Njia bora sana ya kuifikiria biashara yako, ni wewe mmiliki wa biashara kuvaa viatu vya mteja wako.

Hebu fikiria kama wewe ndiyo ungekuwa mteja wa biashara hiyo unayoifanya wewe, je ungeendelea kuwa mteja wa biashara hiyo? Na unapofanya hivi usijaribu kujidanganya, ondoa hisia za kujipendelea na fikiri kwa kina.

Kwa kufikiria hivi, kwa mtazamo wa mteja ni rahisi sana kuona vitu vya msingi kama…

Sababu ya mteja wako kwenda kwa mshindani wako wa kibiashara.

Hili ni jambo kubwa sana ambalo wafanyabiashara wengi huwa hawalipi uzito.

Unajua mteja hawezi tu kuondoka kwako na kwenda kwa mfanyabiashara mwingine, ni lazima kuna sababu. Na sababu hizi zimegawanyika katika makundi mawili.

Kundi la kwanza ni sababu zinazomvuta, hizi zinatokana na mambo mazuri anayoweza kupata kwenye biashara nyingine ambayo hapo kwako hapati.

Kundi la pili ni sababu zinazomsukuma, hizi zinatokana na mambo ambayo hayapendi kwenye biashara yako na hivyo analazimika kutafuta mahali pengine.

Kwa unavyofikiria biashara yako kama mteja, je ni mambo gani yanaweza kukusukuma uondoke kwenye biashara hiyo? Pia tembelea wafanyabiashara wengine na fikiria ni mambo gani kule yanaweza kukuvutia kuwa mteja?

Kuna njia moja ya kuwa na wateja milele, na njia hii ni kujua mahitaji ya wateja wako ni yapi, na mategemeo yao ni yapi kisha yavuke mategemeo yao. Na hakuna kitakachowaondoa kwenye biashara yako.

Fanyia kazi hili kila siku kwenye biashara yako, na utaona mabadiliko makubwa kwenye biashara yako kila siku.

TUPO PAMOJA,

KOCHA.

MUHIMU; Kama una swali, maoni au changamoto yoyote ya kibiashara, weka kwenye maoni hapo chini na tutajadiliana zaidi na kama itahitajika nitaandaa makala ya kuhusu jambo hilo kwenye makala zijazo.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz