Wewe kama mfanyabiashara makini, hitaji la kwanza kabisa ni kuijua vizuri biashara yako, nje ndani. Ni lazima wewe uwe mtaalamu wa biashara yako, kwa kizungu tunasema uwe expert kwenye hiyo biashara unayofanya.
Kwa maana hiyo unahitaji kujua mengi kuhusu biashara yako na wakati huo huo unahitaji kuwa wazi kujifunza kuhusu biashara hiyo. Isifike wakati ukaona kwamba wewe unajua kila kitu kuhusu biashara yako, bado kuna vingi unahitaji kuvijua.
Leo katika mada zetu hizi za biashara leo nataka nikushirikishe neno moja ambalo ni marufuku kumwambia mteja wako. Ninaposema marufuku namaanisha marufuku kweli.
Neno hilo ni HAIWEZEKANI.
Kamwe usimwamnie mteja wako kwamba haiwezekani, hata kama amekupa hitaji la ajabu kiasi gani, msikilize, mwombe akupe muda ufanyie kazi na kisha fanyia kazi. Kwa muda atakaokupa ndipo utakwenda kujifunza kama ni kitu ulikuwa hujui.
Na kama muda utakwisha na hujapata alichotaka basi uwe umeandaa elimu ya kumshauri vizuri mteja kipi kinaweza kuwa bora kwake.
Kwa njia hii utajifunza zaidi kuhusu biashara yako, hasa kwa bidhaa au huduma unazotoa.
Hivyo usimwambie mteja kwamba anachotaka hakiwezekani, bali muombe mteja akuoe muda na ufanyie kazi hitaji lake.
Nakumbuka wakati naanza biashara ya kuwatengenezea watu blogs na website, wateja walikuwa wanakuja na mahitaji ambayo hayajazoeleka. Mwanzo nilikuwa nawaambia hiko hakiwezekani, lakini siku moja nikaingia mtandao wa google na kutafuta kama kitu hiko kinafanyika, nikakuta wengi wanafanya.
Kuanzia wakati ule mpaka sasa, sijawahi tena kumwambia mteja haiwezekani, badala yake nakwenda kutafuta zaidi na mara nyingi huwa napata na hata nikikosa napata mbadala ambao ni bora zaidi kwa mteja.
Kumbuka, usimwambie mteja HAIWEZEKANI, bali fanyia kazi mahitaji yake, ukikosa anachotaka basi njoo na mbadala utakaofanya maisha yake kuwa bora zaidi.
Kila la kheri.
Kama kuna changamoto yoyote ungependa tujadili hapa iweke kwenye maoni hapo chini.