Kama umeweza kusoma hapa, nina uhakika kwamba unajua nini maana ya mtandao wa intaneti. Moja ya mapinduzi makubwa sana ambayo tunayapitia katika zama hizi ni uwepo wa mtandao wa intaneti. Mtandao huu umeleta mabadiliko makubwa sana kwenye kila eneo la maisha yetu. Mtandao wa intaneti umerahisisha njia za mawasiliano, umerahisisha upatikanaji wa habari na pia umeboresha upatikanaji wa bidhaa na huduma muhimu kwetu.

Kama umekuwa mtumiaji wa mtandao huu tayari utakuwa unajua ya kwamba unaweza kuwasiliana kwa njia ya intaneti, unaweza kupata habari kupitia intaneti na mengine. Lakini je unajua ya kwamba wewe pia unaweza kutengeneza kipato kupitia mtandao wa intaneti? Unajua ya kwamba unaweza kugeuza mtandao huu wa intaneti kuwa ndiyo biashara yako kuu? Kama ulikuwa hujui hilo basi leo tutakwenda kujifunza kwa pamoja.

Ukuaji wa mtandao wa intaneti umekuwa kwa kasi sana, kwa sasa inakadiriwa tanzania kuna watumiaji wa mtandao wa intaneti wasiopungua milioni 10. Na idadi hii inaendelea kukua kadiri siku zinavyozidi kwenda, hii inatokana na watu wengi zaidi kupata na kutumia simu zenye uwezo wa intaneti.

Wewe kama mtumiaji wa mtandao wa intaneti, unaweza pia kufaidika zaidi kwa kuufanya mtandao huu kuwa sehemu ya biashara yako. na unachokifanya hapa ni kutumia mtandao wa intaneti kuwa kama sehemu yako ya kuweza kuwafikia wateja wako.

Ni vitu gani unaweza kuuza kwa njia ya intaneti?

Karibu kila kitu ambacho unaweza kuuza kwenye biashara ya kawaida, unaweza pia kukiuza kwa njia ya intaneti, kinachobadilika hapa ni jinsi ya kuwafikia wateja wako na uaminifu unaojenga nao.

Hivyo unaweza kuuza bidhaa zako za kawaida, ila hapa utahitaji kuwatumia wateja wako kule waliko. Pia unaweza kuuza maarifa, vitu kama vitabu, majarida na maarifa mengine. Pia unaweza kuuza maarifa ambayo yapo kwenye mfumo wa kielektroniki mfano vitabu vya kielektroniki, sauti zilizorekodiwa au video.

Njia nyingine unayoweza kutumia kufanya biashara kwa kutumia mtandao wa intaneti ni kutoa ushauri kwa lile eneo ambalo umebobea. Na pia unaweza kutoa mafunzo mbalimbali kupitia njia ya mtandao wa intaneti.

Ni vitu gani unahitaji ili kuweza kufanya biashara kupitia mtandao wa intaneti?

Cha kwanza kabisa na ambacho ni muhimu unahitaji maskani yako kwenye mtandao huu wa intaneti. Hapa ni mahali ambapo wateja wako wakienda kwenye mtandao wa intaneti wanakuta taarifa zako na bidhaa au huduma ambazo unazitoa. Na maskani hii unaipata kwa kuwa na tovuti au blog. Tovuti ni sehemu ambayo unatunza taarifa zako au za biashara yako na hivyo mtu anapotaka kuzipata inabidi atembelee tovuti hiyo. Na blog ni tovuti ndogo ambayo ni rahisi kuanzisha na unaweza kuibadili mara kwa mara kwa kuongeza taarifa mpya mara kwa mara.

Baada ya kuwa na maskani yako, unahitaji kuwa na njia ambayo wateja wako watajua wewe upo na unatoa nini. Na hapa unahitaji kuwafikia wateja wako pale walipo. Lakini je wateja wako wa kwenye mtandao wa intaneti wako wapi? Wengi wapo kwenye mitandao ya kijamii kama facebook, whatsapp, instagram na hata twitter. Hivyo ili kuhakikisha wateja wako wanajua upo na watembelee tovuti au blogu yako, unahitaji pia kuwepo kwenye mitandao hiyo. Hivyo unahitaji kuwa na kurasa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ambapo wateja wako wanakuwepo.

Ukishawafikia wateja wako, sasa wape taarifa za biashara unayofanya kupitia mtandao wa intaneti. Waeleze vizuri na watembelee tovuti au blogu yako. na katika tovuti hakikisha umeeleza vizuri huduma au bidhaa unazotoa na pia jinsi ambavyo mtu anaweza kuvipata. Hapa unahitaji kuwa na ushawishi mkubwa na usikate tamaa haraka kwa sababu inawachukua watu muda kuamini kama kweli biashara kwa njia ya mtandao ni halali au utapeli. Hivyo unahitaji kujijengea uaminifu kwamba wewe hufanyi utapeli ila unafanya biashara ambayo ni halali kabisa.

Kuna mengi utakayoendelea kujifunza baada ya kuingia kwenye biashara hii. Lakini jua hii ni biashara ambayo inakuwa kwa kasi na watu wengi wanazidi kuingia kwenye mtandao kila siku. Kama utapenda kutengenezewa tovuti au blog au ungependa kupata ushauri wa kina zaidi wa jinsi ya kufanya biashara kwa njia ya mtandao wasiliana nami kwa mawasiliano yaliyopo hapo chini.

Mtandao wa intaneti ni soko jipya na huria, kama unaweza kulitumia vizuri unaweza kujenga biashara kubwa ambayo siyo tu ya kitaifa bali inaweza kuwa ya kimataifa. Kila la kheri.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz