Jamaa ameanza biashara na mtaji wa laki tano ila kwa sasa anamiliki biashara kubwa ya mtaji wa bilioni….

Jamaa amelima matikiti na sasa hivi una utajiri mkubwa sana….

Hadithi kama hizi zimejaa kila kona ya mazungumzo yetu. Na ni hadithi ambazo wengi wanapenda sana kuzisikia, na zinawahamasisha wengi kweli.

Na wapo wengi wanaoamua kuchukua hatua, ambacho ni kitu kizuri sana, ila wanapoingia ndani wanakutana hadithi tofauti kabisa. Wanakutana na changamoto kubwa ambazo hawakuambiwa hapo awali.

Ninachotaka kukuambia ni kwamba, hakuna kitu chochote ni rahisi kama kinavyoonekana kwa nje. Hakuna. Mpaka uone mtu ameweza kufanya kitu, jua amepitia changamoto kubwa sana, jua amevuka mengi mpaka kufikia hapo alipofika.

Na kingine ambacho huwa wengi hawajiulizi ni kwamba huyu unayeona kafika pale alianza na wengine wengi, wao wako wapi, wameishia wapi. Utakuta wengi waliweka juhudi lakini wakapotelea njiani.

Siandiki hapa kukukatisha tamaa, ila ninachotaka kukuambia kama rafiki yangu ni kabla hujarukia kufanya jambo lolote, lidadisi kwa undani. Namaanisha jambo lolote lile. Lidadisi kwa undani, jua changamoto zake, angalia wale wanaofanya, wote waliofanikiwa na walioshindwa, kisha fanya maamuzi kama utafanya na ufanye kweli au kama utaachana nacho.

Na hata baada ya kuchunguza sana, bado nataka nikuambie utakutana na changamoto nyingine ambazo hukuzijua, licha ya kufanya uchunguzi wa kina. Hivyo jiandae sana, kama ndiyo kitu ulichochagua kweli kufanya, basi ng’ang’ana mpaka ufike kileleni, bila ya kujali unapitia nini.

SOMA; Unatafuta Njia Rahisi Ya Kupata Fedha? Soma Hapa…

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba hakuna kitu ambacho ni rahisi kama kinavyoonekana kwa nje. Kila kitu kina changamoto zake, na katika wachache walioshinda, kuna wengi ambao wameshindwa. Mimi nitadadisi kwa undani kabla sijakimbilia kuingia kufanya kitu chochote, na nitakapojiridhisha na kuingia kufanya, nitang’ang’ana mpaka nifike kilele cha mafanikio.

NENO LA LEO.

“Nothing in the world is worth having or worth doing unless it means effort, pain, difficulty.” ― Theodore Roosevelt

Kitu chochote ambacho ni cha thamani kuwa nacho au kufanya kwenye dunia hii kinahitaji kuweka juhudi, kinaleta maumivu na ni kigumu kufanya na kufikia.

Hakuna kitu ambacho ni rahisi kufanya kama kinavyoonekana kwa nje, dadisi kwa undani na jitoe kweli kufanya.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.