Baadaye ni njia rahisi ya kujitoa kwenye mvutano mkali unaokuwa nao sasa. Kwenye mvutano kwamba nifanye au nisifanye, njia rahisi ya kujitoa hapo ni kusema nitafanya baadaye.

Lakini baadaye ni mara chache sana inatokea tukafanya tulichotaka kufanya, au tukaleta mabadiliko ambayo tunataka kuleta. Baadaye tunayosema huwa haifiki na hata ikifike tunakuwa na mengine mengi na hivyo hatuchukui tena hatua.

Jikumbushe ni mambo mangapi ambayo uliwahi kusema utafanya baadaye lakini hukufanya kabisa. Tatizo siyo kufanya sasa au baadaye, tatizo ni kwamba kuna ugumu kwenye kufanya jambo, ambao hutaki kuona kwamba unaukwepa na hivyo inakuwa rahisi kujiambia baadaye, ili utoroke ugumu huo.

Dawa.

Unapojikuta kwenye mvutano, unapojikuta kwenye wakati mgumu, usitafute njia rahisi ya kujitoa kwenye hali hiyo, badala yake tafuta njia ya kuongeza mvutano na ugumu huo. Na njia pekee ni kufanya sasa.

Kufanya sasa ni njia ngumu kwa sababu utaendelea kujiuliza maswali ikiwa utaweza au la, ikiwa ufanye au la. Yote haya ni kukupeleka kwenye njia rahisi ya kukwepa. Sasa usikubali njia hii, wewe fanya na ugumu wote utapotea.

Mvutano na mgumu huwa unakuwa mkubwa sana kabla hujaanza, kwa sababu unakuwa umejijengea hofu nyingi. Lakini unapoanza, utaona haikuwa ngumu kama ulivyodhani awali.

Kumbuka neno, na neno ni KUFANYA.

SOMA; MAMBO 20 NILIYOJIFUNZA KWENYE KITABU HOW TO STOP WORRYING AND START LIVING.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba mara zote ambazo nimekuwa najiambia nitafanya baadaye ni njia ya kutoroka ugumu wa jambo. Na mara zote nilizosema nitafanya baadaye nimekuwa sifanyi kabisa. Kuanzia sasa nitaacha kutumia neno baadaye na badala yake nitafanya jambo pale ambapo linaonekana gumu kabisa.

NENO LA LEO.

“Begin when you have the strength. You have it now; therefore the best time to begin is now.” ― Israelmore Ayivor

Anza wakati una nguvu. Na nguvu unazo sasa, hivyo wakati mzuri wa kuanza ni sasa.

Usiseme utaanza baadaye, baadaye huwa haifiki na ni njia rahisi ya kutoroka ugumu. Usiwe mtu wa kutoroka, FANYA SASA.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.