Moja ya njia za kupata au kuongeza mtaji wa biashara yako ni kuomba mkopo. Na siyo kila mtu anaweza kupata mkopo, hivyo unapokuwa na sifa za kupata mkopo, na ukapata mkopo unaohitaji ni jambo zuri kwa biashara yako. Lakini kama ambavyo unajua, au kama hujui unahitaji kujua leo, mkopo ni biashara ya taasisi inayokupa wewe mkopo huo. Hii ina maana kwamba waliyekupa mkopo anategemea kunufaika na mkopo huo. Na ndiyo maana kuna riba na kama utashindwa kulipa basi mali zako zitafilisiwa.

Leo kupitia KONA YA MJASIRIAMALI tutakwenda kujadili mambo muhimu sana ya kila mjasiriamali kuzingatia pale anapopata mkopo wa kibiashara. Hili ni jambo muhimu sana kujua na kuzingatia kwani mikopo hii ambayo imewawezesha wengi kuanza na kukuza biashara zao, pia imewafanya wengi kupoteza biashara zao na mali zao pia. Na kwa kuwa watu wengi wanafanya biashara kwa mazoea, basi mambo haya muhimu hawapati kwa kujifunza.

Kwanza kabisa kumbuka sababu iliyokufanya uombe mkopo. Wakati unaomba mkopo ulikuwa na sababu maalumu na ulijua ukipaya fedha hizi utakwenda kufanya kitu gani. Lakini wengi wanapozipata fedha, ile mipango ya awali inasahaulika na ghafla panajitokeza vitu vingine ambavyo vinaweza kuonekana ni muhimu zaidi. Ukishaanza kutumia mkopo wako kwa vitu vingine tofauti na vile ulivyokuwa umepanga, unajiandaa kuingia kwenye matatizo. Hata kama kuna kitu kizuri namna gani kimejitokeza mbele yako, usianze kufanya kabla hujakamilisha mipango yako ya awali. Hii ni kwa sababu unapokuwa na fedha kila kitu kinaonekana ni muhimu na kizuri. Lakini fedha za mkopo ni fedha ambazo zinahitaji kurudi na riba, hivyo hakikisha unazitumia kwa mipango yako ya awali, zikuzalishie na kukuachia faida pia.

Usitumie fedha yote ya mkopo, weka kiasi pembeni cha kukunyanyua pale mambo yanapokwenda tofauti na mategemeo. Pamoja na kuwa na mipango mizuri kabla ya kuchukua mkopo wa biashara yako, bado ni muhimu kutenga sehemu ya fedha za mkopo na kuweka pembeni. Usichukue fedha zote na kuziweka kwenye mipango yako, huenda mipango hiyo isiende kama ulivyotegemea na ikiwa huna tena fedha basi utajikuta unakwama vibaya sana. Ni vyema kuweka kiasi fulani pembeni ambacho unaweza kukitumia kubadili hali ya mambo pale kila kitu kinapokwama. Kama utatumia fedha yote ya mkopo unaweza kujikuta unalazimika kuchukua tena mkopo juu ya mkopo. Kwa sababu unakuta umeweka fedha zote na unahitaji kiasi kingine ili kumalizia kitu ambacho baadaye kitaleta faida.

Usibadili maisha kwa fedha za mkopo. Fedha ni moja ya vitu ambavyo ni changamoto kubwa sana kwa watu wengi. Na hili ni tatizo ambalo lina mizizi mirefu inayoanzia kwenye malezi na tabia zetu. Kuna watu wakiwa na fedha utawajua, kwa sababu utaona mabadiliko makubwa sana. Utaona maisha yanabadilika, mavazi yanabadilika na hata vyakula vinabadilika. Ni vyema ukajua ya kwamba fedha ya mkopo siyo fedha yako, bali ni fedha ya biashara. Hivyo unapojaribu kutumia fedha hiyo kwa matumizi mengine ambayo siyo ya biashara maana yake unaidhulumu biashara. Acha maisha yako yaendelee kuwa kama yalivyo, kikubwa kwa sasa ni kukuza biashara yako na kama utafanikisha hilo vizuri, ukaweza kulipa mkopo wako na kubaki na faida, utaweza kubadili maisha yako.

Usikimbie deni. Waswahili wanasema kukopa harusi, kulipa matanga. Watu wanafurahia sana wanapoupata mkopo, ila inapofika wakati wa kulipa, wanapatwa na huzuni kubwa. Jiandae kulipa mkopo wa biashara uliochukua. Hakuna namna yoyote unaweza kuukimbia na ukabaki salama. Na kama mambo hayaendi vizuri, biashara haileti marejesho uliyotegemea, usijifiche. Badala yake wasiliana na taasisi iliyokupa mkopo na waeleze hali halisi. Mnaweza kupanga upya namna ya kulipa mkopo huo, na wewe ukajitahidi kukamilisha malipo yako. Lakini unapojificha au kukimbia, unajijenga picha mbaya ambayo baadaye itakunyima fursa nyingi.

Kuomba na kupata mkopo ni jambo moja, na matumizi ya mkopo huu ni jambo jingine muhimu sana. Wengi wamekuwa wakipata mikopo lakini ikaishia kuharibu biashara zao. Hakikisha wewe huwi sehemu ya watu hawa kwa kuwa na matumizi mazuri ya mkopo unaopata. Zingatia haya ambayo tumejadili hapa leo. Kila la kheri.