Kama ambavyo tumekuwa tunajifunza mara kwa mara, kuna eneo moja muhimu sana unaloweza kulitumia vizuri sana kwenye ushindani wa biashara. Japo sijuambii ushindane, ila unapokuwa vizuri kwenye eneo hili hata wale wanaofanya biashara sawa na yako watakuona kwa mbali tu.
Eneo hili ni kutoa huduma bora sana kwa wateja wako.
Kama unavyojua mteja haji kununua kwako kwa sababu anakuonea huruma au kwa sababu tu unauza.
Bali mteja anakuja kununua kwako kwa sababu ana shida anayotaka itatuliwe au ana hitaji analotaka litimizwe.
Hivyo lengo lako kubwa ni kuhakikisha mteja anapofika kwenye biashara yako, anaondoka akiwa bora kuliko alivyofika.
Je ni mambo gani unayohitaji kufanya ili uyoe huduma bora sana kwa wateja wako? Haya ndiyo tutakayojifunza kwenye makala ya biashara leo. Na haya ndiyo ya msingi.
1. Msikilize vizuri mteja na jua tatizo au hitaji lake hasa ni nini. Hakuna kitu ambacho mtu yeyote anapenda kama kuona anajaliwa na kusikilizwa.
2. Mpatie mteja kile ambacho kitatatua tatizo lake na sio kile ambacho kitakupa faida wewe tu.
3. Mfanye mteja kuwa sahihi mara zote, maana mara zote mteja yupo sahihi. Kama kuna changamoto zozote mteja anakutana nazo kwenye biashara yako msaidie kuondokana nazo.
4. Tumia lugha nzuri kwa mteja, hata kama mnatofautiana usichochee kwa maneno makali.
5. Tengeneza urafiki na mteja, mfanye ajione wa pekee sana kwenye biashara yako, na sio ajione tu bali iwe hivyo. Kama unaweza jua majina ya wateja wako, na mnapozungumza waite kwa majina yao.
6. Kuwa na mawasiliano ya wateja wanaonunua kwako mara kwa mara. Na watumie jumbe nzuri mara chache, kama kuna mteja hujamwona siku nyingi kwenye biashara yako, wasiliana naye na mjulie hali.
7. Kama una wasaidizi kwenye biashara yako wafundishe vizuri kwenye utoaji wa huduma kwa wateja.
8. Toa zawadi ndogo ndogo kwa wateja wako, kitu kidogo sana unachofanya kwa mteja wako kama zawadi kitamfanya akujali sana.
9. Mara zote ongelea biashara yako kwa jinsi inavyomsaidia mteja, kadiri mteja anavyosikia zaidi ananufaikaje, ndivyo anavyoona umuhimu wa biashara yako kwake.
10. Mwambie mteja asante kwa kuja kwenye biashara yako na mwambie KARIBU TENA.
Mengi ni mambo madogo madogo ambayo wafanyabiashara wengi watayapuuza na kuona hawana muda wa kuyafanya. Ila wewe usiyapuuze, ni muhimu sana kwa ukuaji wa biashara yako.
Kila la kheri.
Kwa changamoto yoyote au jambo lolote ungependa tujadili kuhusu biashara weka kwenye maoni hapo chini. Karibu sana tujifunze kwa pamoja.