au ambaye angeweza kukusaidia zaidi, anakuambia nieleze unachofanya, ukiwa mwenyewe unajua vizuri kabisa, ila katika hali hii unajikuta unasahau, unajikuta unatetemeka na mwishowe kuonekana haupo makini na kile unachofanya au kile unachotaka.
Unaweza kuondokana na hali hii na ukaweza kujiamini na kuzitumia vizuri fursa kama hizi. Yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia ili kuondokana na hali hii.
1. Jua vizuri unachofanya, na weza kukielezea kwa lugha rahisi sana.
Moja ya vitu vinavyowaondolea watu wengi kujiamini ni kutokujua vizuri kile ambacho wanakifanya. Kwa kutokujua vizuri mara zote huwa na wasiwasi kwamba wengine watajua kwamba hayuko vizuri. Wasiwasi huu unamwondolea kujiamini na hivyo kushindwa kusema kwa hakika ni kitu gani anachofanya.
Na hata baada ya kujua vizuri kile wanachofanya, wengine bado wanashindwa kusema kwa wengine kwa sababu wanatafuta lugha ngumu ya kusema kitu hiko ili waonekane kweli wanafanya kitu muhimu. Kwa kutafuta namna hiyo ngumu wanazidi kujiondolea kujiamini na kushindwa kuwasilisha kwa wengine. Dawa ya hali hii ni kutafuta lugha rahisi sana ya kuelezea kile unachofanya, kwa lugha ambayo mtoto wa darasa la tano au bibi yako mzee sana anaweza kukuelewa. Kama huwezi kuelezea unachofanya kwa lugha rahisi hivyo, hutaweza kukielezea kwa kujiamini mbele za wengine.
2. Ishinde hofu ya kukataliwa.
Kitu kingine kikubwa sana kinachowazuia watu kuweza kusema kitu mbele ya wengine ni hofu ya kukataliwa. Hii nayo ni hofu kubwa sana, na hapa mtu anakuwa anafikiria vipi kama nikishamwambia akakataa. Kwa hofu hii utajikuta ukishindwa kusema kwa kujiamini na hata kutetemeka. Kutetemeka ni hali ya mwili wako kujiandaa na jambo ambalo ni hatari sana, na jambo hili umelitengeneza wewe mwenyewe kwenye mawazo yako kwa kufikiria kukataliwa.
Kuondokana na hofu hii jua ya kwamba kunakukataliwa na kukataliwa siyo mwisho wa dunia. Jua kabisa katika watu 10 utakaowaambia, 9 watakataa, lakini mmoja atakayekubali atakuwa muhimu zaidi kwako. Hivyo ili kumpata mmoja, inabidi uongee na watu kumi. Kwa mtazamo huu utakuwa na hamasa na kujiamini zaidi.
3. Kila mtu atasahau, na hakuna anayejali sana kuhusu makosa yako.
Kitu kingine ambacho kinawapa watu hofu ya kuongea mbele ya wengine ni kufikiria kama wakikosea basi watu watakucheka au kukuona hujui, kukudharau na hata kukutania. Nikuambie tu ukweli ya kwamba haya umeyatengeneza mwenyewe kwenye akili yako. iwe unaongea na mtu mmoja au wengi, kila mtu ana matatizo yake binafsi, hata kama utakosea, usifikiri mtu ataenda kukosa usingizi usiku akifikiria jinsi ulivyokosea. Hata kama watakucheka itaishia pale.
Hivyo ondokana na hofu hii kwamba ukikosea watu watakucheka na kukudharau. Wengi watasahau na kuendelea na maisha yao. Na wachache watakaokumbuka watakusaidia kuwa bora zaidi.
4. Kama unaongea na watu wengi tafuta mmoja wa kuongea naye.
Kama unaongea na kundi kubwa la watu, hofu ndiyo inazidi kuwa kubwa. Na kuondokana na hofu hii acha kulifikiria kundi lote kubwa na badala yake tafuta unayemfahamu kwenye kundi hilo na kwenye akili yako kuwa kama unaongea naye. Unapoona kwamba unaongea na mtu mmoja au wachache, utajiamini zaidi.
5. Unapoongea mwangalie mtu usoni.
Moja ya vitu vinavyowaondolea wengi kujiamini ni pale wanapoongea huku wakiangalia chini au wakiangalia pembeni. Kwa kufanya hivi unazidi kujizidishia hofu kwa sababu huoni unayeongea naye anapokeaje kile unachoongea. Unapoongea na mtu yeyote kuna lugha za alama ambazo unaweza kuziona usoni mwake, kuna alama ataonesha kama anakubaliana na wewe, au kama anashangaa, au kama hakutegemea na alama nyingine nyingi.
Kwa kumwangalia mtu wakati unaongea utajua wakati gani wa kubadili mwelekeo wa mazungumzo yako kutokana na ishara anazokuonesha kupitia uso wake. Japo ni vigumu kama hujazoea, penda kuwaangalia watu usoni unapoongea nao.
Hofu ya kuongea mbele ya wengine ni hofu kubwa na inayowazuia wengi kuzitumia fursa zinazokuja mbele yao. Uzuri ni kwamba unaweza kuondokana na hofu hii kwa kuanza kujiamini kupitia kujua vizuri unachofanya na kutokujali kuhusu kukosea. Pia anza kuongea na watu ambao unawafahamu kitu kile kile ambacho unakwenda kumwambia ambaye humfahamu. Utakuwa umejijengea kujiamini na pia kurekebisha baadhi ya makosa ambayo ungefanya.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.
Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.