Kama unaendesha biashara ndogo ambayo unategemea siku moja ikue, basi jambo kubwa la kuzingatia kuanzia sasa ni kutengeneza mfumo bora wa wafanyakazi kwenye biashara yako. na kama tayari biashara yako ni kubwa, unahitaji kuwa na mfumo bora wa ufanyaji kazi kwenye biashara yako.

Jambo hili ni muhimu kwa sababu wafanyabiashara wengi wamekuwa hawalipi uzito na baadaye linawaingiza kwenye matatizo makubwa. Moja ya matatizo ambayo wafanyabiashara wengi wanaingia ni kutegemea wafanyakazi wachache katika kukuza biashara zao. Na hivyo inapotokea wafanyakazi hawa wameshindwa kuwepo kazini basi biashara zao zinaathirika kwa kiasi kikubwa sana. Na iwapo wafanyakazi wanaamua kuacha kazi basi mambo yanakuwa mabaya zaidi.

Ni muhimu wewe kama mfanyabiashara ukaelewa kwamba ili biashara yako iweze kujiendesha vizuri na kwa mafanikio, basi haipaswi kuterereka kutokana na kutetereka kwa mtu yeyote anayefanya kazi kwenye biashara hiyo, hata kama ni wewe mmiliki wa biashara. Na unaweza kufanya hili kwa kutengeneza mifumo bora kwa wafanyakazi wa biashara yako.

Yafuatayo ni mambo muhimu kuzingatia ili kutengeneza mfumo bora wa wafanyakazi kwenye biashara yako.

1. Tengeneza majukumu ya kazi kulingana na mahitaji ya biashara yako.

Moja ya makosa ambayo wafanyabiashara wengi huwa wanafanya wanapoajiri ni kumuajiri mtu kama mtu na hivyo mfanyakazi anajitengenezea majukumu yake ya kazi kutokana na kile ambacho anahitajika kufanya kila siku. Sasa inapotokea mfanyakazi huyu amekosekana, hata akija mwingine anashindwa kuziba pengo lake. Hali hii inapelekea biashara kuyumba.

Kuondokana na hali hii tengeneza majukumu ya kazi kabla hata hujaajiri msaidizi kwenye biashara yako. Jua mtu unayemuajiri atafanya kipi na kipi, jua ni yapi anatakiwa kukamilisha na mipaka ya wajibu wake wa kazi ni ipi. Kwa njia hii unaweza kuwafuatilia wafanyakazi wako vizuri na hata inapotokea mfanyakazi hayupo basi ni rahisi kumpata mwingine wa kuziba pengo lake.

2. Tengeneza mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wako.

Tatizo kubwa la biashara nyingi katika kuajiri, hasa biashara ndogo ni kwamba ajira zinakwenda kwa makubaliano ya mdomo. Kwamba mnakubaliana atafanya kazi na utamlipa kiasi fulani. Inapotokea changamoto, mfanyakazi wako anaweza kuamua kuondoka na akakuacha bado hujajiandaa na hili litaathiri biashara yako.

Kwa kuwa na mkataba kutawalinda wote wawili, yaani wewe mfanyabiashara na hata mwajiri wako pia. Iwapo mwajiri atataka kuacha kazi, hataweza kuondoka ghafla kabla mkataba wake haujaisha na hivyo utapata muda wa kuandaa mtu wa kuziba pengo lake. Usione mkataba kama njia ngumu kwako, bali utakuepusha na usumbufu usio na msingi.

3. Mara zote kuwa unaangalia watu bora wa kukusaidia kwenye biashara yako.

Ukishaajiri na kupata wafanyakazi wazuri wa biashara yako usijisahau na kuona kila kitu kimekamilika. Zoezi la kuajiri kwenye biashara ni endelevu, kwa sababu huna uhakika na kila mfanyakazi wako. Japo unaweza kuwa umeingia nao mkataba, lakini jambo lolote linaweza kutokea. Na wewe hutaki jambo lolote litokee na kukukuta huna maandalizi yoyote.

Hivyo kila wakati unaweza kuwa unaendelea kuangalia watu bora wa kuajiri kwenye biashara yako, kuwa na wasifu wao karibu na inapotokea unahitaji mtu wa kuajiri basi unakuwa na sehemu nzuri ya kuchagua.

4. Tengeneza mazingira mazuri ya kazi kwa wafanyakazi wako.

Ukishaajiri wafanyakazi bora, bado una kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha kweli wanafanya kazi bora kwa biashara yako. Na hili linakutaka wewe uweke juhudi kubwa na sio tu kuongeza mshahara. Ukweli ni kwamba mfanyakazi wako atatumia muda mwingi wa siku yake kwenye biashara yako kuliko sehemu nyingine ya maisha yake. Hivyo ni vyema ukayafanya mazingira ya biashara yako kuwa rafiki kwake na akajiona yupo sehemu bora. Na hapa kuna mambo mengi sana kama kutambua mchango wake, kumsifia anapofanya vizuri na hata kumtia moyo.

Kupata wafanyakazi bora kwenye biashara yako, na kuendelea kuwa nao kwa muda mrefu ni kitu ambacho kinahitaji uwe na mfumo mzuri kwa wafanyakazi wa biashara yako. bila ya mfumo mzuri utajikuta unasumbuka kila siku na wafanyakazi wanaiyumbisha biashara yako. Fanyia kazi haya ambayo umejifunza na endelea kufanya biashara yako kuwa sehemu nzuri kwa wale wanaokusaidia kwenye kazi.