Unapoweka mipango yako ya kibiashara, ni lazima uwe na makadirio. Na linapokuja swala la fedha kuna makadirio mengi ambayo huwa tunayafanya kama wafanyabiashara.
Tunakadiria matumizi yetu ya kibiashara, na pia tunakadiria mapato yetu na faida pia.
Kitu kimoja cha kushangaza sana kuhusu makadirio yetu ni kwamba huwa siyo sahihi, karibu mara zote.
Huwa tunaweka makadirio ya chini sana kwenye matumizi yetu. Yaani huwa tunajikuta matumizi yetu kwa uhalisia yanakuwa zaidi ya yale ambayo tulikadiria awali.
Na pia huwa tunaweka makadirio ya juu kwenye kipato chetu au faida. Yaani kile ambacho tunakuja kupata kweli, kinakuwa kidogo sana ukilinganisha na tulivyokadiria.
Sasa haya yanaleta changamoto sana pale unapoendesha biashara kwa mtaji kidogo, utajikuta mambo mengi yanakwama na inaweza kupelekea biashara yako kufa.
Hivyo ni vyema kuanzia sasa unapoweka makadirio yako, lilete hili kwenye akili yako na jiandae kwa kuwa na mpango mbadala kama matarajio yako yatakwenda tofauti na ulivyokuwa umepanga.
Biashara siyo tu kuuza na kununua, kuna vitu vidogo vidogo kama hivi ambavyo vinaumuhimu mkubwa sana kwenye biashara yako.
Kila la kheri.
Kocha.