Kama umeweza kusoma hapa basi nina uhakika umeshawahi kufanya mtihani au unajua mtihani maana yake nini.
Na mitihani ipo ya aina nyingi, kulingana na mfumo wa maswali ulivyo kwenye mtihani husika. Kuna mtihani ambao unapewa majibu mengi na kuchagua jibu moja sahihi (multiple questions) na pia kuna mtihani ambao unapewa swali na unatakiwa kujieleza kwa kuandika insha (essay).
Sasa kama tukichukulia maisha kama mtihani, basi huu ni mtihani wa insha na siyo mtihani wa kuchagua jibu moja sahihi. Hakuna njia moja sahihi ya kuyaendea maisha ambayo ukishaipata tu basi umefanikiwa, bali kila mtu ana njia ambayo ni sahihi kwake. Hivyo juhudi zako mwenyewe na kuyajua vizuri maisha yako ndizo zitakazokuwezesha kufanikiwa. Kama ilivyo kwenye mtihani wa insha kwamba kulielewa swali na kujieleza vizuri ndiyo kunapelekea ufaulu.
Pia kwenye mtihani wa kuchagua jibu moja sahihi unaweza kubahatisha, lakini mtihani wa insha huwezi kubahatisha, ni lazima uwe unajua. Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye maisha, maisha hayabahatishi, bali maisha yanafanyiwa kazi, kwa juhudi na maarifa na ndipo unafanikiwa.
Kwenye mtihani huu wa maisha umepewa swali moja tu; JE UNATAKA NINI KUTOKA KWENYE HAYA MAISHA? Halafu umepewa karatasi nyeupe za kutosha uandike majibu yako. Kwenye uhalisia swali ni maisha yako na karatasi nyeupe ni siku za maisha yako. Na tofauti na mtihani wa kawaida, mtihani wa maisha kila mtu ana jibu lake sahihi na hivyo usijaribu kuiga jibu la mtu mwingine. Jibu mtihani wako, kwa kufanyia kazi kile ambacho unakitaka kutoka kwenye maisha haya.
SOMA; Usidharau Ushindi Mdogo Mdogo Unaoupata Kila Siku, Ni Muhimu Kwa Mafanikio Yako, SEHEMU YA PILI.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba hakuna njia moja sahihi ya kufanikiwa kwenye maisha, bali kila mtu anaweza kuwa na njia yake. Pia hakuna kubahatisha kwenye maisha, lazima ujue ni kipi unataka na kukifanyia kazi. Nimeshajua ni nini ninataka kutoka kwenye maisha yako na nimejitoa kufanyia kazi mpaka nikipate.
NENO LA LEO.
Life is the most difficult exam. Many people fail because they try to copy others. Not realizing that everyone has a different question paper.
Maisha ndiyo mtihani mgumu kuliko yote. Watu wengi wanashindwa mtihani huu kwa sababu wanaiga majibu ya wengine. Bila ya kujua kwamba kila mtu ana maswali tofauti.
Chagua kufaulu mtihani wa maisha kwa kujua kile hasa unachotaka na kukifanyia kazi ili kukipata au kukifikia.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.