Mara nyingi wafanyabiashara tumekuwa tukijiuliza iwapo bidhaa au huduma tunayomuuzia mteja wetu inaendana na thamani ya fedha anayotoa. Kwa njia hii tumekuwa tunachukulia fedha ya mteja kama ndiyo kitu muhimu sana kwao, na hivyo kuhakikisha hawapotezi fedha zao kwa kufanya biashara na sisi.

Ni kweli kabisa fedha ya mteja ni muhimu, ameipata kwa njia ngumu na hivyo pia anastahili kupata thamani inayoendana na fedha aliyolipia. Na iwapo hata pata thamani inayoendana na alicholipa unakuwa umempoteza mteja huyo kwa sababu hakuna mtu yeyote anayependa kupoteza fedha aliyoipata kwa taabu.

Lakini siyo fedha pekee ambayo ndiyo kitu muhimu sana kwa mteja wako, kuna kitu kingine ambacho ni muhimu sana kwa mteja wako, na usipokuwa makini unaweza kumpoteza mteja wako kwa kumpotezea kitu hiko ambacho ni muhimu kwake. Leo kupitia makala hii tutakwenda kuangalia kwa undani kitu hiki muhimu sana kwa mteja wako na njia za kuhakikisha mteja wako ananufaika zaidi na biashara yako bila ya kupoteza kile ambacho ni muhimu sana kwake.

Kitu ambacho ni muhimu sana kwa mteja wako, na kwa kila mtu ni muda. Muda ni muhimu kuliko fedha, kwani ukipoteza fedha unaweza kupata nyingine, ila unapopoteza muda ndiyo imetoka, huwezi kupata muda huo tena. Muda una thamani kubwa sana na hivyo ni muhimu sana ujali muda wako mwenyewe na hata muda wa mteja wako.

Kama ambavyo umekuwa unajali kuhusu fedha ya mteja wako, na kuhakikisha mteja anapata thamani inayoendana na fedha anayolipa, ndivyo unavyohitaji kujali kuhusu muda wa mteja wako. Hakikisha mteja wako anapata thamani ambayo inaendana na muda anaowekeza kwa kile anachonunua kwenye biashara yako.

Kama unauza bidhaa, basi hakikisha kwa matumizi ya bidhaa hiyo mteja wako hapotezi muda wake. Na kama ukiweza kumsaidia kuokoa muda zaidi kupitia bidhaa yako basi utajenga mahusiano bora sana na mteja wako. Bidhaa yako inaweza kuwa na thamani ya fedha ambayo mteja ameilipia lakini anapokwenda kuitumia akapoteza muda mwingi kuliko ambavyo angeweza kwa kutumia bidhaa nyingine.

Kama unauza huduma, ni vyema ukajua ya kwamba mteja anapotenga muda ili kupata huduma yako, maana yake ameamua kuacha kufanya vitu vingine ambavyo ni vya muhimu sana kwake. Kama mteja amekuja kwako kwa ushauri, maana yake kuna mambo ameacha kufanya kwa muda huo na hivyo kukusikiliza wewe. Kama ni kitabu unauza, jua ya kwamba mteja wako amechagua kuacha kufanya mambo mengine ili asome kitabu chako. Ni vyema ukajiridhisha kwamba kwa huduma unayotoa, mteja hatojutia kupoteza muda wake. Ya kwamba ataondoka akiwa anajisifu kuwa amekuwa na matumizi bora sana ya muda wake kwa kutumia huduma zako.

Muda ni changamoto kwa kila mtu katika nyakati hizi. Na hii inatokana na wingi wa vitu vya kufanya huku tukiwa na masaa yale yale 24 kwa siku. Hivyo utakapofanya kosa na kupoteza muda wa mteja wako, kuna uwezekao mkubwa ukawa umempoteza mteja huyo moja kwa moja. Na kama akijua sehemu nyingine ambapo ataweza kutunza muda wake, au matumizi yake ya muda yakawa mazuri, basi atakusahau kabisa.

Fikiri kwa kina uwekezaji ambao mteja wako anaweka kwenye biashara yako, na siyo kwenye fedha tu, bali kwenye muda pia. Na ili kuhakikisha mteja wako hapotezi muda wake, ni vyema ukahakikisha ameelewa jinsi ya kutumia huduma au bidhaa ambayo umemuuzia. Kwa sababu moja ya vitu vitakavyompa mteja wako changamoto ni kushindwa kutumia huduma au bidhaa waliyolipia kwenye biashara yako.

Kuanzia sasa fanya tathmini ya biashara yako na ona kama kuna kitu chochote ambacho kinapoteza muda wa mteja wako, kifanyie marekebisho ili mteja wako apate thamani kubwa kupitia biashara yako kutokana na fedha na muda anaowekeza. Thamini muda wa mteja wako, hakikisha biashara yako inamwezesha yeye kuwa na matumizi bora kabisa ya muda wake. Kila la kheri katika kuboresha biashara yako.

TUPO PAMOJA,

KOCHA.