Kitu chochote kikubwa unachotaka kufanya kwenye maisha yako, kinaanza na kile ambacho unacho kwa sasa. Hakuna njia nyingine unayoweza kuanzia.
Hivyo kama unasubiri siku moja ukishapata kitu fulani ndiyo uanze, unajichelewesha bure. Kwa kusubiri hivi hutaweza kuanza.
Lakini kama utaangalia ni nini unacho sasa, na kufikiria njia bora ya kuanza kutumia ulichonacho, utapata hata kile ambacho kwa sasa huna, ambacho ndiyo ulikuwa unasubiri ukipate.
Kwa kuwa hakuna wakati utakuwa tayari kusema tayari nina kila ninachotaka, ni vyema kuamua kuanza na kile ulichonacho sasa, kama kweli unataka kufika kule unakotaka kufika. Lakini kama unataka sababu ya kwa nini usifanye, basi kile unachokosa ni sababu nzuri, na ambayo haitakosa mashiko, maana mara zote kipo ambacho unakosa.
Unaamua nini rafiki, kuanza na kile ulichonacho, au kuendelea kusubiri na kupoteza muda? Kwa sababu kuendelea kusubiri siyo ndiyo kunakuletea mazingira bora, bali kunakuchelewesha kuchukua hatua na hivyo kuipoteza fursa.
SOMA; Mambo 15 Ya Kung’ang’ania Bila Ya Kujali Watu Wanasema Nini.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba njia pekee ya kufika kule ninakotaka kufika ni kuanza na kile ambacho ninacho kwenye mikono yangu kwa sasa. Kusubiri mpaka nipate kile ninachofikiria nitapata baadaye ni kujichelewesha, maana sitafika wakati na kuwa na kila ninachotaka. Ni vyema nikaanza na vile ninavyokosa nitavipata mbele ya safari.
NENO LA LEO.
Anza na ulichonacho sasa kwenye mikono yako. Usisubiri mpaka upate kila kitu, huwezi kufikia hali hiyo ya kuwa na kila kitu. Anza na ulichonacho na vile unavyokosa utavipata ukishaanza safari.
Hivi ndivyo mafanikio yanavyotengenezwa, siyo kwa kuangalia umekosa nini, bali kwa kuangalia una nini na unakitumiaje.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.