Unapoanza na biashara moja na ukaona inafanya vizuri, unapata mawazo ya kukua zaidi kibiashara, na kufikiria kufungua biashara nyingine mpya.
Hili ni wazo zuri sana kwa sababu huwezi kubaki pale pale kwa siku zote, kama mfanyabiashara makini ni lazima ukue.
Lakini hapa kwenye ukuaji, hasa wa kuanzisha biashara mpya kuna changamoto moja kubwa sana.
Wengi wa wanaoanzisha biashara mpya, huwa zinapelekea kuzorota na hata kufa kwa zile biashara za zamani.
Hivyo unahitaji kuwa makini sana ili na wewe usijekuwa mmoja wa watu hao.
Ili kuepuka biashara yako mpya kuua biashara ya zamani, zingatia mambo haya muhimu sana unapofungua biashara mpya;
1. Usifungue biashara mpya kwa mtaji wa biashara ya zamani. Hili ni kosa ambalo wengi wamekuwa wanafanya na linawagharimu. Usitoe fedha ambayo ni sehemu ya mtaji wa biashara yako na kwenda kuanzisha nayo biashara nyingine. Hapa lazima utaleta mtikisiko kwenye biashara yako.
Badala yake anza biashara yako nyingine kutokana na faida uliyopata kutoka kwenye biashara uliyonayo sasa. Na hii itakuwa iipimo kizuri kwamba kama umeweza kutengeneza faida kubwa kiasi hiko basi unaweza kufungua biashara nyingine. Lakini kama hujaweza kutengeneza faida ya kukuwezesha kufungua biashara nyingine, bado una kazi kubwa yakufanya kwenye biashara yako ya sasa. Usikimbilie kufungua biashara nyingine.
2. Usipunguze usimamizi au uangalizi wa biashara yako ya zamani. Hili ni kosa jingine kubwa ambalo wengi wanafanya, kwa kuwa wanaona biashara inakwenda vizuri wanafikiri haihitaji tena usumamizi wao kwa sana.
Hata biashara yako iwe inakwenda vizuri kiasi gani, bado inahitaji sana usimamizi wako, hasa wa karibu. Hivyo unapofikiria kufungua biashara nyingine mpya, ujue ya kwamba kuna mahali inabidi upate muda wa ziada kwenye siku yako, lakini siyo kupunguza kwenye usimamizi wa biashara yako ya sasa.
Zingatia mambo haya mawili ambayo ni hatari sana kwenye biashara ya zamani pale inapoanzishwa nyingine mpya.
Kila la kheri.
MUHIMU; Kama una changamoto yoyote ya kibiashara iweke kwenye maoni hapo chini ili tuweze kusaidiana.