Jana kuna watu wengi wameweza kufanya mambo yao vizuri tu bila ya wewe kuwepo. Kuna siku ambazo hukuweza kwenda kwenye kazi yako au biashara yako na waliopo chini yako waliweza kufanya kazi zao bila ya matatizo.
Mtoto wako au mdogo wako au yeyote ambaye yuko chini ya uangalizi wako kuna wakati ameweza kufanya maamuzi muhimu kwake bila hata ya wewe kuwepo.
Ninachotaka kukuambia hapa ni nini?
Najua umekuwa unajaribu kuwa kiranja wa dunia nzima. Kwamba ili kitu kifanyike vizuri ni lazima wewe uwepo, ukifanye wewe mwenyewe au ukisimamie kwa karibu. Hizi ni hisia ambazo watu wengi wanakuwa nazo na zinawanyima uhuru, kuwachosha na kushindwa kuwaamini wengine.
Unachotakiwa kujua ni kwamba watu wengine pia wanaweza kufanya majukumu yao vizuri bila ya wewe kuwepo moja kwa moja. Muhimu ni wewe kuwaelekeza vizuri ni kipi wanachopaswa kufanya kisha wape uhuru wa kufanya, bila ya wewe kuwepo moja kwa moja.
Hofu yako ni kwamba watakosea, ndiyo lazima watakosea, lakini ni kupitia makosa yao ndiyo watajifunza zaidi. Na wanapoanza na makosa madogo ndivyo wanavyoweza kuepuka makosa makubwa. Lakini kama utawazuia kabisa kufanya makosa madogo madogo, watakuja kufanya makosa makubwa ambayo yatawagharimu sana.
Hii ni kwa wote ambao wanasimamia wengine, wameajiri wengine, wazazi na walezi na mtu yeyote ambaye anapenda kudhibiti na kusimamia kila kitu. Huwezi kuwa kiranja wa dunia nzima, utaumia na kuwazuia wengine kukua. Hakikisha watu wanajua wajibu wao kisha wape uhuru. Wanafanya vizuri zaidi wakiwa na uhuru kuliko wakiwa wanasimamiwa kwa karibu sana.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Njia Bora Ya Kujenga Upendo Wako Kwa Wengine.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba nimekuwa najaribu kuwa kiranja wa dunia. Nimekuwa nakazana kuhakikisha kila kitu nakifanya mimi mwenyewe au nakisimamia mwenyewe. Lakini hili limekuwa linaniumiza na kunichosha na pia linawanyima wengine fursa ya kujifunza, kukua na kufanya kwa uhuru. Kuanzia sasa nitahakikisha wengine wanayajua majukumu yao vizuri kisha ninawapa uhuru wa kuyafanya wao wenyewe.
NENO LA LEO.
“There is no greater power and support you can give someone than to look them in the eye, and with sincerity/conviction say, ‘I believe in you.” ― Ken Poirot
Hakuna nguvu kubwa na msaada unaoweza kumpa mtu kama kumwangalia machoni kwa uaminifu na ushawishi na kumwambia NINAKUAMINI.
Amini kwamba wengine wanaweza kufanya makubwa bila ya kusimamiwa moja kwa moja na wewe. Wape uhuru wa kufanya kile wanachopenda kufanya.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.