Heshima ya kweli ni upendo.
Watu wengi wanaamini wanaheshimika pale ambapo wanaogopeka. Au wanafikiri kuonesha heshima kwa wengine ni kuwa na hofu nao au kuwaogopa. Hii siyo kweli.
Upendo na hofu au woga ni vitu ambavyo haviwezi kwenda pamoja kwa wakati wowote ule. Ni vitu vinavyopingana, upendo unapokuwepo, hofu haiwezi kuwepo.
Kama unataka kuheshimika kweli usijenge mazingira ya watu kukuogopa au kukuhofia. Badala yake jenga mazingira ya watu kukupenda. Kwa sababu upendo ndio unaobeba heshima ya kweli.
Kama unataka kumheshimu mtu, usimuogope au kumhofia, badala yake mpende. Unapompenda mtu unampa nafasi ya kuwa yeye na kwa njia hii atakuheshimu.
Upendo ndiyo nguzo kuu ya heshima na maisha bora pia. Kwa sababu bila ya kuheshimiana, maisha hayawezi kuwa bora.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba heshima ya kweli inatokana na upendo. Na upendo hauwezi kukaa mahali pamoja na hofu. Hivyo ili niheshimike na wengine ni lazima niondoe hali ya kuhofiwa na niwe na hali ya kupendwa. Na ili niwaheshimu wengine ni lazima niache kuwaogopa na badala yake niwapende. Upendo ndiyo nguzo ya heshima na maisha bora.
NENO LA LEO.
A great relationship is about two things, first, find out the similarities, second, respect the differences. – Unknown
Mahusiano bora yanajengwa na vitu viwili, kwanza jua maeneo mnayokubaliana na pili heshimu tofauti zenu.
Hakuna watu ambao wanaweza kufanana kwa kila kitu. Tofauti zipo na ni sehemu ya maisha yetu, tuheshimiane kwa tofauti hizi.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.