Pamoja na kwamba nafasi za ajira zimekuwa chache sana kwenye zama hizi, bado kuna tatizo kubwa hata kwa wale ambao wanazipata nafasi hizi za ajira. Maeneo mengi ya kazi yamekuwa na changamoto kubwa sana ambazo zinawazuia watu kuweza kufanya kazi zao kwa furaha na uzalishaji mkubwa.

Na changamoto kubwa kwenye maeneo ya kazi inaanzia hapa; kuwafanya watu wawili au zaidi, wanaotoka kwenye mazingira tofauti kufanya kazi kwa lengo moja ni kitu kigumu sana. Hii ni kwa sababu licha ya kuwa na ujuzi wa kazi, kuna ujuzi muhimu sana kuhusu tabia za watu na jinsi ya kuweza kwenda na wengine. Ujuzi huu haufundishwi shuleni na hivyo wengi wamekuwa wakikutana na changamoto kwenye maeneo ya kazi ambazo wangeweza kuziepuka kama wangekuwa na ujuzi juu ya watu.

Mambo haya 54 utakayokwenda kujifunza hapa yanatokana na kitabu kinachoitwa THE HARD TRUTH ABOUT SOFT SKILLS, workplace lessons smart people wish they’d learned sooner. Kitabu hiki kimeandikwa na Peggy Klaus.

Karibu tujifunze kwa pamoja mambo haya 54 ambayo ni muhimu sana kwako kama unataka kufanikiwa kwenye kazi. Mambo haya ni muhimu kwa waajiriwa ila pia kwa wafanyabiashara ni muhimu zaidi kwa sababu biashara yako inapokua utahitaji kuajiri na maarifa haya ni muhimu sana kwako ili kwenda vizuri na wafanyakazi wako.

Karibu tujifunze.

1. Anza kwa kujijua wewe mwenyewe kwanza. Kujua kazi yako ni muhimu, ila kujijua wewe mwenyewe ni muhimu zaidi. Jua ni maeneo gani uko vizuri, maeneo gani una mapungufu na vitu gani unavyopendelea na usivyopendelea pia.

2. Jua ni vitu gani upo tayari kupoteza. Huwezi kuwa na mafanikio kwenye kila eneo la maisha yako, kuna wakati utahitaji kupoteza kitu kimoja ili kupata kitu kingine. Mfano mlinganyo kati ya kazi na familia ni kitu kigumu kufikia. Kuna wakati utahitaji kupoteza muda wa kuwa na familia ili uwe kwenye kazi na kuna wakati utahitaji kupoteza muda wa kazi ili uwe na familia.

3. Mabadiliko yanatokea kila siku kwenye eneo lako la kazi. Hata kama ulifanikiwa sana kwenye kazi yako huko nyuma, hiyo siyo dhamana kwamba utaendelea kufanikiwa, unahitaji kwenda na mabadiliko.

4. Usikilize moyo wako. Kuna wakati ambapo unahitaji kufanya maamuzi lakini huna uhakika, nafsi yako huwa inakuwa na hisia fulani kuhusu hali unayopitia, zisikilize hisia hizo na zitathmini kwa kina.

5. Kuwa tayari kuchukua hatua za hatari (risk), kwa sababu hatua hizi ndizo zinazokuletea mafanikio makubwa zaidi. Kwa kuepuka hatua hizi hutaweza kukua.

6. Acha kujizuia wewe mwenyewe. Vitu vingi ambavyo unaogopa kufanya kwenye eneo lako la kazi, ni wewe mwenyewe unajizuia. Kama kuna kitu unataka kufanya tofauti, badala ya kusema hakitakubalika, hebu uliza na kitetee, utagundua watu wapo tayari.

7. Uadilifu ni kitu muhimu sana kwenye eneo lako la kazi. Jijengee uadilifu na ulinde sana. Usijihusishe kwenye jambo lolote ambalo linakwenda kinyume na uadilifu, hata kama unaona hakuna atakayejua au anayekuona, ukweli ni kwamba siku moja kila mtu atajua.

8. Bahati haiji bali inatengenezwa. Na bahati inatengenezwa kwa kuwa na maandalizi nakufanya kazi kwa juhudi kubwa sana. Acha kusubiri bahati na badala yake weka juhudi.

9. Bosi wako anataka wewe mwenyewe ufikirie ni jinsi gani unaweza kuifanya kazi yako kwa ubora sana. Mabosi hawapendi watu ambao hawawezi kujituma na kujiongeza wenyewe. Usisubiri kuambiwa kila kitu, jiulize ni kipi muhimu na kifanye.

10. Jua ni wakati gani wa kung’ang’ana na wakati gani wa kusonga mbele. Kuna watu ambao wanapenda kuwa na taarifa kidogo tu ndio waanze na kuna ambao wanapenda taarifa nyingi ndiyo waanze kazi. Wewe jua ni wakati gani unahitaji taarifa kidogo na wakati upi unahitaji taarifa nyingi.

11. Kama huwezi kufanya kitu usiseme NDIYO, lakini pia kuwa makini unaposema HAPANA. Hakuna kitu kibaya kama kukubali kufanya kitu halafu usikifanye. Lakini pia inaleta picha mbaya pale unaposema hapana hasa kwa bosi wako. Jifunze jinsi ya kusema hapana bila ya kuleta picha mbaya.

12. Tabia yako ya kuahirisha mambo inajaribu kukufundisha kitu fulani. Kama umekuwa na tabia ya kuahirisha mambo, kuna kitu fulani ambacho tabia hiyo inajaribu kukufundisha. Angalia kwa kina kwa nini hupendi kuanza kitu kwa wakati, huenda hujajiandaa vya kutosha au una uvivu.

13. Kulalamika ni kwa watoto na hakuna mtu anayependa mtu anayelalamika kila wakati. Epuka kuwa mtu wa kulalamika kwa kila jambo kwenye eneo lako la kazi. Watu watakuwa wanakukimbia kwa sababu kila wakikutana na wewe una jipya la kulalamikia.

14. Simamia vizuri mikutano yako, vinginevyo itakuwa sehemu ya kupoteza muda. Kwanza jua ni mikutano ipi muhimu wewe kuhudhuria na ipi unaweza usihudhurie na ukatoa sababu ya kueleweka. Mikutano mingi unayohitajika kuhudhuria inakuwa haina tija, jua jinsi ya kusimamia hilo.

15. Unachofikiri kila mtu anaja, mara nyingi siyo ukweli. Kuna vitu vya wazi kabisa ambavyo unaweza kufikiri kila mtu anajua, lakini siyo kweli. Hivyo kama kuna kazi unataka ifanyike ielezee kwa kina ni nini hasa unataka kifanyike.

16. Kusikiliza kuna sehemu mbili, sanaa na ukimya na vyote ni muhimu. Kusikiliza sio kukaa kimya pekee, bali kufuatilia kwa kina kile ambacho mtu mwingine anaongea. Sikiliza kwa makini na siyo tu usubirie kujibu. Utajifunza mengi sana kwa kusikiliza.

17. Tengeneza mawasiliano yako kulingana na yule au wale unaowasiliana nao. Inapokuja kwenye mawasiliano, kuwa kama kinyonga, andaa ujumbe wako ambao utaendana na hadhira yako. jua watu wanapendelea au wanaelewa zaidi kwa njia ipi na itumie.

18. Tumia maneno matatu ya maajabu, TAFADHALI, ASANTE na SAMAHANI. Haya ni maneno matatu ambayo yanaweza kuleta muujiza mkubwa sana kwenye hali yoyote ile. Hakikisha unayatumia kila unapohitaji kupata kitu kutoka kwa mtu mwingine.

19. Funga mdomo wako. Kadiri unavyoongea sana ndivyo inavyokuwa rahisi kwako kuongea mambo ambayo siyo muhimu, na yakakufanya uonekane siyo makini. Funga mdomo wako na ongea yale ambayo ni muhimu tu.

20. Kuwa mjanja kwenye kuuliza maswali ya kijinga. Kuna wakati utahitaji kuuliza swali lakini ukaona swali hilo ni la kijinga, kwa maana huenda kila mtu anajua kasoro wewe tu. Ni vyema ukajifunza njia bora ya kuuliza maswali haya kuliko kukaa kimya halafu ukaenda kuharibu kazi.

21. Jifunze jinsi ya kuongea mbele ya wengine bila ya kutumia vilevi. Hofu namba moja kwa watu wengi ni kuongea mbele ya wengine. Kuna watu wako radhi wazikwe wakiwa hai kuliko kuongea mbele ya watu wengi. Lakini kwenye kazi yako utahitaji kuongea mbele ya watu katika kuwashawishi kuhusu kitu unachotaka kufanya. Jifunze jinsi ya kuepuka hofu hii bila ya kutumia vilevi, na njia bora ni kujiandaa vyema.

22. Vitabu vinahukumiwa kwa mwonekano wake wa nje, na wewe pia. Watu watakuhukumu kwa mwonekano wako wa nje, huna jinsi ya kukwepa hilo. Unapokutana na mtu ndani ya sekunde kumi za kwanza ameshajua wewe ni mtu wa aina gani na atakuchukuliaje. Hivyo hakikisha unaniweka kwenye hali ambayo watu watakuhukumu kama unavyotaka wakuhukumu, hasa unapokutana nao kwa mara ya kwanza.

23. Usiwe mtu wa mwisho kujua maendeleo yako. kwenye eneo lako la kazi, watu wanaweza kuwa na taarifa nyingi kuhusu wewe kuliko hata unavyojijua wewe mwenyewe, hasa kwenye ufanyaji wako wa kazi. Usijifungie mwenyewe kwa kufikiri unafanya kazi bora sana, badala yake omba mrejesho kwa wengine, kuhusu ufanyaji wako wa kazi.

24. Usimvumilie bosi mwonevu, kama itakubidi ni bora ukaacha kazi. Kama ilivyo kwa tabia tofauti za wanadamu, unaweza kukutana na bosi ambaye ni mwonevu na akawa anakunyanyasa sana. Kama utavumilia manyanyaso hayo kwa sababu unataka kuendelea kuwa na kazi hiyo unatakiwa kujua kitu kimoja, ndiyo atazidi kukunyanyasa. Badala yake mwambie ukweli na kama hatajirekebisha ni bora utafute kazi nyingine.

25. Huhitaji kuwa rafiki wa kila mtu, hiyo ni kazi ya mbwa. Ukitaka kazi iharibike, hasa kama wewe ni msimamizi na una watu wako chini yako, basi jaribu kumfurahisha kila mtu. Kazi haitaweza kwenda, jua kuna watu watachukia kwa jinsi utakavyopenda mambo yaende, lakini ni lazima yaende.

26. Mtu anayekutesa anaweza kuwa mwalimu wako mkubwa. Kuna watu utakaokutana nao kwenye kazi ambao hamtaweza kwenda pamoja, lakini pia watu hawa watakupa fundisho kubwa sana kwa jinsi gani ya kuenda na watu ambao hamuendani.

27. Jua wapi pa kuchora mstari kati ya kujiendeleza na kujiharibu. Kukosoa mwenyewe ni moja ya njia za kujiendeleza, lakini pale unapojikosoa kupita kiasi unaishia kujiharibu kwa sababu utashindwa kufanya jambo lolote kubwa kwenye kazi zako.

28. Kuwa mtulivu unapokuwa kwenye kikaango. Unapofanya makosa, au unapokosolewa au unapopewa taarifa ya maendeleo yako ya kazi, usikubali hisia zako zikutawale na kuanza kulaumu au kujitetea. Badala yake kaa kimya, tafakari hali hiyo unayopitia na ona ni kipi bora kufanya. Ukikubali hisia zikutawale utaharibu mengi.

29. Jifunze sheria ambazo hazijaandikwa kwenye eneo lako la kazi. Kuna sheria na taratibu kwenye eneo lako la kazi ambazo zimeandikwa. Na kuna nyingine nyingi ambazo hazijaandikwa popote, wala hakuna atakayekuambia, bali utaona kuna vitu ambavyo watu huwa wanafanya na vingine huwa hawafanyi. Utajifunza sheria hizi kwa kuwa mtazamaji mzuri wa mambo yanavyoendeshwa kwenye eneo lako la kazi.

30. Vichwa viwili ni bora kuliko kimoja, hakikisha unakuwa na mshauri. Kwenye eneo lako la kazi, tafuta mshauri, mtu ambaye ana uzoefu kwenye kazi hiyo na pia ana heshimika na wengine. Huyu atakusaidia kujua ni mambo yapi muhimu kuzingatia ili uweze kufanikiwa kupitia kazi yako.

31. Usiogope hofu ya kushindwa ikuzuie kufanya makubwa. kama unapata nafasi ya kukutana na bosi mkubwa wa eneo lako la kazi, usikubali hofu ikuzuie kujieleza wewe ni nani na unafanya nini. Hii ni njia nzuri ya kujenga mtandao wako.

32. Linapokuja swala la UMBEYA, jifunze njia ya kuukwepa. Hakuna sumu kubwa kwenye eneo la kazi kama umbeya. Usikubali kabisa kujihusisha kwenye umbeya au majungu ya aina yoyote. Mtu anapokuletea habari za mtu mwingine, muulize je umeshamwambia mhusika habari hizo? Usikubali kujadili mtu ambaye hayupo, na lolote utakalosema kuhusu mtu, hakikisha ungeweza kulisema mbele yake pia.

33. Fikiri kwa kina kabla hujaamua kumshitaki bosi wako. Kwa sababu baada ya mashitaka haya mahusiano yenu hayatakuwa tena mazuri, hivyo hakikisha ni jambo lenye ushahidi na hatua unayochukua wewe ni ya kunusuru kazi nzima.

34. Kuwa makini na mahusiano ya kimapenzi kwenye eneo la kazi. Kwanza kabisa ni vyema ukaepuka kuwa na mahusiano ya kimapenzi kwenye eneo lako la kazi, maana mahusiano yenu yataathiri kazi pia. Na ni marufuku kabisa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mtu unayemsimamia au anayekusimamia wewe, hapo kazi lazima iharibike. Kama itashindikana kuepuka mahusiano hayo, basi yawe na mtu ambaye mpo vitengo tofauti na mkubaliane kazi itakuwa kazi na mapenzi ni mapenzi, japo hilo pia ni gumu sana.

35. Jichukulie wewe kama bidhaa. Kwa njia hii utahitaji kujitangaza ili watu wajue sifa zako na kile ambacho unaweza kufanya. Unahitaji kujitandaza wewe mwenyewe, la sivyo hakuna atakayejua uwepo wako.

36. Geuza mafanikio yako kuwa hadithi. Kama ambavyo tumejifunza hapo juu, ni muhimu kujitangaza. Lakini kujitangaza kwa kujisifia pekee haileti picha nzuri kwa wengine, wengi wataona unaringa. Badala yake geuza mafanikio yako kuwa hadithi ambavyo unaweza kuichomekea kwenye mazungumzo yako na watu wengine. Na wao pia wakaichukua kama hadithi na kuisambaza. Jiulize ni kitu gani kitawafanya watu wakukumbuke, na tengeneza hadithi kwa njia hiyo.

37. Jiandae wakati wowote ule. Hujui ni wakati gani utaipata fursa ya kuongea na mtu ambaye ni muhimu kwa mafanikio yako ya kazi. Hivyo kwa wakati wowote ule kuwa umejiandaa kiasi kwamba mtu akikuuliza wewe ni nani na unafanya nini, uweze kumweleza kwa njia ambayo atashawishika kutaka kukujua zaidi.

38. Tengeneza hadithi mpya, za zamani zinachuja. Usiwe mtu wa kutumia mafanikio fulani uliyoyapata zamani kujisifia kila siku. Watu wakishasikia sana hadithi yako wanaichoka. Mfano ni wale watu ambao wanajisifia kwa vyuo walivyosoma au ufaulu walipata enzi hizo. Watu hawataki kujua miaka 20 iliyopita ulifanya nini, wanataka kujua siku za karibuni umefanya nini.

39. Weka maneno sahihi kwenye midomo ya wengine. Kama kuna mtu ambaye anatakiwa kukutambulisha kwa watu wengine, hakikisha mtu huyo anatoa maelezo sahihi kuhusu wewe. Na njia ya kuhakikisha hilo ni kuwaambia ukweli kuhusu wewe. Usije ukatambulishwa kivingine na wewe ukaja kujitambulisha tofauti.

40. Hakikisha unaonekana hata kama haupo karibu. Kwenye eneo lako la kazi hakikisha watu wanajua uwepo wako hata kama unafanyia kazi mbali. Kama watu hawajui uwepo wako ni rahisi kukusahau kwenye mambo muhimu na ya haraka. Hivyo hata kama upo mbali jua ni watu gani muhimu wa kuendelea kuwasiliana nao na kuwapa maendeleo yako.

41. Wazuie watu wanaoiba sifa zako. Hakuna jambo linaloumiza kwenye eneo la kazi kama wewe ufanye kazi halafu mtu mwingine ndiyo achukue sifa ya kazi yako, kama vile ameifanya yeye. Ukiona mtu amefanya hivyo mwambie wazi kwamba hukufurahishwa na kitendo hiko.

42. Usichukulie kila kinachotokea kwamba kimekusudiwa kwako wewe tu. Watu wengi hupenda kutafuta tafsiri ya kitu ambayo inaonesha kwamba kitu hiko kilifanyika ili kuwaumiza wao. Hii ipo sana wa wanawake. Kwa jambo lolote linalotokea, hutafuta jinsi ya kuliunganisha na wao kuonewa. Ondokana na hisia hizi na jua ukweli wa kila jambo linalotokea.

43. Jali hisia za wengine. Kwenye jambo lolote unalofanya, jali hisia za watu wengine. Hasa unapokuwa bosi au msimamizi unaweza kuwa unafanya mambo ambayo unaona ni sahihi ila yakawa yanaumiza hisia za wengine. Jali hilo sana.

44. Ushindani wa moja kwa moja ni sumu kali. Badala ya kutengeneza mazingira ya ushindani kwenye eneo la kazi, tengeneza mazingira ya ushirikiano. Ushindani na ushirikiano haviwezi kwenda pamoja, kwa kushindana mnaweza kurudishana nyuma lakini kwa kushirikiana mtasonga mbele.

45. Angalia upande chanya. Kwa kila mtu utakayefanya naye kazi, ana ubora wake na pia ana madhaifu yake. Kama utaangalia madhaifu pekee utaona ni mtu ambaye hafai, lakini kama utaangalia mchango wake mzuri utaona ni mtu anayefaa kwenye kazi. Angalia kama ubora wa mtu unazidi mapungufu yake na ona mnaweza kwendaje pamoja.

46. Angalia ubaguzi usikuzamishe. Ubaguzi wa aina yoyote ile kwenye eneo la kazi utakurudisha nyuma. Unapowabagua watu kwa misingi ya imani zao au makabila yao utakosa nafasi nzuri ya kushirikiana nao. Na mara nyingi vigezo ya ubaguzi havipo sawa kwa wote. Unaweza kusema wazaramo ni wavivu, lakini siyo kweli kwamba wazaramo wote ni wavivu. Mchukulie mtu kama mtu na sio kutokana na kabila, rangi au dini yake.

47. Jua ni kipi unakwenda kukutana nacho. Watu wengi wanapokuwa wafanyakazi wa kawaida, huwa wanawalaumu sana mabosi wao, lakini wao wanapokuwa mabosi wanaishia kulalamikiwa kwa kuwa mabosi wabaya. Ukweli ni kwamba wengi wanakuwa hawajajiandaa vyema wanapopewa majukumu makubwa na hivyo kujikuta wakifanya vibaya. Kabla hujakubali majukumu makubwa, jua ni kipi hasa unakwenda kukutana nacho.

48. Meneja mzuri anajua ni wakati gani wa kuongoza. Katika mfumo wa elimu kuna tofauti kati ya kiongozi (leader) na meneja au msimamizi (manager), ya kwamba meneja anasimamia majukumu ya kila siku wakati kiongozi anakuwa na maono ya mbali. Ukweli halisi ni kwamba meneja mzuri ni lazima awe pia kiongozi, na hata kiongozi mzuri nahitaji kuwa meneja. Huwezi kutofautisha vitu hivyo viwili kama unataka kufanikiwa kwenye kazi.

49. Epuka kuwa mjuaji wa yote, msemaji wa yote, na mdhibiti wa yote. Mabosi wengi hujiona wao ndio kila kitu, wao ndio wanajua zaidi kuliko wengine, wao ndio wasemaji wa kuu na wao ndio wanaweza kudhibiti kila kitu. Kama wewe ni bosi au msimamizi na ukawa na mtazamo huu, kazi yako itakuwa ngumu mno. Unahitaji mchango na msaada wa wengine ili kazi yako iweze kwenda vizuri.

50. Watu siyo wasomaji wa mawazo yako. kama kuna kitu unataka sema wazi ni nini unataka. Usifikiri kwamba watu wataelewa ni kipi unataka na kukupa, kila mtu anachanganywa na mambo yake. Sema ni kipi unataka ndiyo utapewa, hakuna awezaje kusoma mawazo yako.

51. Kuwa makini na maneno unayosema hasa unapokuwa bosi. Ukishakuwa bosi kwenye eneo lako la kazi, basi kila neno unaloongea watu watalitafsiri kwa njia zao wenyewe. Kuwa makini na maneno unayoongea, watu wanaweza kuyatafsiri vibaya na ukaleta picha mbaya kwenye eneo la kazi. Hata unapotoa utani, kuwa makini sana.

52. Wachukulie watu wote kwa usawa. Mara nyingi watu wanapopanda vyeo kazini, huona wale waliopo chini yako kama watu wa chini kwao na hivyo hawawapi heshima kama wale ambao wako juu yao. Usiingie kwenye hili, endelea kumheshimu kila mtu kwenye kazi yako, hata kama wewe ni bosi na yeye ni mfagiaji. Kila mtu ni muhimu na kuna wakati atakufaa sana.

53. Kutokujiamini kutakufuata kila unapopanda. Kila unapopanda cheo au kufanya mambo makubwa, kuna hali fulani ya kutokujiamini inakujia. Kwa hali hii unaona kama hustahili kuwa na cheo hiko, au kuona ulibahatisha na kwamba siku moja watu watakustukia na utapoteza sifa yako. hii ni hali ya kawaida, hivyo hakikisha haikuzuii wewe kuendelea kufanya mambo yako.

54. Unyenyekevu utakusaidia sana kwenye safari yako. hata kama umefanikiwa kiasi gani kwenye kazi yako, kuwa mnyenyekevu. Jua kwamba hujui kila kitu na hivyo jipe nafasi ya kujifunza kila siku na kupitia kila mtu. Endelea kujifunza kupitia kazi yako, watu wengine na hata kujisomea.

Haya ndiyo mambo 54 ya kuzingatia kama unataka kuwa na mafanikio makubwa kupitia kazi unayofanya. Pia mambo hayo ni muhimu kwa kila mjasiriamali na mfanyabiashara kuzingatia katika mahusiano yake na wengine na hata mahusiano yake na wafanyakazi wake.

Jifunze mambo haya na yapitie mara kwa mara na kisha fanyia kazi.

Nakutakia kazi njema na yenye mafanikio makubwa.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz