Adui namba moja wa ubora ni uzuri.

Tunapofanya kitu kizuri, tunaridhika na kuona hapo tayari tumeshamaliza kila kitu. Tunaona kama tayari tumefikia kilele cha mafanikio na hivyo kuacha kuweka tena juhudi. Na hapo ndipo tunapoacha kabisa kuendea ubora.

Uzuri ni adui mkubwa sana wa ubora kwa sababu kwa asili binadamu huwa tunaridhika haraka. Pale ambapo tunaona tumefanya kitu kizuri tunaona hakuna haja ya kuenda mbali zaidi. Ni mpaka pale inapotokea changamoto ambayo inafanya uzuri usiwe tena uzuri na ndipo tunagundua ya kwamba tulijisahau.

Mifano ipo mingi kwenye maisha yetu ya kila siku;

Mtu anapata kazi nzuri inayompa kipato kizuri na anaona hiki ndiyo kilele cha mafanikio. Hakazani tena kujiongeza kwa ujuzi wake na wala kuongeza kipato kwa njia nyingine. Ni mpaka pale kazi hiyo inapoisha ndiyo anakuja kugundua ya kwamba alichelewa kuchukua hatua.

Mwingine anaanzisha biashara na inamlipa vizuri, inakua kwa kiasi na anajisahau, anaona yale ndiyo maisha aliyokuwa anatafuta na hivyo kuacha kuweka juhudi kama za mwanzo. Ni pale biashara hiyo inapopata changamoto ndipo anapokuja kuona ya kwamba kama angejua mapema angewekeza kwenye biashara nyingine zaidi.

Lengo la kukuandikia kwenye ukurasa wa leo rafiki ni kukukumbusha ya kwamba unapokubali uzuri, maana yake umeagana na ubora. Napenda nikukumbushe kwamba ubora huwa haudumu hata siku moja, kitu ambacho unaona ni bora leo, kesho kitaishia kuwa kuzuri. Hivyo ni jukumu letu kila siku kuweka juhudi kuboresha zaidi, hakuna ubora udumuo bila ya juhudi.

Tusijisahau na kuona ndiyo tumeshaweza kila kitu, kuna kazi kubwa sana ipo mbele yetu, tuendelee kuweka juhudi kubwa.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba adui namba moja wa ubora ni uzuri. Kama nitafanya kitu kizuri na nikaridhika nacho na hivyo kuacha kuweka juhudi kubwa, ninakuwa nimeagana kabisa na ubora. Mimi nimeamua ya kwamba sitaridhika na uzuri, bali kila siku nitaweka juhudi ili kupata ubora zaidi. Najua hata nikifikia ubora hautodumu muda mrefu kama sitaendelea kuweka juhudi.

NENO LA LEO.

Adui namba moja wa ubora ni uzuri. Binadamu huwa tunaridhika haraka pale tunapofanya kitu kizuri na hivyo kuacha kuweka juhudi. Kwa kufanya hivi tunakosa kuwa bora zaidi. Ubora unatokana na kuendelea kuweka juhudi kwenye kile ambacho mtu umechagua kufanya.

Endelea kuweka juhudi bila ya kuchoka, hiyo ndiyo njia ya kufikia ubora.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.