Kuna changamoto nyingi tunakutana nazo katika mahusiano yetu na wengine. Yawe ni mahusiano ya kikazi, kibiashara, kifamilia au mengineyo, kuna wakati tunajikuta kwenye hali ya kutokuelewana.
Tunapokuwa kwenye hali hizi za kutokuelewana, hasa pale ambapo kuna kitu tunashindania, inahitaji ukomavu mkubwa sana ili kuweza kufikia muafaka bora kwenu wote. Na katika hali hii mnaweza kuafikiana kwamba kila mmoja apate kiasi, au mmoja apate na mwingine akose, au kila mmoja akose.
Hapa leo tutajadili muafaka wa kila mmoja akose, hasa kwa yule anayesema ni bora tukose wote. Kwanza kutaka muafaka kama huu ni kuonesha uwezo mdogo sana wa kufikiri ambao mtu anao. Na siyo tu uwezo mdogo, bali pia inaonesha ni jinsi gani mtu hajiamini.
Mtu anayefikiria kwamba ni bora tukose wote ni mtu ambaye hajiamini, anategemea wengine kwa kila kitu. Mara nyingi mtu huyu anakuwa na maisha mabovu na hivyo kuona kama hakuna atakayepata basi wote watakuwa na maisha magumu kama ya kwake.
Kama umewahi kupata mawazo kama haya katika hali yoyote ile, unahitaji kujifanyia tathmini na kujiondoa kwenye uchanga huo wa kifikra. Na kama ukikutana na mtu wa aina hiyo, ambaye anafikiri ni bora mkose wote, jiepushe naye. Kwa sababu tatizo lake siyo kupata au kukosa pekee, bali tatizo lake lipo ndani kabisa, ni swala la kujiamini na mtazamo wa maisha.
Kwa watu ambao hawajiamini, mara zote huona wengine wanafaidi kuliko wao na hivyo kuona ni bora kila mtu akose. Na kwa wale ambao wana mtizamo hasi kuhusu maisha, hawaamini kama jambo lolote jema linaweza kutokea na hivyo kuona bora kila mtu akose.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba fikra za bora tukose wote hazianzii kwenye kupata na kukosa, bali zinaanzia kwenye hali ya mtu mwenyewe, na zinaanzia kwenye kujiamini na mtizamo wa maisha. Kwa wasiojiamini pia hawaamini wengine na kuona bora kila mtu akose. Mimi najiamini na pia nina mtazamo chanya na maisha yangu, sitajiingiza kwenye hali yoyote ambayo kila mtu anakosa.
NENO LA LEO.
Bora tukose wote ni fikra za watu ambao hawajiamini na wana mtizamo hasi juu ya maisha. Wasiojiamini wanaona mara zote kama wengine wanafaidi kuliko wao, na hivyo kuona njia bora ni kumharibia kila mtu. Achana na mawazo haya potofu na waepuke wenye mawazo kama haya.
Kila mtu anaweza kupata na kuwa na maisha bora. Jiamini na mara zote angalia upande chanya, utaziona fursa nyingi zaidi.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.