Huo ndiyo mzunguko wa maisha, ambao huwezi kuvuka hatua hata moja, ni lazima uanze hatua ya kwanza ndipo uende ya pili mpaka ya mwisho.
KUWA.
Ni lazima uwe mtu ambaye anaendana na kile ambacho unakitaka. Kama unataka kuwa na mafanikio, lazima uwe mtu ambaye anayaendea mafanikio. Lazima ujijengee tabia zinazoendana na kile unachotaka. Ni lazima uwe mwaminifu, muadilifu na mchapa kazi. Unahitaji kuwa na nidhamu na kuwa na mtizamo sahihi. Hii ni hatua ya kwanza na muhimu sana.
FANYA.
Hii ni hatua ya pili muhimu, ni lazima ufanye kile ambacho kitakufikisha kwenye kile unachotaka. Hakuna njia nyingine ya tofauti ni lazima ufanye, ni lazima ujitoe na uwe mvumilivu. Na urudie tena na tena na tena. Ni lazima uweke juhudi kwa chochote kile unachotaka, maana hakuna kinachokuja bila ya juhudi.
PATA.
Ni sheria ya dunia kwamba unavuna kile ambacho umepata. Hivyo kama umeshakuwa, na umeshafanya, kinachotokea ni wewe kupata. Na utapata kadiri ya ulivyofanya. Na hata kama utakosa, utakuwa umepata somo ambalo baadaye litakuwezesha kupata zaidi. Ukifanya utapata.
TOA.
Hii ni hatua ya mwisho kabisa kwenye mzunguko huu wa maisha. Ni lazima utoe kwa wengine, kile ambacho wewe umepata. Uwawezeshe na wao kupata zaidi. Na muhimu zaidi huwezi kutoa kabla hujapata. Hivyo pata kisha toa kuwawezesha wengine nao waweze kupita vizuri kwenye mzunguko huu.
Na huo ndiyo mzunguko wa maisha, mzunguko huu ndio unatufanya tuwe na maisha yenye maana hapa duniani. Usijaribu kuvuka hatua yoyote ile.
TAMKO LANGU;
Nimeamua kuwa mtu mwema, mwaminifu, mwadilifu na mwenye nidhamu. Nimejitoa kufanya kwa moyo wangu wote na kuweka juhudi kubwa kwenye kile ninachofanya. Nina uhakika wa kupata matokeo bora sana kupitia kile ninachofanya na nitawashirikisha wengine ili nao waweze kuwa na maisha bora. Najua maisha bora ni maamuzi yangu, nimeshaamua kuwa na maisha bora. NITAKUWA, NITAFANYA, NITAPATA, NITATOA.
NENO LA LEO.
Ni lazima uwe mtu ambaye unayavutia mafanikio kwako, hivyo uwe na tabia za mafanikio.
Ni lazima ufanye yale ambayo yatakuletea mafanikio. Ni muhimu ujitoe kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.
Kwa kuwa na kufanya ni lazima utapata matokeo bora sana, unavuna kile ulichopanda, ni sheria ya dunia.
Ni lazima utoe kile ulichopata, ili kuwawezesha wengine nao kuwa na maisha bora.
KUWA. FANYA. PATA. TOA ndiyo mnyororo wa thamani.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.