Tumekuwa tukikumbushana mara kwa mara umuhimu wa kusema HAPANA, hasa kwa mambo ambayo hayana manufaa kwako. Maana haya ndiyo mambo ambayo yanatupotezea muda wetu mwingi na hayana thamani yoyote.

Lakini kuna sehemu moja muhimu ambayo unatakiwa kusema NDIYO kila mara. Na hapa ni pale unapokutana na dunia. Unapokutana na dunia uso kwa uso, sema tu ndiyo, na utanufaika sana.

Maji ndiyo kitu chenye nguvu kubwa sana duniani, na unajua nguvu hii inatoka wapi? Nguvu hii inatokana na kukubali kwa maji, kwa kusema ndiyo. Hata siku moja hutakuta maji yenyewe yakitoka bondeni na kuelekea kilimani, bali yanatoka milimani na kuelekea bondeni. Na hata yanapokutana na kizuizi, hayasemi hapana, bali yanatafuta sehemu rahisi ya kupenyeza. Na kikubwa kuliko yote, maji yapo tayari kujibadilisha kwenye umbo lolote, na ndio maana yanaweza kuingia popote. Na pia yanaweza kufanya uharibifu mkubwa kwa kuanza kidogo kidogo.

Ukiweza kujijengea tabia kama za maji hakuna kitu kitakachokushinda kwenye dunia hii. Na ili kuwa na tabia hizi, ni lazima useme NDIYO kwa dunia. Mara nyingi huwa tunaibishia dunia, dunia inaleta hiki sisi tunapinga na kutaka kingine, mwishowe tunakosa tulichopewa na kile tulichotaka pia. Badala yake unaweza kusema ndiyo kwa kile dunia imekuletea na baada ya hapo kujiuliza utakitumiaje kupata kile ambacho unakitaka.

Tunajua dunia ina changamoto nyingi sana, lakini bado tunakazana kuzikataa changamoto hizi. Lakini ukiweza kusema ndiyo, utajikuta unaweza kuzitatua changamoto zozote unazokutana nazo na unaendelea kuwa bora kila siku.

Sema ndiyo kwa dunia, na maisha yako yatakuwa bora zaidi kila siku. Ni muhimu ujue ni wakati gani dunia ndiyo inahusika na wakati gani watu wengine ndiyo wanahusika. Ni hatari zaidi ukisema ndiyo kwa wengine ukifikiri unasema ndiyo kwa dunia. Njia ya uhakika ya kujua hii ni dunia ni pale kitu kimetokea na huwezi kuzuia au kubadili na unahitaji kufanya maamuzi.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; THE 10X RULE, Tofauti Pekee Kati Ya Mafanikio Na Kushindwa.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba ili niwe na nguvu kubwa za kufanya mambo makubwa, nahitaji kusema NDIYO kwa dunia. Kwa kusema kwangu ndiyo najia fursa kubwa zaidi ya kujifunza na kutumia hali ninayopitia kunifikisha kule ninakotaka. Kuanzia leo nitaacha kushindana na dunia, nitasema NDIYO na nategemea kufanya makubwa.

NENO LA LEO.

‘You can’t stop the waves, but you can learn to surf.’— Jon Kabat-Zinn

Huwezi kuyazuia mawimbi, ila unaweza kujifunza jinsi ya kupiga mbizi.

Usikazane kushindana na dunia, sema ndiyo na utapata fursa nyingi za kujifunza na kufikia mafanikio makubwa.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.