Habari mpenzi msomaji wa Amka Mtanzania? Karibu katika makala yetu ya leo ambapo tutazungumzia adui namba moja katika malezi ya watoto. Karibu tujifunze kwa pamoja ndugu msomaji. Licha ya changamoto ya kiuchumi kusumbua watu wengi lakini siku hizi malezi kwa watoto imekuwa changamoto miongoni mwa wazazi wengi. Wazazi wengi wamehamia katika ulimwengu wa ‘ubize’ na kusahau wajibu wao katika malezi ya watoto na hatimaye watoto wanakosa malezi mazuri katika familia watoto wanageuka kuwa yatima kama vile hawana wazazi, watoto wanakosa upendo kutoka kwa wazazi wao. Inafikia kipindi watoto wanawaogopa wazazi wao wanaishi maisha kama ya paka na panya maisha ambayo hayana furaha, amani na upendo. 

 
Wewe kama mzazi unapata faraja gani kuwa na mafanikio halafu familia yako ni mbovu? Familia haina amani, furaha na upendo? Wazazi wengine ni wabishi hawataki kukubali kosa kuwa wamekosea ili wabadilike na kuboresha familia zao. ‘Ubize’ wako hauna maana kama umesahau jukumu la malezi ya watoto wenu, wazazi wakishazaa tu wanaachia wasichana wa kazi ndio walee watoto au wengine wanawapeleka watoto kwa bibi zao ili walelewe wao hii sio haki kabisa, jukumu la malezi siyo la bibi na babu au dada wa kazi. Mafanikio yako, ubize wako hauna maana kama familia yako ni mbovu na watoto wako wameharibika kutokana na kukosa malezi bora.
SOMA; Mambo Matano(5) Muhimu Ya Kuzingatia Kwenye Malezi Ya Watoto Ili Kuwaandaa Kufikia Mafanikio.
Kwa hiyo, ni dhahiri kabisa adui namba moja katika malezi ya watoto ni mzazi au wazazi. Watoto wanahitaji kupata malezi kutoka kwa baba na mama, mtoto aonje upendo wa wazazi aone thamani ya kuwa na wazazi, acha kusingizia ubize na kutafuta sababu juu ya malezi ya watoto, acha kulea watoto kama vile bata anavyolea watoto wake. Bata anatangulia mbele yeye anawaacha watoto nyuma wala hana habari nao na wazazi wengine kweli wanawalea watoto kama vile bata anavyowalea watoto wao. Mpe malezi mazuri mtoto wako kama vile ndio siku yako ya mwisho hapa duniani, kama hujawahi kumwambia mtoto wako nakupenda mwanangu basi mwambie leo, kama hujawahi kumkumbatia mwanao mkubatie leo, kama hujawahi kumbusu mtoto wako basi mbusu leo afurahie uwepo wa mzazi wake hapa duniani. Changamoto za kidunia zipo lakini zisikufanye ushindwe kumlea mtoto katika malezi mazuri.
Wazazi wakikosa misingi imara na familia inayumba, huwezi kumpata mtu sahihi kama wewe siyo mtu sahihi ukitaka kumpata mtu sahihi basi kuwa sahihi kwanza wewe mwenyewe, ukitaka familia yako iwe bora, iwe sahihi kama wewe ni mzazi basi kuwa bora kwanza wewe na familia itakua bora. Huwezi kuiambia familia iwe bora yaani watoto wakati wewe mzazi siyo bora. Kuwa mfano kwa familia yako nayo itakua bora. Inasikitisha sana pale mzazi anapotengeneza hali ya ubinafsi mfano kuna wazazi wengine wanaangalia Tv chumbani hii ni kukwepa kukaa na watoto na kutengeneza chuki, wazazi mkipata nafasi ya kuangalia tv na watoto kaeni pamoja mzungumze pamoja, mcheke na mfurahi ndio raha ya familia, hata mkipata nafasi ya kula pamoja kuleni pamoja watoto muwaoneshe upendo wa kukaa mezani na kula pamoja siyo ukionana mtoto ni salamu tu na huna muda tena mtoto.
Shida ya malezi inaanza kwa wazazi wenyewe kama wazazi wamekosa kuwa na upendo wao wenyewe wanatengeneza mazingira ya hofu, chuki na visasi katika familia na hatimaye kuwagawa watoto. Watoto wote ni sawa tuwapokee kama tulivyopewa acheni tabia ya kusema mtoto huyu ni wangu na mtoto huyo ni wako wape haki sawa ya malezi watoto wote bila ubaguzi. Kuwapa watoto adhabu kupita kiasi na mtoto kutopewa adhabu akifanya kosa nayo ni hatari katika malezi, kuwapa watoto adhabu mbadala kama vile kumzomea mtoto, kumtukana unamwathiri mtoto kisaikolojia. Watoto wengine wanalelewa malezi ya ajabu katika familia na kufanywa wao ndio watawala wa familia anafanya chochote anachojisikia na mzazi hana kauli juu ya mtoto.
SOMA; Huyu Ndiye Mwalimu Wa Kwanza Na Muhimu Sana Kwenye Malezi Ya Mtoto.
Dawa nzuri ni kubadilika tu kwa wazazi bila kuweka sababu na kujitambua kuwa jukumu la malezi ni la kwako na mtoto akiharibika mzigo unakua ni kwa wazazi hata ukiwa mtafutaji mzuri familia yako ikiwa ni mbovu mali zako zina faida gani? Kulingana na ubize huu unawafanya wazazi hata kuwapeleka watoto wadogo kabisa shule za bweni kwa sababu ya majukumu na kukwepa wajibu wao, ni hatari kwa mtoto kwani unamnyima haki ya malezi yake ambayo hawezi kuipata sehemu nyingine yoyote zaidi ya wewe mzazi. Pia kuwaanzisha watoto shule wakiwa na umri mdogo chini ya miaka 5 wanakadiriwa kuishi maisha mafupi ukilinganisha na watoto wanaoanza shule wakiwa na miaka 6 hii ni kulingana na tafiti zilizofanyika kwa miaka 80 kuanzia mwaka 1921 na ulianzishwa na Dr Terman utafiti huu upo katika kitabu cha The Longevity Project. Pia dini ina mchango mkubwa katika malezi ya watoto hivyo ni wajibu kuwafundisha watoto dini ili wawe na hofu ya Mungu katika maisha yao.
Kwa kuhitimisha makala hii, wazazi ndio kioo katika malezi ya mtoto na ili tuwe na jamii bora lazima tuwe na familia bora na msingi wa familia bora unajengwa na wazazi wawili. Baba na mama wakiyumba na familia nzima inayumba hivyo basi, wazazi wana mchango mkubwa sana katika malezi ya watoto.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com