Tunataka mambo mazuri lakini hatupeni kusubiri, na wala hatuna uvumilivu.

Lakini kama ambavyo wote tunajua, mambo mazuri siyo rahisi na hayapatikani kirahisi.

Unakuwa bora kwa kurudia tena na tena na tena kile ambacho unataka kuwa bora.

Hata kama umekutana na changamoto kiasi gani, hata kama umekwama kiasi gani, unahitaji kurudia tena.

Kadiri unavyorudia ndivyo unavyojifunza zaidi.

Kadiri unavyorudia ndivyo unavyoondoa hofu ya kushindwa.

Na kadiri unavyorudia ndivyo unavyojipa ujasiri wa kuchukua hatua mbazo ni hatari.

Rudia rudia na rudia tena.

Kama kuna kitabu umesoma na kujifunza vitu vizuri rudia tena kukisoma, utajifunza vizuri zaidi.

Kama umeanza biashara na ikawa na matokeo mazuri, rudia kile kizuri ambacho umefanya. Na kama umeanza na matokeo yakawa mabaya rudia lakini boresha kile ambacho hukufanya vizuri.

Maisha ni mchezo wa kurudia, na kila tunachofanya tunarudia, unalala, unaamka, unakula, unafanya shughuli zako, na unalala tena.

Tumia hili kwenye kazi zako na maisha yako kwa ujumla. Fanya kitu ukijua utarudia tena na tena na tena. Na kuwa tayari kurudia. Usione kama ni mzigo, bali ona ni sehemu ya kile unachofanya.

SOMA; Somo Litaendelea Kujirudia Mpaka Uelewe…

TAMKO LANGU;

Najua hakuna ubora kama sitorudia kile ninachofanya. Nimejitoa kurudia tena na tena na tena mpaka pale nitakapopata ninachotaka. Na hata nikishapata, bado nitarudia tena. Kwa sababu kadiri ninavyorudia ndivyo ninavyozidi kuwa bora na ndivyo ninavyoondokana na hofu.

NENO LA LEO.

“By constant practices, deliberate repetitions and uninterrupted exercises, leaders go from zero to hero. They don’t quit.” ― Israelmore Ayivor

Kwa kufanya mara kwa mara, na kurudia tena na tena, viongozi wanatoka sifuri mpaka kwenye ushujaa. Hawakati tamaa.

Hakuna kitu kitakuja kwenye maisha yako kwa kufanya mara moja. Vitu vyote vizuri vinakuja kwa kurudia kufanya tena na tena na tena. Jitoe sasa kurudia kufanya tena.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.