Kitu Kimoja Kinachowatofautisha Waliofanikiwa Na Walioshindwa, Na Jinsi Unavyoweza Kukitumia Kufikia Mafanikio Makubwa.

Habari rafiki?
Unaposikia mafanikio makubwa ni kitu gani kinakuja kwenye akili yako? umiliki wa mali nyingi? Kuwa na fedha nyingi? Au kuendesha biashara kubwa? Je ni kuwa na familia bora? Au ni kuwa na ushawishi kwa wale wanaokuzunguka? Inawezekana pia ni kuweza kuwasaidia wale wenye matatizo mbalimbali.
Haijalishi ni picha gani inayokuja kwenye mawazo yako, kila mmoja wetu ana maana yake ya mafanikio makubwa, na ni sawa kabisa. Kwa kuwa wote hatuwezi kuwa na malengo sawa, hivyo basi mafanikio yana maana tofauti kwa kila mtu.
Lakini licha ya kuwepo kwa maana tofauti ya mafanikio kwa kila mtu, bado wote tuna kitu kimoja ambacho kinatuleta pamoja katika swala la mafanikio. Na kitu hiko ni kwamba kila mmoja wetu anataka kufikia mafanikio makubwa, kila mmoja wetu anataka kuwa bora leo kuliko alivyokuwa jana. Na huu ndio msingi mkuu wa maisha na ndiyo kinatusukuma wengi kuchukua hatua mbalimbali.
Pamoja na kwamba wote tunataka kufanikiwa, lakini siyo wote tunafanikiwa. Ni wachache sana ambao wanafikia mafanikio makubwa, huku wengine wengi wakishindwa. Sasa hapa ndipo tunapata swali kubwa sana, ni nini kinawatofautisha watu hawa? Ni nini kinawatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa?
Ukiangalia kwa nje, hasa kwa jicho la wanaoshindwa, utaziona sababu nyingi sana za kwa nini wao wameshindwa na wenzao wamefanikiwa. Watakupa sababu kama kutoka familia yenye uwezo, kupata msaada kutoka kwa wengine, kuwa na kipaji na kile wanachofanya na wengine watasema kuwa na bahati. Kwa nje ni rahisi kuyaona hayo, lakini kwa bahati mbaya sana, siyo kweli.

http://www.amkamtanzania.com/2016/04/semina-utoaji-wa-huduma-bora-kwa-wateja.html
KUJIUNGA NASEMINA HII NZURI SANA KWAKO BONYEZA HIYO PICHA AU BONYEZA MAANDISHI HAYA

 
Kuna sababu moja kubwa sana kwa nini baadhi ya watu wanafanikiwa na wengine wengi wanashindwa. Sababu hii ipo wazi, ila wale wanaoshindwa huwa hawaijui, na hata wakiijua huwa hawaipendi, kwa sababu hawapo tayari kuitumia na hivyo kuona haifai. Lakini wote waliofanikiwa wanakubaliana kabisa na sababu hii moja, kwamba ndiyo imewawezesha kufika pale walipofika licha ya vile ambavyo vinaonekana kwa nje.
Leo kupitia makala hii utakwenda kuijua sababu hii moja, utakwenda kujifunza jinsi unavyoweza kuitumia na wewe pia na kisha utakwenda kufanya maamuzi wewe mwenyewe, ikiwa uitumie au la. Na kama unavyonijua, hakuna kitu ninachokusisitiza kama kuchukua hatua, usifurahie tu kujifunza, badala yake chukua hatua, amua kufanya kitu na ujionee mwenyewe kama inawezekana au la.
Ni kipi kinawatofautisha waliofanikiwa na walioshindwa?
Sababu moja kubwa sana, ambayo inawatofautisha waliofanikiwa na walioshindwa, na inawafanya waliofanikiwa wazidi kufanikiwa na huku ikiwaacha walioshindwa nyuma ni kuwa tayari na kujitoa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa. Najua baada ya kusikia hivyo umesema aah hivyo tu mbona nilikuwa najua mara zote.
Ndiyo ulikuwa unajua ya kwamba mafanikio yanatokana na kazi, lakini kuna makubwa zaidi kuhusu kazi ambayo bado hujayajua, na haya ndiyo yanawawezesha baadhi ya watu kuwa na mafanikio makubwa.
SOMA; Sababu Tatu(3) Zinazokuzuia Kufanikiwa Kwenye Kazi Unayofanya.
Watu wote waliofikia mafanikio makubwa, licha ya sababu nyingine tunazoziona kwa nje, ni watu ambao wanafanya kazi mno. Ni watu ambao wamejitoa moja kwa moja kwenye kuweka kazi kubwa, kwa juhudi na maarifa mpaka wapate kile ambacho wanakitaka.
Watu hawa wanajua ya kwamba kushindwa ni moja ya vitu vinavyoweza kutokea, lakini siyo sababu ya kukata tamaa. Na hivyo huendelea kufanya tena na tena na tena hata baada ya kushindwa mara nyingi sana. Katika hali kama hiyo wale walioshindwa wanakuwa wameshakata tamaa na kuacha, hawa wenzao wanaendelea kuweka juhudi kubwa.
Kitu kingine kikubwa usichokijua kuhusu kazi ni kwamba watu waliofanikiwa, wana miaka mingi ambayo walikuwa wanafanya kazi bila ya kuonekana na watu. Kuna wakati walikuwa wamejichimbia, wanafanya kazi usiku na mchana, na hakuna hata aliyekuwa anawaona, na baadaye kazi zile zinakuja kuwazalishia kwa kiasi kikubwa.
Pia watu hawa walikuwa tayari kukosa baadhi ya mambo ya kijamii, wakaacha kukaa vijiweni kupiga soga, au kukutana bar kila jioni kwa kunywa na marafiki. Wakasahau kuhusu tv na kushinda kwenye mitandao ya kijamii. Wakaweka akili zao na nguvu zao katika kazi ambayo wanaifanya, na baada ya muda matokeo makubwa yakaanza kuonekana.
Ni kazi rafiki yangu, kazi hasa, siyo ile ya kutaka kuonekana, bali kazi ya ukweli, ambayo inatoka moyoni, ndiyo inawatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa. Hizi sababu nyingine za nje kama kusaidiwa, bahati, vipaji mwisho wa siku haviwezi kufua dafu kwenye kazi.
Ndiyo maana kuna watu wamerithi mali nyingi sana lakini wameishia kushindwa kabisa kwenye maisha. Kuna watu ambao wamezaliwa na vipaji vizuri lakini maisha yanawapiga. Na pia kuna wengine wengi ambao wana elimu kubwa, maarifa mazuri lakini hakuna kikubwa walichoweza kufanikisha.
Hakuna kitu kinachoweza kuzidi kazi, ni kweli unahitaji vitu vingine muhimu sana ili kufikia mafanikio, ila hivi vyote vitakuwa na maana kama utakuwa tayari kuweka kazi, na ni kazi ya maana siyo ya kitoto.
Ufanye nini rafiki yangu?
Jitoe kufanya kazi, kazi kubwa kwa kutumia maarifa na nguvu zako zote. Chagua lile eneo ambalo unataka kufikia mafanikio makubwa, kama ni biashara sawa, kama ni ajira sawa, kama ni familia yako au shughuli nyingine ya kijamii sawa.
Ukishachagua kile unachotaka kufanikiwa, sasa jiambie ya kwamba unakwenda kuweka kazi mpaka ukifikie, amua ya kwamba hakuna kitu chochote kitakachokurudisha nyuma katika kufikia kile ulichochagua. Na weka kazi, funga mdomo, acha kupiga kelele na fanya kazi.
SOMA; Hii Ndio Kazi Inayolipa Sana Ambayo Hata Wewe Unaweza Kuifanya.
Na ukishachagua njia hii jua kabisa ya kwamba kuna watu wengi watakaokupiga na kukukatisha tamaa na pia kuna shughuli nyingi za kijamii ulizokuwa unapenda kufanya kwa sasa utazikosa. Kubaliana na hilo na anza kuweka kazi.
Na muhimu sana kuzingatia sisemi uparamie kazi na kuanza kufanya, bali uweke malengo na mipango ambayo utaifanyia kazi. Ni lazima uwe na picha kubwa kwenye akili yako ya wapi unapotaka kufika. Ni lazima uwe na maarifa sahihi, na kila siku uendelee kuongeza maarifa hayo kupitia kujifunza. Na pia ni lazima ujifanyie tathmini kila mara ya ulikotoka, ulipo sasa na kule unakotaka kufika.
Ninaamini umetoka na kitu hapa leo rafiki yangu, nina uhakika pamoja na kujua umuhimu wa kazi, leo umeongeza sababu nyingine kwa nini ujitoe sana. Na ninajua utakwenda kujitoa na kufanya makubwa sana. Na tutakutana pamoja kwenye kilele cha mafanikio.
Nakutakia kila la kheri katika utekelezaji wa haya ambayo umeondoka nayo, nasisitiza tena, kufanya ndiyo kutakusaidia.
TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: