Kuna maeneo mengi sana ya maisha yako ambayo huwezi kutumia neno kamwe. Na hii ni kwa sababu mambo mengi yanaweza kutokea bila ya wewe kuwa na maamuzi ya moja kwa moja. Unaweza kusema kamwe sitofanya kitu fulani, lakini ukajikuta kwenye mazingira ambayo inabidi ufanye. Wazungu wanasema NEVER SAY NEVER.

Lakini kuna maeneo ya maisha yako unaweza kusema KAMWE, na haya ni yale maeneo ambayo wewe una udhibiti wa moja kwa moja na yako ndani ya uwezo wako. Leo nakwenda kukushirikisha eneo moja la maisha yako ambalo kuanzia sasa unahitaji kutumia neno kamwe.

Na eneo hili ni kwenye uwezo wako binafsi. Unajua ya kwamba hakuna mtu anayeweza kukuzuia wewe kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako. ni wewe pekee ndiye unayeweza kujizuia.

Hivyo leo nakuambia KAMWE usijiwekee vikwazo na vizuizi kwenye njia yako ya kuelekea kwenye mafanikio. Usijiwekee kikomo chochote, usijiwekee mipaka yoyote kwenye uwezo wako.

Kamwe usiseme mimi siwezi kufikia mafanikio makubwa, usiseme mimi siwezi kuikuza biashara yangu ikawa kubwa.

Kataa kabisa ukomo huu unaotaka kujiwekea kwenye eneo lolote la maisha yako. Chochote unachofikiria sema nitaweka juhudi zangu zote na maarifa niliyonayo na nitakayoendelea kupata mpaka nikifikie kitu hiki. Halafu fanyia kazi.

Kwa kuanza na kikomo unakuwa umeshakata tamaa na huwezi kujaribu zaidi. Lakini unapoondoa vikwazo hivi unajipa uhuru wa kufanya, na unapofanya na ukawa king’ang’anizi, hakuna kinachoweza kukuzuia.

KAMWE USISEME SIWEZI, KAMWE USISEME NITASHINDWA, jua utashinda na weka juhudi na maarifa.

SOMA; Ni Vikwazo Gani Unaendelea Kujiwekea Kwenye Maisha Yako.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba ili niweze kufikia mafanikio makubwa, kwanza ninahitaji kuondoa kabisa vikwazo vyote ambavyo nimekuwa najiwekea mimi mwenyewe. Kuanzia sasa sitosema kwamba siwezi au nitashindwa. Badala yake nitajitoa kwa kuweka juhudi na maarifa mpaka nitakapofika pale ambapo ninataka kufika. Najua ninaweza na nina uhakika nitashinda.

NENO LA LEO.

Don’t limit yourself. Many people limit themselves to what they think they can do. You can go as far as your mind lets you. What you believe, remember, you can achieve. – Mary Kay Ash

Usijiwekee kikomo wewe mwenyewe. Watu wengi wanajiwekea ukomo kwa kile wanachofikiri wanaweza kufanya. Unaweza kwenda mbali zaidi kadiri mawazo yako yanavyoweza kukupeleka. Kumbuka chochote unachoamini unaweza kukifikia.

Kamwe usijiwekee ukomo, jitoe kuweka juhudi na maarifa na utafika popote unapotaka kufika.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.