Kitu kimoja muhimu sana ambacho kila mmoja wetu anacho ni uwezo wa kujua kipi bora kwa maisha yake. Yaani kila mmoja wetu anajua kabisa anahitaji nini kwenye maisha yake ili yawe bora, ili akiri amefanikiwa. Na kila mmoja wetu anayo picha fulani ya mafanikio hayo kwenye akili yake.

Kitu kingine cha kusikitisha ni kwamba wengi hawawezi kufikia picha ile, na ni kwa sababu wamekuwa wanasukuma mbele kuchukua hatua. Wanajua kabisa wanachofanya sasa hakitawafikisha wanakotaka, lakini wanaendelea kufanya. Wanajua kabisa kile ambacho wanatakiwa kufanya ili wafike kule wanakotaka kufika, lakini bado hawaanzi kufanya.

Ni jambo la kuumiza na kusikitisha sana pale unapokuwa na maisha ya aina mbili, maisha ya kwenye fikra zako na maisha yako halisi. Na hapa ndipo matatizo mengi yanapoanzia. Kadiri pengo kati ya maisha ya ndoto yako na maisha yako halisi linavyozidi kuwa kubwa, ndivyo hali yako ya kutoridhishwa na maisha inakuwa kubwa na unaelekea kukata tamaa.

Ndiyo maana leo nakuuliza mpaka lini?

Mpaka lini utaendelea kuishi maisha hayo ambayo wewe mwenyewe unajua siyo maisha yako?

Mpaka lini utaendelea kusukuma mbele maamuzi ya wewe kuanza kuishi maisha yako?

Mpaka lini utaacha pengo la maisha yako halisi na maisha ya ndoto yako liendelee kukua?

Ni wakati sasa wa kukaa chini na kuamua, ya kwamba imetosha, unachotaka ni kuishi maisha yale ya ndoto yako. na haya hayahitaji mambo mengi sana, bali yanahitaji maamuzi yako, na kujitoa kuyasimamia.

Tuna nguvu kubwa sana ndani yetu za kuweza kushinda kitu chochote. Tusiendelee kuzipoteza kwa kuishi maisha ambayo siyo ya kwetu.

SOMA; BIASHARA LEO; Huwezi Kuwa Sahihi Mara Ya Kwanza.

TAMKO LANGU;

Nasema imetosha sasa, siwezi tena kuendelea kuwa na maisha ya aina mbili, maisha ya ndoto yangu na maisha yangu halisi. Sasa nimeamua kuyaishi maisha ya ndoto yangu. Na nimejitoa kweli kuhakikisha nayafikia yale maisha ya ndoto yangu. Najua nina nguvu kubwa sana iliyopo ndani yangu, na siwezi kushindwa na jambo lolote. Nimejitoa na sitokata tamaa kamwe.

NENO LA LEO.

Keep your dreams alive. Understand to achieve anything requires faith and belief in yourself, vision, hard work, determination, and dedication. Remember all things are possible for those who believe. – Gail Devers

Weka ndoto zako hai. Elewa kwamba kufikia kitu chochote unahitaji imani, kujiamini mwenyewe, maono, kufanya kazi, maamuzi na kujitoa. Kumbuka kila kitu kinawezekana kwa anayeamini.

Ishi sasa ndoto yako, usiendelee tena kusubiri.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.