Katika majumuiko yetu na watu wengine, tumekuwa tukiwahukumu kwa hali ambazo siyo kweli. Hata sisi wenyewe pia, tumekuwa tunajihukumu kwa hali ambazo siyo kweli.
Moja ya njia tunazowahukumu nazo wengine na hata sisi wenyewe pia ni kutumia kauli kama MARA ZOTE, KILA MARA au DAIMA…
Mara zote wewe umekuwa unachelewa…
Kila mara wewe ndiyo unafanya makosa….
Daima umekuwa mtu wa roho mbaya…
Na mengine mengi.
Katika kuhukumu huku, tunachukua tabia ambayo mtu ameifanya, labda mara nyingi halafu tunasema ndiyo tabia ambayo anafanya kila mara au daima. Kitu ambacho siyo sahihi kabisa.
Hakuna mtu yeyote duniani ambaye MARA ZOTE, KILA MARA au DAIMA anafanya kitu fulani, hakuna. Hata kama mtu anakosea mara nyingi kiasi gani, kuna wakati anakuwa sahihi. Hata kama mtu anachelewa kiasi gani, kuna wakati anawahi. Na kinyume chake pia.
Lakini kwa sababu sisi hatuna muda wa kuangalia na kufuatilia kila kitu, tunachukua kile ambacho tumekiona na kujumuisha ndicho kinachotokea mara zote, kila mara au daima.
Kuanzia sasa, acha kutumia kauli hizo kwa wengine na hata kwako pia. Utaimarisha mahusiano yako na wengine na hata kujiamini wewe mwenyewe pia. Maana unapoona mtu fulani mara zote yupo hivi, inaleta hali ya kutokuaminiana na pia kuweka makundi yasiyo ya msingi.
SOMA; Hakuna Aliye Bora Au Hovyo Zaidi Yako.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba hakuna mtu ambaye MARA ZOTE, KILA MARA au DAIMA ni mtu wa aina fulani au tabia fulani. Watu ni mchanganyiko wa vitu vingi, hakuna anayefanya makosa mara zote na pia hakuna ambaye yupo sahihi mara zote. Nitaacha kuyatumia maneno hayo kwa watu na hata kwangu mwenyewe ili kuacha kutengeneza makundi yasiyo ya kweli.
NENO LA LEO.
Nobody is perfect, and nobody deserves to be perfect. Nobody has it easy, everyone has issues. You never know what people are going through. So pause before you start judging, mocking or criticizing others. Everybody is fighting their own unique war!
Hakuna aliyekamilika, hakuna anayestahili kukamilika. Hakuna ambaye mambo ni marahisi kwake, kila mtu ana changamoto zake. Huwezi kujua ni mambo gani wengine wanapitia. Hivyo subiri kabla hujaanza kuhukumu, kufanya mzaha au kukosoa wengine. Kila mmoja anapigana vita yake mwenyewe.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.