Sababu Tano (5) Kwa Nini Ni Muhimu Sana Kila Mtu Awe Na Blogu Yake.

Habari za wakati huu rafiki yangu?
Nina imani kubwa ya kwamba unaendelea vyema na unaendelea kufanyia kazi yale ambayo umekuwa unajifunza kila siku kupitia AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA ili kuboresha maisha yako. Hongera sana kwa hatua hii muhimu ambayo umekuwa unachukua, kwa sababu hakuna mwingine wa kuyafanya maisha yako kuwa bora isipokuwa wewe mwenyewe.
Leo nataka nikushirikishe kitu kimoja muhimu sana ambacho kama utakwenda kufanyia kazi basi utayafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Kitu hiko ni kwamba kila mtu anatakiwa kuwa na blogu, ndiyo namaanisha hata wewe unahitaji kuwa na blogu yako. Na kabla hatujaangalia kwa undani kuhusu blog, tuangalie kingine muhimu sana ambacho ndiyo kinasababisha uwe na blog yako.
Ni muhimu sana kila mmoja wetu akawa anaandika kila siku, haijalishi unaandika kuhusu nini, lakini zoezi la kuandika kila siku litakubadilisha na kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Unapojiwekea utaratibu wa kuandika kila siku, na ukaufuata unakuwa umejijengea nidhamu nzuri sana ambayo itakuwezesha pia kufanya mambo mengine makubwa.
Je kwa nini ni muhimu kwa kila mtu kuwa na blog?
Mwaka 2014 kupitia AMKA MTANZANIA niliendesha semina kwa njia ya mtandao iliyoitwa JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG. Watu wengi walishiriki semina ile na walijifunza mambo yote muhimu kuhusu blog. Na baada ya semina ile wengi walichukua hatua ya kuanzisha blog zao na wengi wanaendelea kuzikuza. Kuna ambao tayari wamepata nafasi za kuandika makala kwenye magazeti mbalimbali na yote hii ilitokana na kazi walizofanya kupitia blog zao.
Ni muhimu sana hata wewe uwe na blog yako kama bado kwa sababu zifuatazo;
1. Kama unafanya biashara basi blog ni sehemu muhimu ya biashara yako.
Kama ulikuwa hujajua ni kwamba watu wengi sasa wanatumia mtandao wa intaneti, na kadiri siku zinavyozidi kwenda idadi ya watumiaji wa intaneti inazidi kukua. Hivyo wateja wa biashara yako wapo kwenye mtandao wa intaneti. Na wanapokuwa na shida inayohusiana na biashara yako wanaingia kwenye google na kutafuta. Sasa kama wewe una blog ambayo inaelezea kuhusu biashara yako na jinsi inavyoweza kuwatatulia watu matatizo yao, blog yako itaonekana kwenye google na mteja huyu atakutafuta zaidi.
Hakuna kosa kubwa mfanyabiashara yeyote anaweza kulifanya kwenye karne hii kama kugoma kutumia mtandao wa intaneti kukuza biashara zake. Ujio wa mtandao wa intaneti na ukuaji wa mitandao ya kijamii ni mapinduzi makubwa sana.
2. Kama umeajiriwa au ni mtaalamu wa kitu fulani basi blog inakuwezesha kuwa na mchango kwa jamii kupitia taaluma yako.
Umuhimu wa blog hauishii kwa wafanyabiashara pekee, bali pia unakwenda kwa wote wenye utaalamu fulani. Iwe wameajiriwa au wamejiajiri wenyewe, kama una taaluma yoyote ambayo ina mchango kwa jamii, unaweza kutumia blog kutoa mchango huo na kujijengea hadhira ambayo baadae unaweza kuifanya kuwa biashara.
Kwa mfano kama wewe ni mtaalamu wa afya unaweza kuwa na blog inayoandika kuhusu mambo ya afya na jinsi gani jamii inaweza kuwa na afya bora, kuepuka magonjwa na mambo mengine muhimu kuhusu afya.
Kama wewe ni mwanasheria unaweza kuwa unatoa elimu kwa jamii kuhusu mambo ya kisheria, kwa kuwa wengi hawapati uelewa huo.
Kama wewe ni mwalimu, unaweza kutumia blog yako kuandika kuhusu maendeleo ya elimu, mchango wa wazazi, jamii na mfumo wa elimu katika kuboresha elimu ya watoto. Pia unaweza kuandika kuhusu malezi ya watoto kutokana na changamoto unazokutana nazo kila siku.
Taaluma yoyote ile uliyonayo, kuna namna ambavyo jamii inaweza kunufaika na njia ya wewe kuinufaisha jamii ni kuwa na blog.
Uzuri wa kuwa na blog unayoandikia kuhusu taaluma yako ni kwamba kadiri unavyotoa elimu, watu wengi zaidi watakutegemea na baadaye watataka ushauri zaidi kutoka kwako na hapo unaweza kutoza gharama.
3. Ni njia ya wewe kujijengea nidhamu binafsi.
Unapokuwa na blog, na ukapanga uandike kila siku, au mara tatu kwa wiki, au hata mara moja, halitakuwa zoezi rahisi. Lakini utakapokazana na kuweza kuandika kama ambavyo umejipangia wewe mwenyewe, utakuwa umeweza kujijengea nidhamu binafsi. Nidhamu hii itakusaidia kwenye maeneo mengine mengi ya maisha yako. Kuacha mambo mengine yote ambayo ulikuwa unaona ni muhimu sana kwako kufanya, na kukaa chini ili uandike ni jambo la kishujaa sana, litakujengea kujiamini na utaweza kufanya mengi na makubwa.
4. Ni njia ya kujitengenezea ushindi.
Kama unataka kuwa na ushindi kila siku, basi anza kuandika kila siku. Siku zetu zinatofautiana sana, kuna siku utaweka mipango yako na utaitekeleza vizuri ila kuna siku utaweka mipango na hutaweza kuitekeleza kutokana na changamoto mbalimbali. Sasa siku kama hizo ambazo unashindwa kutekeleza mipango yako unaweza kuona kama umezipoteza. Lakini kama utakuwa umeianza siku hiyo kwa kuandika, mwisho wa siku utakapokuwa unaitafakari siku yako utaona kwamba uliweza kuandika, na hii inakupa ushindi mkubwa sana. Itakuzuia kukata tamaa na itakuhamasisha kuendelea kufanya tena na tena.
5. Njia ya kujipatia kipato.
Sababu nyingine muhimu ya wewe kuwa na blog ni kujipatia kipato. Unaweza kuitumia blog yako kama njia ya kujipatia kipato. Lakini hii haianzi haraka, siyo kwamba ukifungua blog leo basi unaanza kuingiza kipato. Bali inakuhitaji muda, ufanye kazi na uanze kujijengea wasomaji ambao wanakufuatilia kisha waanze kuhitaji zaidi kutoka kwako na hapo unaweza kujitengenezea kipato. Zipo njia tofauti za kujitengenezea kipato ambazo nimezielezea kwa kina kwenye kitabu JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG 
Uchukue hatua gani?
Hatua ya kuchukua ni leo hii wewe kufungua blog yako na kuanz akuandika. Chagua eneo ambalo unapendelea kuliongelea au unapenda kujifunza zaidi na anza kuliandikia.
Lakini mimi sina uelewa wowote kuhusu blog, hilo siyo tatizo. Unaweza kujifunza mwenyewe jinsi ya kuanzisha bloga yako na siyo ngumu. Kwenye kitabu JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG nimeeleza kwa kiswahili rahisi jinsi unavyoweza kufungua blog yako mwenyewe. Kuna maelekezo kabisa ya picha ya jinsi ya kufanya hivyo.
Jipatie kitabu hiko kwa gharama ya tsh elfu kumi (10,000/=). Kupata kitabu hiki tuma fedha tsh elfu 10 kwenye namba 0717396253 au 0755953887 na kisha tuma ujumbe wenye email yako na maelezo kwamba unataka kitabu cha blog na utatumiwa kitabu hiko mara moja. Fanya hivyo sasa hivi.
Na ikiwa hutaki kujitengenezea blog yako mwenyewe basi ninaweza kukutengenezea blog nzuri sana na iliyokamilika na pia kukushauri vizuri kuhusu blog hiyo. Tuwasiliane kwa maelezo zaidi kama unataka msaada huo wa kutengenezewa blog.
Kwa vyovyote vile hakikisha unakuwa na blog yako na unaandika kila siku, au mara kwa mara kama kila siku haiwezekani, hata kama hutapata fedha, bado utanufaika zaidi wewe binafsi.
Chukua hatua kwa haya ambayo umejifunza, jipatie kitabu cha blog au tuwasiliane ili niweze kukutengenezea blog nzuri.
Nakutakia kila la kheri.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: