Kadiri teknolojia inavyozidi kukua, ndivyo tunavyozidi kusahau kwamba tunahitaji kuweka mipaka.

Teknolojia hizi mpya zimekuwa sehemu ya maisha yetu kiasi kwamba tumeshajijengea hali kwamba hatuwezi kukaa mbali nazo.

Hebu jiulize ni kwa dakika ngapi unaweza kukaa bila ya kugusa simu yako, hasa kama unatumia simu hizi za kisasa? Jiulize je unaweza kukaa siku nzima bila ya kuingia kwenye mtandao au bila ya kutumia kifaa cha kielektroniki?

Najua utaona ni vigumu kwa sababu tumeshajiondolea mipaka, hakuna tena mpaka kati yetu na teknolojia. Ndiyo maana hata muda wa kulala bado wengi wanakaa karibu na vifaa vyao hivi.

Na hata tunapotembelea mitandao hii, hakuna mwisho, kila unapoangalia unazidi kutaka kuangalia, ulipanga uchungulie kwa dakika tano, nusu saa imepita bado upo.

Na kama umebanwa na ukakosa muda wa kuingia kwenye mitandao hii japo kwa masaa machache tu, akili yako haitulii, unaona kama kuna kitu kikubwa sana umekikosa, au umepitwa.

Hakuna kitu ambacho hakipaswi kuwa na mipaka, kuwa na  kiasi kwenye maisha. Na tunapokuja kwenye matumizi ya simu na mitandao ya kijamii, tunahitaji mipaka imara zaidi. Kwa sababu vitu hivi vinatupunguzia ufanisi wetu.

Sasa weka mipaka yako, usikubali siku yako itawaliwe na kila kinachoendelea, badala yake ipange siku yako mwenyewe, na chagua ni muda gani wa siku ambao utaingia kwenye mitandao hii, na uwe muda mfupi sana usizidi saa moja kwa siku moja. Pitia yale ya muhimu tu, mengine achana nayo.

Jiwekee mipaka, chagua muda ambao umeshamaliza yale muhimu ndipo uingie kwenye mitandao. Na pia mara kwa mara tenga siku ambayo hutoingia kabisa kwenye mitandao hii, siku ambayo hutatumia kabisa kifaa chochote cha kielektroniki, na tumia siku kama hizo kuyatafakari maisha, na kupitia na kupanga malengo yako.

SOMA; Fanya Usafi Huu Wa Mitandao Ya Kijamii.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba nimepoteza mipaka kwenye matumizi ya simu na mitandao ya kijamii. Nimekuwa natumia vitu hivi kupita kiasi na hivyo kupunguza ufanisi wangu kwenye mambo muhimu kwangu. Kuanzia sasa naweka upya mipaka na simu na mitandao ya kijamii ili isiwe kikwazo kwangu kufikia mafanikio makubwa.

NENO LA LEO.

Kila kitu unachofanya kwenye maisha yako kinapaswa kuwa na mipaka. Na hii pia ni kwenye matumizi yako ya simu na mitandao ya kijamii. Usikubali kutawaliwa na mitandao hii, chagua muda mfupi wa kutembelea mitandao hii, usipoteze muda wako siku nzima kuzurura kwenye mitandao ya kijamii. Kwa kujiwekea mipaka hakuna kikubwa utakachokosa, na badala yake utaongeza ufanisi wako kwenye kazi zako.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.