Kila kitu kinachoendelea kwenye maisha yako ni mwalimu wako. Hali yoyote unayopitia, changamoto zozote unazokutana nazo, hawa ni walimu kwako na wamekuja na masomo muhimu sana unayotakiwa kuyazingatia.
Unapompoteza mtu unayempenda, au ambaye ni muhimu sana kwako, tukio hili ni mwalimu kwako. Na linakupa funzo kubwa sana kwamba hutakuwa na wale unaowapenda milele, na hivyo ni vyema kutumia muda huu unaopata kuwa nao kuwa muda bora kwenu wote.
Unapopata hasara kwenye biashara yako, huyu ni mwalimu anakuja kukuonesha ni maeneo gani kwenye biashara yako ambayo hujawa makini, au bado hujayajua vizuri. Na unapopata faida kwenye biashara ni mwalimu kwako anayekufundisha njia bora unazopaswa kuendelea kutumia kwenye biashara yako.
Unapofukuzwa kazi ni mwalimu anakuja kukufundisha kwamba hakuna kitu kwenye maisha kinachodumu, na usiweke mategemeo yako yote kwenye kitu kimoja. Na unapopata kazi au kupandishwa cheo pia ni mwalimu kwako anayekuonesha kwamba kuna watu wanathamini kile unachotoa, hivyo endelea kutoa kwa ubora.
Wengi tunakosa nafasi ya kujifunza kupitia walimu hawa wanaotuzunguka kwa sababu tunapotezwa na hisia. Tunakuwa na huzuni na hasira pale tunapopoteza na tunakuwa na furaha pale tunapopata. Hivyo hatujifunzi kutoka kwa mwalimu na hili linapelekea tatizo kutokea tena au kama ni nafasi nzuri tuliipata inapotea.
Kila kinachotokea kwenye maisha yako, kila siku na kila wakati, jipe dakika chache na jiulize je mwalimu huyu amekuja kunifundisha nini? Jua somo na songa mbele.
SOMA; UCHAMBUZI W AKITABU; The Four Purposes Of Life (Makusudi Makuu Manne Ya Maisha)
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba kila kinachotokea kwenye maisha yangu ni mwalimu ambaye amekuja kunifundisha somo muhimu sana kuhusu maisha. Lakini mara nyingi nimekuwa nakosa masomo haya kwa sababu hisia zimekuwa zinanitawala. Kuanzia sasa nitajipa muda wa kutafakari kwa kina kila kinachotokea kwenye maisha yangu na kujua ni somo gani napaswa kujifunza hapo.
NENO LA LEO.
Seek to learn constantly while you live; do not wait in the faith that old age by itself will bring wisdom. –Solon
Tafuta kujifunza kila mara wakati unaishi, usisubiri kwa kuamini kwamba uzee ndio utakaokuletea hekima.
Maisha yako ya kila siku ndiyo darasa lako, kila kinachotokea ni mwalimu wako. Jifunze kwenye kila kitu kinachotokea kwenye maisha yako, kila kitu kimebeba somo kubwa.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.