Ukweli ni kwamba kila mmoja wetu anapenda kuwa na maisha ya mafanikio, na maisha yoyote ya mafanikio yanaanza na mtu kuwa na afya bora. Na kitu kingine muhimu sana ni kwamba kila mmoja wetu anapenda kuishi miaka mingi, kila mtu anapenda kuwa na maisha marefu zaidi hapa duniani.

Lakini hivyo sivyo ilivyo kwenye uhalisia, watu wengi hawana afya bora, na watu wengi wanakufa mapema kabla hata ya kufikia uzee. Je ni kitu gani kinasababisha haya, je wale ambao wanaweza kuishi miaka mingi mpaka kuvuka miaka mia moja wana siri gani ambayo wengine hawaijui? Hili ndilo swali alilojiuliza Dr Howard Friedma na mwenzake Dr Leslie Martin. Swali hili liliwafanya waende maabara kufanya utafiti na utafiti waliofanya ndipo walikuja na kitabu THE LONGEVITY PROJECT.

Ndani ya kitabu hiki wametushirikisha mbinu za afya bora na kuweza kuishi miaka mingi. Pia wameeleza jinsi gani tumekuwa tunadanganywa na kujidanganya kuhusu afya bora na kuishi miaka mingi. Kabla hata hatujaenda mbali napenda nikuambie kwamba mambo mengi unayojua kuhusu afya bora siyo sahihi kama unavyofikiri. Kujua hili kwa kina twende pamoja kwenye uchambuzi huu.

Utafiti huu wa afya bora na kuishi miaka mingi ulifanyika kwa kuangalia taarifa za utafiti uliofanyika kwa miaka 80. Kuanzia mwaka 1921 Dr Terman alianzisha utafiti kwa kuwachukua watoto wa shule wenye miaka kumi na ambao walikuwa na akili sana darasani. Alipata watoto zaidi ya 1500 na aliwafuatilia kwa ukaribu tangu hapo mpaka wanapokufa. Kupitia utafiti huu kuna mengi sana ambayo wengi wamejifunza kutoka kwenye kundi hili. Na hapa ndipo tunazipata siri za afya bora na kuishi maisha marefu kwa sababu kati ya hao kuna ambao walifika miaka zaidi ya 90 na kuna ambao walikufa kabla hata ya kufika miaka 60. Maisha yao yamefuatiliwa kwa karibu sana na hapa ndipo tumepata mengi kuhusu maisha.

Karibu tujifunze kwa pamoja kupitia maisha ya watu hawa waliofuatiliwa kwa muda mrefu sana.

1. Ushauri mwingi unaotolewa kuhusu afya bora na kuishi miaka mingi haupo sahihi. Mambo yafuatayo yamekuwa yakisemekana yanawafanya watu kuishi maisha marefu, lakini siyo kweli;

Kwamba wenye roho nzuri wanakufa haraka ila wenye roho mbaya wanaishi muda mrefu (uongo)

Kwamba ukiona au kuolewa unaishi miaka mingi (uongo)

Kwamba ukifikiria mawazo ya furaha unaondoa msongo wa mawazo na utaishi miaka mingi (uongo)

Kwamba watu wa dini wanaishi miaka mingi kuliko wale ambao siyo wa dini (uongo)

Kwamba unahitaji kufanya mazoezi kwa muda fulani kila siku ndio utaishi miaka mingi (uongo)

Kwamba kuwa na wasiwasi ni vibaya kwa afya yako na utakufa haraka (uongo)

Kwamba ukistaafu mapema kazi zako na kupata muda wa kupumzika unaishi miaka mingi (uongo)

Kwamba ukimwanzisha mtoto shule mapema anakuwa na faida zaidi kwenye maisha (uongo)

Kulingana na utafiti huu ambao umeingia ndani kabisa kwenye tabia halisi za watu, kumeonekana kuna vitu vinachangia mtu kuwa na afya bora, lakini siyo kama vinavyoonekana kwa nje. Tutajifunza vyote hapa.

2. Afya bora na kuishi miaka mingi kunaanza na haiba ya mtu. Wale watu ambao ni waangalifu, ambao wanafanya mambo yao kwa mpangilio, ambaoni ving’ang’anizi kwa kile ambacho wanakitaka wanaonekana kuishi miaka mingi kuliko wale ambao wapo wapo tu. Wale ambao wanajua malengo yao na wanayafanyia kazi, wanaishi muda mrefu kuliko wale ambao wanasukumwa tuna kile kinachotokea.

SOMO; Jitengenezee haiba ambayo itakufanya uwe mwangalifu na ujitoe kufanyia kazi malengo yako.

3. Siyo kweli kwamba wale watu ambao wanajichanganya sana na wengine (social) ndio wanaoishi miaka mingi. Kwani watu hawa pia wana hatari ya kujihusisha na mambo ambayo yanaweza kuharibu afya zao. Kama kuwa na marafiki ambao ni walevi au kulazimika kufanya mambo ambayo siyo bora kwao ila kwa sababu wameshaonekana ni watu wa kujumuika sana inabidi wafanye.

SOMO; Kujichanganya siyo kigezo cha kuishi maisha marefu, bali kuwa na maisha bora kiafya ndiyo kunakupa miaka mingi.

4. Watu ambao wana matumaini (optimistic) wanaishi maisha marefu kuliko watu ambao wanakata tamaa. Na sababu zinazowafanya hao kuishi maisha marefu ni kuendelea kupambana hata kama mambo yanaonekana magumu. Hata kama wanaumwa, wanakuwa na matumaini watapona na hivyo kufuata vizuri mpango wa matibabu waliopewa, kama ni dawa kunywa kwa wakati.

SOMO; Kuwa mtu wa matumaini, kamwe usikate tamaa.

5. Kwa kawaida tumekuwa tukiambiwa kwamba ukiwa na furaha unakuwa na afya bora na kuishi miaka mingi, upo mpaka usemi kucheka kunaongeza maisha. Lakini utafiti huu umeonesha kwamba furaha na afya vinakwenda pamoja. Unapokuwa na afya bora unakuwa na furaha, na unapokuwa na furaha unakuwa na afya bora. Na furaha hii inatokana na jinsi ambavyo watu hao wanavyoishi maisha yao, kazi zao, na hata wale watu wanaowazunguka.

SOMO; ili kuishi miaka mingi chagua maisha ambayo yatakuletea furaha, fanya kazi au biashara unayopenda na zungukwa na watu wanaofanya maisha yako kuwa bora.

6. Watu wenye mawazo ya majanga mara zote huwa hawaishi miaka mingi. Watu hawa wanaokuwa na mawazo ya majanga muda wote, mara nyingi hufa kwa ajali au kutokana na vurugu. Kinachowafanya watu hawa kufa mapema ni kujilaumu sana kupita kiasi, na hivyo kukata tamaa. Hali hii inawapelekea kutokuwa makini na maisha yao na hivyo kupelekea kufa mapema.

SOMO; Ondokana na mawazo yoyote hasi au ya majanga kuhusu maisha yako, jua hayo ni mawazo tu na usikubali yatawale akili yako, kwani yatajenga uhalisia.

7. Magonjwa mengi yanayowasumbua watu uzeeni yana chanzo chake utotoni. Pia kumwahisha mtoto shule kabla ya umri wake au kumvusha madarasa inampunguzia umri wa kuishi. Hii inatokana na kukua na watu ambao wamemzidi umri na hivyo anaweza kuonewa na hili kuwaathiri zaidi huko mbeleni.

SOMO; japo huwezi kubadili hali ya utoto uliyopitia, unaweza kumwandaa mtoto wako ili aweze kuishi maisha marefu.

8. Watoto ambao wametokea kwenye familia ambazo wazazi walitalikiana wanakufa mapema ukubwani kuliko wale ambao wanatoka kwenye familia ambazo ziko imara. Kwa wastani wanakufa miaka mitano kabla ya wenzao. Na pia wale ambao wanakulia kwenye familia zisizo na amani wanaonekana kufa mapema zaidi ya hata wale ambao wazazi walitalikiana.

SOMO; japo huwezi kubadili hili kwako, unaweza kuwalinda watoto wako wasije kuingia kwenye hatari ya kufa mapema.

9. Kufanya mazoezi ni muhimu kwa afya, lakini siyo kama ambavyo tunaambiwa. Mazoezi ya kufanya wakati wa ujana lakini uzeeni ukaacha hayakuongezei miaka ya kuishi. Unachohitaji ni kuwa na maisha ambayo ni active, kuchagua kitu cha kufanya ambacho kitaufanya mwili wako uwe active muda mwingi. Hata wale ambao hawakuwa wakifanya shughuli za kuchangamsha mwili wakiwa vijana, kufanya uzeeni kunawaongezea miaka ya kuishi.

SOMO; Ni muhimu sana kuchagua kitu ambacho kinaushughulisha mwili wako na uweze kufanya kitu hiko kwa miaka yako yote hata utakapokuwa mzee. Hiki ndiyo kitakachokuongezea miaka mingi ya kuishi.

10. Kumekuwa na ushauri kwamba waliooa au kuolewa wanaishi miaka mingi kuliko wale ambao wanabaki kuwa waseja. Lakini hili ukiliangalia kwa ndani liko tofauti kidogo. Wanaume wanaooa na kuachana na wake zao, wanakufa mapema kuliko hata wale ambao hawakuoa kabisa. Na kwa wanawake wanaoolewa wa kuachika wanakufa mapema. Wanawake wasioolewa kabisa hawana tofauti kubwa ya umri wa kuishi ukilinganisha na wale ambao wameolewa na wanaishi vizuri na waume zao. Kwa vyovyote vile kuvunjika kwa ndoa kunawapunguzia wanaume miaka ya kuishi kuliko kwa wanawake.

SOMO; kuona au kuolewa na kudumu kwenye ndoa kunakuongezea miaka ya kuishi. Ila changamoto za ndoa na kuachana kunapunguza miaka ya kuishi hasa kwa wanaume.

11. Watu wenye mafanikio wanaishi miaka mingi kuliko wale walioshindwa. Na refu huu wa maisha hautokani tu na kuwa na fedha, bali yale maisha ambayo wanakuwa wamechagua kuishi. Pia changamoto na msongo wa mawazo ambao watu wanakutana nao wakati wanafanyia kazi malengo yao hauwapunguzii miaka ya kuishi, badala yake unawaongezea miaka zaidi.

SOMO; Kwa vyovyote vile hakikisha unafanikiwa, unafanikiwa kwa kuchagua ni nini unachotaka na kuchagua kukifanya hasa, usifike wakati na kusema umestaafu, bali endelea kufanya kwa maisha yako yote.

12. Siyo kweli kwamba kufanya kazi muda mrefu kunapunguza miaka ya kuishi. Pia katika mafanikio, utafiti ulionesha siyo wale wanaofanya kinachotokana na vipaji vyao ndio wanaoishi muda mrefu, bali wale ambao wameweza kubobea kwenye chochote wanachofanya, na wanazalisha majibu mazuri, wanakuwa wameridhishwa sana na maisha yao na hii inawaongezea miaka ya kuishi.

SOMO; Kijue vizuri kile unachofanya, kuwa na uzalishaji mzuri na ridhika na kile unachopata huku ukiendelea kuweka juhudi zaidi. Utaishi miaka mingi.

13. Imekuwa ikionekana kwamba watu ambao ni wafuasi wa dini wanaishi miaka mingi kuliko wale ambao siyo wafuasi wa dini. Utafiti huu umekwenda ndani zaidi na kugundua kwamba wale ambao ni wafuasi wa dini ni kweli wanaishi muda mrefu siyo kwa sababu ya dini zao bali kwa tabia ambazo zinatokana na dini zao. Kwa mfano watu wa dini wanajiepusha na tabia mbaya kiafya. Wafuasi wazuri wa dini huwezi kuwakuta ni walevi wa kupindukia, au wanatumia madawa ya kulevya au hata uzinifu. Haya yote yanawalinda na kuwa na afya mbovu. Pia kwenye dini watu anajumuikia pamoja na hivyo kuwa karibu na watu kitu ambacho kinawaongezea muda wa kuishi.

SOMO; Iwe ni mtu wa dini au la, hakikisha unajijengea tabia ambazo zitaimarisha afya yako kwa chochote unachofanya. Pia hakikisha unakuwa kwenye jumuia ya watu ambao wote mna mawazo sawa na hivyo kuwa sehemu ya kitu fulani.

14. Maisha ya kijamii yana mchango mkubwa sana kwenye kuishi miaka mingi. Wale ambao wamejitenga na jamii na wako kivyao vyao wana hatari ya kufa kwa umri mdogo. Ila wale ambao wanakwenda vizuri na jamii yao, iwe ni familia, marafiki, wanaweza kuishi miaka mingi. Na hapa haijalishi ukubwa wa wale ambao uko karibu nao, bali kinachojali ni ule ukaribu wa mahusiano yenu. Watu ambao wanajitoa kwa wengine na ambao wana uhakika kuna watu ambao wapo tayari kujitoa kwa ajili yao pia wanaishi miaka mingi.

SOMO; Tengeneza mahusiano bora na jamii inayokuzunguka. Kuwa na mahusiano bora na familia yako na pia marafiki zako. Pata muda wa kukaa na wale watu ambao ni wa muhimu kwako. Itakuongezea miaka ya kuishi.

15. Wasiwasi umekuwa unaonekana ni chanzo cha watu kufa mapema. Lakini utafiti huu umeonesha wale wenye wasiwasi, hasa wanaume wanaishi miaka mingi kuliko wale ambao hawana wasiwasi. Wale wenye wasi wasi hasa kwenye mambo muhimu kwao wanakuwa waangalifu na kuhakikisha wanajua zaidi. Mfano kwenye maswala ya afya, wenye wasiwasi watapata matibabu bora na kuwa na afya bora.

SOMO; usiogope kuwa na wasi wasi, ila pia usikubali wasiwasi ukuzidi mpaka ushindwe kuchukua hatua muhimu kwa maisha yako.

16. Imezoeleka kwamba wanawake wanaishi miaka mingi kuliko wanaume. Kwenye kila jamii wanawake wanaishi kwa wastani miaka mitano zaidi ya wanaume. Utafiti huu ulichimba ndani zaidi na kugundua vitu tofauti pia. Kwa mfano waliangalia katika tabia, kuna tabia ambazo mara nyingi zipo kwa wanawake (feminine) na kuna tabia ambazo mara nyingi zipo kwa wanaume (masculine). Sasa kuna wanawake ambao wana tabia ambazo mara nyingi zipo kwa wanaume, na kuna wanaume ambao wana tabia ambazo mara nyingi zipo kwa wanawake. Katika utafiti huu waligundua kwamba wanawake na wanaume ambao wana tabia zinazopatikana mara nyingi kwa wanawake, wanaishi miaka mingi kuliko wanaume na wanawake ambao wana tabia nyingi za kiume.

SOMO; Baadhi ya tabia ambazo zinaonekana ni sawa kwa wanaume kufanya na siyo kwa wanawake zinawaweka wanaume kwenye hatari ya kufa mapema. Kama ulevi, uvutaji wa sigara na mengine. Jiepushe na tabia hizo.

17. Msongo wa mawazo umekuwa unaonekana ni chanzo cha watu wengi kufa. Lakini huu siyo ukweli, kwa sababu msongo wa mawazo ni hali ya kawaida kwa kila mtu. Ila pale msongo wa mawazo unapopitiliza na mwili kushindwa kujirejesha kwenye hali yake ya kawaida ndipo hatari ya kiafya inapoanza na mtu kufa mapema. Pia njia ambazo watu wanatumia kuondokana na msongo wa mawazo zinazidi kupunguza maisha yao, njia kama ulevi, kula sana, kuepuka kula na mengine ndiyo yanapelekea hatari ya kufa kuwa kubwa.

SOMO; Jua jinsi ya kukabiliana na msongo wa mawazo unapotokea, huwezi kuepuka ila unaweza kutatua pale mambo yanapokwenda tofauti na ulivyokuwa umetegemea. Usikubali msongo wa mawazo ukufanye upoteze dira ya maisha yako.

18. Kuna mambo matano yanayopelekea kuwa na afya mbovu na mtu kufa haraka;

Moja ni sumu, sumu zozote kwenye mwili wako zitakufanya ufe mapema. Na hapa sumu ni kama vilevi, uvutaji, mihadarati, na sumu nyinginezo kama kuzidisha dawa (overdose)

Mbili ni mionzi. Mionzi inakatisha sana maisha ya wengi, na hii inatokana na viwanda, silaha za kivita na pia kufanyiwa sana vipimo kama x-ray na ct scan.

Tatu ni maambukizi. Magonjwa yanayoambukizwa kama yale yanayosababishwa na virusi, bakteria na hata fangasi yamekuwa yanapunguza maisha ya wengi.

Nne ni ajali. Ajali za vyombo vya usafiri au vifaa vya kazi zinapunguza miaka ya kuishi.

Tano ni magonjwa ya kurithi. Hapa mtu unakuwa umezaliwa na hali ambayo inakuweka kwenye hatari ya kuumwa au kufa mapema kuliko wengine.

SOMO; Kwa hayo manne ya kwanza jiepushe nayo, kwa hilo la tano fanya vipimo mapema na fuata ushauri wa kitaalamu ili kuishi muda mrefu.

19. Mwili wa binadamu mara zote upo kwenye hali ya kubadilika. Na kitu chochote unachofanya ni lazima ufanye kwa kiasi. Kukosa maji kutakupelekea kufa, ila pia kunywa maji mengi sana kutakupelekea kufa. Kuwa na msongo wa mawazo uliopitiliza ni hatari, lakini pia kukosa msongo kabisa maisha yanachosha. Hivyo kwenye maisha yako, kazana kufanya kwa kiasi.

SOMO; Chochote unachofanya kwenye maisha, fanya kwa kiasi, hii ndiyo siri ya kuishi maisha marefu.

20. Mwisho kabisa tumalize kwa kusema kwamba hakuna kitu kimoja ambacho kinaweza kuwa sawa kwa watu wote. Kuishi maisha marefu siyo kitu kinachotokana na tabia moja, au tabia chache kama watu wanavyoambiwa, badala yake ni mfumo tata, kuna mambo mengi sana yanayohusika na hivyo unahitaji kujijua wewe mwenyewe vizuri ndio uweze kuishi maisha marefu. Kuna kitu ambacho akifanya mwingine atakuwa na maisha marefu ila ukifanya wewe itakuwa majanga. Hivyo jijue vizuri, jua ni kipi unapendelea kufanya na hakikisha wakati wowote unachagua kuishi maisha yanayotokana na tabia bora za kiafya.

Tafakari vizuri haya uliyojifunza, kisha yatafakari maisha yako na angalia ni maeneo gani unayohitaji kurekebisha ili uweze kuboresha maisha yako na kuweza kuishi maisha yenye afya bora na miaka mingi. Kumbuka haya yote yanaanza na wewe mwenyewe kuchukua hatua.

Chukua hatua sasa.

Rafiki na kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz