Hakuna wakati mzuri wa kupima ukuaji wetu, kupima maendeleo yetu binafsi kama wakati ambapo tunapitia changamoto.
Mambo yanapokuwa shwari hakuna tatizo, kila kitu kinakwenda kilivyopangwa na hata mtu wa kawaida ataonekana ni bora kwenye nyakati hizo.
Lakini mambo yanapokuwa magumu, changamoto zinapoibuka, hapa ndipo tunapowajua wale wa tofauti, wale waliojitoa kweli na wale ambao wapo wapo tu.
Na katika changamoto yoyote kuna njia mbili za kupambana nayo, kuna njia rahisi na kuna njia sahihi. Hizi ni njia mbili tofauti kabisa, na haziwezi kuwa pamoja, ni unachagua kufanya kilicho rahisi au kufanya kilicho sahihi.
Wakati wa changamoto kuna njia nyingi rahisi kuchukua. Kukataa changamoto, kutafuta mtu wa kumlaumu juu ya changamoto hiyo, kukata tamaa na kuacha na kuamua kuiacha mpaka itakapoondoka yenyewe. Njia rahisi inaweza kuwa rahisi sasa, lakini baadaye ina madhara makubwa sana.
Pia wakati wa changamoto kuna njia sahihi za kuchukua, kutafuta kiini cha changamoto, kujiuliza umechangiaje changamoto hiyo na kujitoa kuifanyia kazi changamoto ili uweze kusonga mbele. Njia sahihi ni ngumu mwanzoni ila ina manufaa makubwa sana kwa baadaye.
Mara zote unapojikuta kwenye changamoto, au unapokuwa njia panda, na kuna njia rahisi na njia sahihi, chukua njia sahihi. Usijali inakuumizaje kwa sasa, njia sahihi ndiyo itakayokutoa, nyingine zitakupotezea tu muda na nguvu zako.
SOMA; SIRI YA 40 YA MAFANIKIO; Chagua Uwanja Sahihi Wa Mapambano
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba kwenye changamoto ninazokutana nazo, kuna njia rahisi na njia sahihi. Njia rahisi ni rahisi mwanzoni lakini baadaye inaniletea changamoto zaidi. Na njia sahihi ni ngumu mwanzoni lakini itaniletea faida kubwa zaidi. Kuanzia sasa nitakuwa nachukua njia sahihi, bila ya kujali nipo kwenye mazingira gani.
NENO LA LEO.
Have the courage to say no. Have the courage to face the truth. Do the right thing because it is right. These are the magic keys to living your life with integrity. W. Clement Stone
Kuwa na ujasiri wa kusema hapana. Kuwa na ujasiri wa kukubali ukweli. Fanya kilicho sahihi kwa sababu ni sahihi. Hizi ni funguo za kuishi maisha ya uadilifu.
Mara zote fanya kile ambacho ni sahihi, usikimbilie kufanya kile ambacho ni rahisi.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.