Mtaji Hautakufuata Hapo Ulipo, Mtaji Wa Uhakika Unaweza Kuupata Kwa Njia Hii Moja Ya Uhakika.

Habari rafiki?
Kama ambavyo wote tunajua, upatikanaji wa ajira ni tatizo katika zama hizi. Na tatizo hili siyo kwa nchi yetu pekee bali ni kwa maeneo mengi duniani. Hii inatokana na mfumo wa elimu kushindwa kuendana na mabadiliko makubwa yanayoendelea, ambapo kwa sasa teknolojia imechukua nafasi kubwa hivyo uhitaji wa wafanyakazi unapungua. Huku pia uzalishaji wa wafanyakazi ukiongezeka kutokana na kuongezeka kwa fursa za kupata elimu.
Hivyo vijana wamesoma, na sifa za kuajiriwa wanazo, ila nafasi za ajira ndiyo hazipatikani. Na kwa kukosekana huku kwa nafasi za ajira, kimbilio pekee linakuwa ni kujiajiri au kufanya biashara. Vijana wamekuwa wakishauriwa sana kuingia kwenye biashara, badala ya kukaa tu na kusubiri kuajiriwa.
Lakini vijana wamekuwa na kilio kimoja, mtaji hakuna, hatukopesheki, hatuna dhamana za kuweka ili kupata mikopo benki, na mengine mengi. Ni kweli kabisa hizi ni changamoto za wazi ambazo zinazuia watu kuingia kwenye biashara.
Kama umekuwa msomaji wa muda mrefu wa AMKA MTANZANIA, unajua ya kwamba sisi hatukubaliani na majibu rahisi. Ni kweli iko wazi wewe kijana huwezi kukopesheka, na hakuna anayejali kukupa wewe mtaji, au umetokea kwenye familia ambayo haina uwezo. Lakini sasa unafanya nini? Unakaa na kuilaumu serikali, au kulaumu wale ambao ulifikiri wanapaswa kukuwezesha wewe?
Unaweza kulaumu utakavyo, unaweza kutukana na kulalamika kadiri unavyotaka wewe mwenyewe, lakini mwisho wa siku tunarudi hatua ya kwanza. Je kulaumu kwako au kulalamika kwako kumesaidia kubadili hali uliyonayo? Mara zote jibu linakuwa hapana. Utakapomaliza kulalamika, ukweli utabaki pale pale, kwamba umesoma, kazi huna na pia hujaweza kujiajiri.
Na hapa ndipo AMKA MTANZANIA inapoingia. Hapa ndipo sasa ninapokuambia achana na hayo yote uliyodanganywa tangu unakua mpaka leo. ulivyodanganywa na wazazi na jamii kwamba ukisoma kwa bidii na ukafaulu utapata kazi nzuri na kuwa na maisha mazuri. Na walimu wako wakakudanganya tena wakati wanakufundisha ya kwamba ukienda kazini utafanya hivi na hivi. Na sasa umekutana na uhalisia kwamba kusoma umesoma, lakini kazi hakuna.
Hapa ndipo unapoamua kushika hatamu ya maisha yako, hapa ndipo unapoamua wewe ndiye dereva mkuu wa maisha yako na hapa ndipo unapoamua wewe ndiye wakujenga au kubomoa maisha yako. na baada ya kuamua haya ndipo unapoamua kuchukua hatua.
Leo nataka tushirikishane njia mbadala za kupata mtaji, nasema njia mbadala kwa sababu haziendani na zile njia zilizozoeleka na hivyo ni njia ngumu na zinahitaji kujitoa na kujituma.
Kabla hatujaangalia njia hii mbadala napenda uwe tayari umeshaamua kushika hatamu ya maisha yako, umeshaamua kuacha kulalamika na kulaumu, na umeshakubali maisha ni yako na jukumu ni lako. Kama bado hujakubali hayo ni vyema usiendelee kusoma kwa sababu utakayojifunza hapo chini hayataendana na wewe na hivyo utaishia kupingana na mimi kitu ambacho pia hakitakusaidia.
Kama umeshakubali kwamba maisha ni yako basi karibu sana.
Njia ya uhakika kwako kupata mtaji wa uhakika, ni kuanza kufanya kitu, na kuanza kufanya kwa ngazi ya chini sana, kwa kuanzia pale ambapo upo sasa.
Wacha nikuibie siri moja ambayo nimekuwa najifunza kadiri ninavyozungumza na kuwasiliana na watu wengi.
Ukweli ni kwamba hapa tanzania kuna watu wengi wana fedha, ila hawana kitu cha kuzifanyia, badala yake wameziweka tu benki au wananunua vitu ambavyo haviongezeki thamani haraka. Watu hawa wamejifunza kuficha fedha zao au kuziweka kwenye vitu kama ardhi kwa sababu wameumizwa sana.
Kuna wazazi ambao wamejaribu kuwafungulia watoto wao biashara lakini zikaishia kufa. Kuna watu ambao wameanzisha biashara ili kuwasaidia ndugu zao ambao hawana ajira lakini wakaziua. Na pia kuna watu ambao wameanzisha biashara na kuajiri watu ambao hawana ajira, lakini wakaishia kuua biashara zile.
Hii inatokana na ukweli kwamba watu wengi hawapo tayari kujituma ili kuweza kutoa matunda mazuri, au kuanzia biashara chini na kuikuza. Na ndiyo maana watu hawatakuamini wewe ambaye umekaa chini na kulalamika kwamba huna mtaji. Kwa sababu hata mtu akikupa, utakwenda kupoteza, kwa sababu biashara siyo rahisi kama wengi wanavyoona kwa nje.
Sasa ninachotaka kukushirikisha hapa leo ni wewe kuwa upande wa pili, usikae chini kupiga kelele kwamba mtaji huna au kitu gani umekosa. Badala yake fanya kwa vitendo. Chagua kufanya kitu ambacho mtu akiangalia anajua kweli huyu mtu amedhamiria kuleta mabadiliko kwenye maisha yake. Na siyo unafanya tu kwa sababu unataka uonekane, bali unafanya kwa sababu ndicho ulichoamua kufanya na una uhakika kitawezekana.
Ngoja tupeane mifano nina imani tutaelewana vizuri zaidi.
Kwa mfano umesomea mambo ya kompyuta (TEHAMA), lakini mpaka sasa bado hujapata kazi. Kaa chini na angalia ni jinsi gani jamii inayokuzunguka inaweza kunufaika na kile unachokijua. Kwa mfano dunia ya sasa kila kitu kinaweza kunufaika na mtandao wa intaneti. Lakini kwa hapa kwetu Tanzania bado kuna watu wengi hawajaweza kutumia vizuri mtandao wa intaneti. Kuna biashara nyingi ndogo na za kati ambazo hazina tovuti. Kuna shule nyingi za sekondari ambazo hazina tovuti. Tovuti ni kitu ambacho sio kigumu kutengeneza kama kweli unataka kufanya hivyo.
Sasa wewe unaweza kuandaa mpango wako wa kutengenezea watu tovuti kwa gharama rafiki. Ukaandaa ushawishi wako kwa nini mtu anahitaji tovuti na wewe unawezaje kumsaidia kwenye hilo. Kisha ukazunguka kwa wafanyabiashara au shule za sekondari. Ukitembelea watu 100, na kuongea nao vizuri juu ya uhitaji wao na kile unachotoa wewe, hutakosa 10 ambao watataka kupata huduma zako. Hata ukipata mmoja, mtumie huyo kuianza biashara yako.
Mfano mwingine ni kwenye kilimo. Najua hapa utasema sina mtaji, sina shamba na vingine vingi. Lakini kumbuka sisi tumeshajitoa kushika hatamu ya maisha yetu. Hivyo angalia njia zozote unazoweza kutumia kupata fedha kidogo tu ya kuanzia. Labda una simu ya bei kali unaweza kuuza, labda kuna matumizi ambayo umekuwa unafanya lakini siyo muhimu sana kwako unaweza kuyaacha.
Tafuta eneo dogo la shamba, karibu na ulipo, usinunue, bali kodi. Unaweza hata kuanza na nusu heka, chagua kufanya kilimo cha muda mfupi, kama matikiti maji, au vitunguu, au aina nyingine za matunda na mboga mboga. Weka juhudi zako katika kufanya kilimo hiki vizuri na utakapoanza kuona mambo yanakwenda vizuri, ongea na watu kwamba umechukua hatua kufikia hapo ulipofika sasa na hivyo unahitaji wakuunge mkono. Watu wengi sana watakuunga mkono na utaendelea na kilimo chako.
Hizi ni njia za uhakika ambazo ukipita ni lazima utapata mtaji. Lakini pia ni njia ngumu mno ndiyo maana wengi hawapo tayari kuzipita. Je wewe upo tayari? Kama ndiyo anza na nijumuishe kuwa mmoja wa wale utakaotaka wakuunge mkono kwenye juhudi zako. Baada ya kufanya na ukaona kweli unaweza kupata kitu fulani kwa njia uliyochagua.
hiyo mifano miwili niliyotoa siyo lazima ufanye kama ilivyo, nimeitumia tu kukupa mwanga, unaweza kufanya hivyo au unaweza kuboresha zaidi kulingana na pale ulipo na kile unachotaka kufanya.
Amua kuchukua hatua ya kuboresha maisha yako au amua kuendelea kulalamika kwamba mtaji hakuna. Miaka mitano ijayo kutakuwa na tofauti kubwa sana kama utachukua hatua leo, au utaendelea kuwa mlalamikaji kama hutataka kuchukua hatua.
Nakutakia kila la kheri kwa hatua yoyote utakayoamua kuchukua.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

One thought on “Mtaji Hautakufuata Hapo Ulipo, Mtaji Wa Uhakika Unaweza Kuupata Kwa Njia Hii Moja Ya Uhakika.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s