Utata Wa Mafanikio; Tabia Nane Unazohitaji Kuwa Nazo Kwa Pamoja Ili Kufikia Mafanikio Makubwa.

Kwa nini baadhi ya watu wanafikia mafanikio makubwa kwenye maisha huku wengine wakiishia kuwa watu wa kawaida tu? Je ni kipi kinawatofautisha watu hawa? Elimu? Rangi? Kabila? Familia wanazotokea?
Wengi wamekuwa wakifikiria sababu hizo kama ndiyo zinawafanya watu fulani kufanikiwa na wengine kushindwa. Lakini wengi wa waliofanikiwa wanaonekana kuenda kinyume na sababu hizo. Yaani kuna watu ambao wana mafanikio makubwa ila hawana elimu kubwa, na wakati huo kuna watu wana elimu kubwa ila hawana mafanikio. Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye rangi, familia wanazotokea na kadhalika.
Kwa sababu hizo za hali ya mtu kushindwa, basi watu wakahamishia mawazo yao kwenye sababu nyingine, wakasema huenda ni kujitoa kufanya kazi kwa bidii, au kuwa na bahati, au kuwa na mawazo mazuri. Lakini pia kwenye sababu hizi pia zinakataa, kuna ambao wanafanya kazi sana, lakini hawana mafanikio. Na kuna ambao wanaanza na mawazo bora sana lakini hawafiki mbali.
Hapa ndipo mwandishi Richard St. John alipochukua jukumu la kuwahoji watu wote ambao wamefikia mafanikio makubwa. na kugundua kwamba mafanikio hayatokani na kitu kimoja, bali vitu vingi ambavyo vinapokuja pamoja vinamfanya mtu kufikia mafanikio makubwa. na hapa ndipo alipokuja na tabia nane ambazo watu wote wenye mafanikio makubwa wanazo.
Kupitia makala hii tunakwenda kujifunza tabia hizi nane, na ombi langu kwako ni uhakikishe tabia hizi unajijengea na kuwa nazo zote kwa pamoja, ili kujihakikishia kufikia mafanikio makubwa. karibu tujifunze kwa pamoja.
Kabla hatujaingia kwenye tabia hizi nane, naomba nikukumbushe kwamba tunapozungumzia mafanikio hatuzungumzii fedha pekee, maana hiki ndio wengi huwa wanafikiri. Tunazungumzia ule mchango ambao mtu ameweza kuutoa kwa dunia na wale wanaomzunguka na kufanya maisha yao kuwa bora zaidi. Na mara zote watu hawa wanaotoa mchango huu bora kwa wengine, fedha huwafuata bila hata ya kutumia nguvu ya ziada. Hivyo karibu tujifunze kwa pamoja ili uweze kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufikia mafanikio haya makubwa.

 
Tabia nane za watu wenye mafanikio makubwa.
TABIA YA KWANZA; Penda unachofanya.
Hakuna mtu ambaye amefanikiwa ambaye hapendi kile anachofanya. Hii ni tabia ambayo kila mtu aliyefanikiwa anayo, wanapenda sana kile ambacho wanakifanya, na wapo tayari kukifanya hata kama hawalipwi fedha. Katika kuwahoji watu waliofanikiwa, Richard aliambiwa na mmoja, nipo tayari kumlipa mtu ili aniruhusu kufanya ninachofanya.
Umeelewa vizuri hapo rafiki yangu, yaani mtu anapenda kile kitu anachofanya, kiasi kwamba kama atanyimwa asifanye, yupo tayari hata kulipia ili apate nafasi ya kukifanya. Sasa hebu niambie ni nini kitamzuia mtu kama huyu kufikia mafanikio?
Ni muhimu sana kupenda kile unachofanya kwa sababu kuu mbili;
Sababu ya kwanza safari ya mafanikio ni ndefu, siyo fupi kama wengi wanavyodanganyana, unahitaji miaka siyo chini ya kumi ndiyo uweze kufikia mafanikio makubwa. sasa kufanya kitu usichokipenda kwa miaka kumi ni sawa na kuchagua kupoteza maisha yako.
Sababu ya pili ni changamoto, hakuna kitu chochote utakachofanya ambacho kitakosa changamoto. Unapokutana na changamoto kwenye kitu unachokipenda unaendelea kuweka juhudi. Lakini unapokutana na changamoto kwenye kitu usichokipenda unazidi kukata tamaa.
HATUA YA KUCHUKUA; Fanya kile ambacho unapenda kufanya. Kama unachofanya sasa siyo unachopenda, unaweza kufanya moja kati ya haya mawili, penda hiko unachofanya kwa sasa, au anza kufanya kile unachopenda, japo kwa pembeni. Hakuna namna unaweza kufikia mafanikio makubwa kama hupendi kile unachofanya.
SOMA; Jinsi Unavyoweza Kuwa Sumaku Ya Fedha, Njia Kumi (10) Za Kuivuta Fedha Ije Kwako Muda Wote.
TABIA YA PILI; Kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.
Hakuna kitu chochote ambacho kinakuja bila ya kufanya kazi. Hiki ni kitu ambacho wanaofikia mafanikio makubwa wanakijua na hawatafuti njia yoyote ya kukwepa. Wenye mafanikio wapo tayari kujitoa na kuweka juhudi kubwa kwenye kazi zao, wako tayari kufanya kazi kwa muda wa ziada. Hakuna mtu aliyefanikiwa sana ambaye anafanya kazi masaa nane kwa siku na siku tano kwa wiki, hii ni njia ya wanaoshindwa.
Ila sasa ukija upande wa pili, kwa wale wanaoshindwa, ndiyo utaona picha ya tofauti kabisa. Kwanza wanachukulia kazi kama adhabu, na mara zote wanatafuta njia ya kukwepa majukumu yao. Hawapo tayari kujituma na kuweka juhudi kubwa kwenye kile wanachofanya. Mara nyingine hupata mawazo ya kuwapoteza zaidi kama kufikiria kushinda bahati na sibu au kupata bahati ya mafanikio.
Kazi kazi kazi, ni lazima kuweka kazi ya maana kama kweli mtu anataka kufikia mafanikio makubwa.
HATUA YA KUCHUKUA; Jitoe kuweka juhudi kubwa na maarifa kwenye kazi au biashara unayofanya. Usiwe na mawazo ya wanaoshindwa, kwamba uanze kazi saa mbili, umalize saa kumi, jumatatu mpaka ijumaa. Jioni za siku za wiki, jumamosi na jumapili yote kuwa siku za mapumziko. Hii ni njia ya uhakika ya kushindwa. Thamini kazi, na jitume sana kwenye kuifanya.
TABIA YA TATU; Kuwa na lengo na umakini.
Huwezi kumkuta mtu aliyefanikiwa akijaribu kufanya jambo moja, halafu akaenda jingine, na jingine tena. Watu wote waliofanikiwa wanajua ni nini hasa ambacho wanakitaka, na wanapeleka nguvu zao zote kuhakikisha wanapata kile ambacho wanakitaka. Watu waliofanikiwa wanakuwa na malengo, ambayo wameyapangilia vizuri kabisa na kila siku wanayafanyia kazi. Hawafanyi mambo kwa kujaribu au kukurupuka, wanajua ni wapi wanakwenda na hivyo kuwa tayari kufanya kile kinachohitaji kakufanya.
Pia watu hawa wana umakini mkubwa, wanajua ya kwamba hawana nguvu wala muda wa kuweza kufanya kila kitu wanachotamani kufanya. Na hivyo wanachagua kufanya mambo machache muhimu kwao na kuachana na mengine ambayo hayana umuhimu kwao.
Sasa njoo kwa wale ambao hawafanikiwi, kwanza wapo tu, hawajui ni wapi wanapotaka kwenda, wao wanaangalia siku ya leo inavukaje, ikishavuka wanafikiria tena kesho. Yaani badala ya kuchagua kuishi wao wanachagua kusukuma siku. Hawajui miaka mitano ijayo wanataka kuwa wapi, miaka kumi na hata ishirini wawe wapi. Na hivyo hawana kipaumbele chochote kwenye maisha yao kitu ambacho kinawafanya wanakosa umakini.
HATUA YA KUCHUKUA; Jiulize miaka mitano ijayo utakuwa wapi, vipi miaka kumi ijayo? Kama huna wazo lolote ni wakati wa kukaa chini sasa na kujiwekea malengo ambayo ndiyo utayafanyia kazi. Usikubali kusukuma siku, chagua kuishi kwa kuchagua kufanyia kazi kitu ambacho ni kikubwa, hivyo malengo ni muhimu.
SOMA; Sababu Tano Zinazokuzuia Kufikia Malengo Yako Ya Kila Mwaka Na Jinsi Ya Kuepuka Hilo 2016.
TABIA YA NNE; Kujisukuma.
Pamoja na kupenda kile unachofanya, pamoja na kuwa tayari kuweka juhudi kubwa, siyo kwama mambo ndiyo yatakuwa mteremko. Unahitaji kujisukuma sana, yaani sana. Kuna wakati utaona kama mambo hayaendi, pamoja na kuweka juhudi kubwa huoni matokeo uliyokuwa unategemea. Wakati kama huu ndiyo rahisi sana kukata tamaa na kuacha, lakini hapa ndipo wanaofanikiwa wanapotofautiana na wanaoshindwa.
Wanaofanikiwa wanaendelea kujisukuma licha ya kuwa kwenye wakati mgumu. Wanajisukuma kuendelea kuweka juhudi kubwa, hawajionei huruma hata kidogo, kwa sababu wanajua kama wakifanya hivyo hawataweza kufika mbali. Watu hawa wanaendelea kufanyia kazi mipango yao hata pale kila kitu kinapoonekana kigumu na kimekwama. Na ni ubishi wao huu ndio umekuwa unawasaidia wanafikia mafanikio makubwa.
Wale wanaoshindwa wao hawajisumbui kujisukuma, wanapokutana na changamoto au ugumu hukimbia haraka na kusema haiwezekani. Hawajisumbui kuendelea kuweka juhudi kubwa, na ni watu wa kukata tamaa haraka sana.
HATUA YA KUCHUKUA; Jiulize je umekuwa unaweka juhudi kiasi gani hata pale unapokutana na ugumu au changamoto. Na jiambie kauli hii moja, utaendelea kufanyia kazi mipango yako, hata kama unakutana na ugumu kiasi gani. Amua kwamba hiyo ndiyo njia pekee uliyochagua kufuata na hakuna nyingine.
TABIA YA TANO; Mawazo.
Watu waliofanikiwa huwa na mawazo ambayo wanayafanyia kazi. Wanaanza na wazo la kawaida na wanalifanyia kazi huku wakipata mawazo mengine zaidi ya kuboresha. Hawasubiri mpaka wapate wazo moja bora sana, badala yake huanza na wazo lolote ambalo linaendana na kile ambacho wanapenda kufanya, kisha wanaanza kulifanyia kazi.
Kwa upande wa wale wanaoshindwa, huwa wanakuwa na mawazo, tena mengi, lakini utekelezaji wao ni hafifu sana. Mara nyingi huwa wanaona wazo walilonalo siyo bora na hivyo kuendelea kutafuta mawazo bora zaidi. Wakati wao wanazunguka kutafuta mawazo, wenzao wanafanyia kazi mawazo waliyonayo. Wanapokuja kupata wazo wanalofikiri ni bora, wanapoanza kulitekeleza wanagundua lina mapungufu na hii inazidi kuwakatisha tamaa.
HATUA YA KUCHUKUA; Je mpaka sasa bado unatafuta wazo bora? Unaendelea kupoteza muda wako, angalia ni nini unapenda kufanya, anza na wazo lolote linalokujia na endelea kuliboresha kadiri siku zinavyokwenda. Usisubiri mpaka upate wazo bora, wazo bora tayari lipo ndani yako, na litafunguka pale utakapoanza kufanyia kazi mawazo uliyonayo.
TABIA YA SITA; Kuboresha.
Hakuna kitu ambacho kimekamilika, na kuwa vizuri leo haimaanishi utaendelea kuwa vizuri siku zijazo. Wanaofanikiwa wanalijua hili na wanalifanyia kazi kila siku. Wanajua chochote wanachofanya leo kinahitaji kuboreshwa zaidi kila siku kama kweli wanataka kuwa na mafanikio makubwa. kwa chochote wanachofanya wanajua kabisa ya kwamba hakuna wakati watafika na kusema tayari tumefikia kilele. Wanajua kuboresha zaidi ni zoezi endelevu na wamekuwa wakiboresha sana kile ambacho wanafanya.
Wasiofanikiwa hawaoni umhimu wa kuboresha, wanaendelea kufanya kile ambacho wamezoea kufanya, na wanaendelea kukifanya kwa mtindo ule ule ambao wamezoea kufanya. Wanafanya mambo yao kwa mazoea na hawakazani kuenda nje ya kile walichozoea. Kwa njia hii wanazidi kurudi nyuma wakati dunia inakwenda mbele kwa kasi.
HATUA ZA KUCHUKUA; Jiulize je kile unachofanya kila siku unaboresha au unafanya kama ambavyo umezoea kufanya? Je unakazana kufanya vitu vipya ambavyo vitaleta mabadiliko bora zaidi au unaendelea kufanya kile ambacho umekuwa unafanya kila siku na kwa mtindo ule ule? Unahitaji kuboresha kila siku kile unachofanya kama unataka kufikia mafanikio makubwa.
SOMA; Kitu Kimoja Ambacho Wapenda Mafanikio Wote Wanacho Kwa Pamoja.
TABIA YA SABA; Hudumia wengine.
Hakuna mafanikio ambayo yanatokana na wewe mwenyewe. Mafanikio yako yatatokana na ile huduma ambayo unaitoa kwa wengine. Na kadiri kile unachofanya kinavyogusa maisha ya wengi, ndivyo unavyokuwa na nafasi kubwa zaidi ya kufanikiwa. Watu wenye mafanikio wanafurahia kuwa mchango kwenye kuboresha maisha ya wengine. Mara zote wanajiuliza ni watu gani ambao hawajawafikia bado, wanajiuliza ni kipi wakifanya kitawasaidia wengine zaidi. Kwa njia hii wanawafikia wengi na wao kuzidi kufanikiwa.
Wale wanaoshindwa wamekuwa wakijiangalia wao wenyewe tu, wamejawa na ubinafsi, hawajali wengine wananufaika vipi, wao wanachojali ni nini wanapata. Hawaoni kama kuboresha maisha ya wengine ni nafasi bora kwao, bali wanaona ni kama mzigo. Kwa mtazamo huu wanashindwa kuwafikia wengi zaidi na hili linawazuia kufikia mafanikio makubwa.
HATUA ZA KUCHUKUA; Fikiria ni watu gani wanaonufaika na ile kazi au biashara unayoifanya, kisha angalia ni jinsi gani unaweza kuwafikia watu wa aina hiyo zaidi. Lengo lako liwe kutoa huduma bora sana kwa wengi ili uweze kupata mafanikio makubwa.
TABIA YA NANE; Ng’ang’ana.
Watu wenye mafanikio ni ving’ang’anizi wakubwa sana. Watu hawa huwa hawakubali kushindwa au kuacha kirahisi. Wamejitoa kupambana mpaka tone la mwisho. Hawakubali kirahisi pale anapoambiwa hapana au haiwezekani. Wanajua mlango mmoja ukifunga, kuna milango mingine bado ipo wazi. Pamoja na kukutana na magumu na changamoto nyingi, haiwajii kwenye akili yao kwamba ndiyo mwisho wa safari waliyochagua. Wanajua hiyo ni hali ya kawaida na wanaendelea kupambana mpaka wafikie kile wanachokitaka.
Wale wasiofanikiwa hawang’ang’ani sana, wanajaribu na wanapokutana na vikwazo wanaishia hapo. Hawakazani tena kuendelea kuweka juhudi, badala yake wanakimbia na kusema haiwezekani.
HATUA YA KUCHUKUA; Kama kweli unataka kufikia mafanikio makubwa, jipange kabisa ya kwamba hutakubali kitu chochote kikurudishe nyuma. Unahitaji kuwa king’ang’anizi maana ni wengi na mengi yatakuwa yanakurudisha nyuma. Bila ya kujitoa hivyo, hutaweza kupiga hatua yoyote kubwa.
Hizo ndiyo tabia nane ambazo unatakiwa kuwa nazo kwa pamoja ili uweze kufikia mafanikio makubwa. Kama ulivyoona hapo juu, tabia hizo hazitegemei kiwango chako cha elimu, au umetokea familia gani au una rangi gani. Tabia hizo zinaanza na wewe mwenyewe kuamua kufanikiwa na kujijengea tabia hizo nane.
Pia kuna tabia nyingine saba ambazo zitakuwezesha kuwa na ufanisi mkubwa, unaweza kukisoma kwenye kitabu hiki hapa ambacho utakipata kwa kubonyeza maandishi haya. Ni nzuri na muhimu sana, usiache kuzisoma.
Nakutakia kila la kheri katika kujijenga tabia hizo nane.
TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s