Hayupo mtu ambaye amepita njia uliyopita kwenye maisha mpaka kufika hapo ulipo sasa.

Hayupo mtu ambaye amepitia kila changamoto ambayo umeshapitia mpaka kufika hapo ulipo sasa.

Hayupo mtu ambaye ameshakutana na watu ambao umeshakutana nao mpaka sasa.

Hayupo mtu ambaye ameshajitoa kukosa baadhi ya mambo mazuri kama ulivyojitoa wewe mpaka kufikia sasa.

Hayupo mtu ambaye anajua ni kipi hasa unachotaka kwenye maisha yako, ni kipi unakipa thamani kama ambavyo wewe unajua.

Ni wewe pekee ambaye una uzoefu na maisha yako na unajua ni wapi unataka kufika. Wengine wanaona kwa nje tu, lakini wewe ndiye uliye ndani.

Sasa swali linakuja, kwa nini hutaki kufanya maamuzi yako mwenyewe mpaka uangalie wengine?

Kwa nini unataka kufanya kile ambacho wengine wanafanya, japo unajua siyo unachotaka?

Kwa nini unajiuliza sana wengine watakuchukuliaje na wakati hiko ndiyo muhimu zaidi kwako.

Nikupe siri moja; chochote utakachofanya, wachukue watu wawili na watakuwa na maelezo tofauti kuhusu ulichofanya. Hivyo bado hawataona kile ulichofanya, bali wataona kile wanachotaka kuona.

Hivyo chagua kuishi maisha ya mafanikio, na acha kutaka kufanya kile ambacho kila mtu anataka kufanya na acha kuhofia wengine wanakuchukuliaje.

SOMA; Hakuna Anayejali Maisha Yako Zaidi Yako Mwenyewe.

TAMKO LANGU;

Najua ya kwamba hakuna mtu mwingine mwenye uzoefu wa maisha yangu zaidi yangu mimi mwenyewe. Na hivyo nitatumia uzoefu huu na kile ninachotaka kwenye maisha kuhakikisha nafikia mafanikio makubwa. sitakazana kufanya kile ambacho kila mtu anafanya, na sitajali wengine wananichukuliaje.

NENO LA LEO.

Wewe pekee ndiye mwenye uzoefu mkubwa na maisha yako. Ni wewe pekee ndiye unayejua ni kipi unachotaka kwenye maisha yako. Acha kukazana kufanya kile ambacho kila mtu anafanya, na acha kuhofia wengine wanakuchukuliaje, kazana kufanya kile ambacho kitakufikisha kwenye maisha ya ndoto yako.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.