Moja ya vitu vinavyotuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye chochote tunachofanya kwenye maisha yetu ni mazoea.
Huwa tunaanza kufanya kitu tukiwa na hamasa kubwa sana na tunaweka juhudi kubwa na ubunifu pia. Lakini baada ya muda tunazoea na hivyo kufanya kwa mazoea, ubunifu unakwisha na juhudi zinakuwa kidogo.
Hii ni kwenye kila eneo la maisha yetu, kuanzia ndoa, kazi, biashara, elimu na mengine mengi.
Sasa njia moja ya kuondokana na hili ni kujifukuza wewe mwenyewe.
Yaani wewe mwenyewe unajifukuza kwa kuwa na fikra hizi. Kwamba ikiwa nitafukuzwa hapa nilipo, na mwingine akapewa kitu hiki afanye, je atakifanya kwa utofauti gani?
kwenye biashara jiulize ikiwa mteja wako atakufukuza, yaani ataacha kununua kwako, je ataenda kununua kwa mtu anayefanyaje kwenye biashara zake?
Ikiwa upo kwenye ajira jiulize kama mwajiri wako atakufukuza leo, je mwingine atakayeajiriwa ataifanyaje kazi unayofanya sasa?
Ikiwa ni kwenye ndoa au mahusiano mengine jiulize, iwapo uliyenaye sasa ataamua kukuacha, je mwingine atakayekuwa naye, atakuwa na sifa zipi za tofauti?
Jiulize swali hili kwenye kila eneo la maisha yako na utaona ni jinsi gani unaweza kuliboresha zaidi. Na yale majibu unayoyapata yafanyie kazi mara moja.
Usisubiri mpaka ufukuzwe, jifukuze wewe mwenyewe ili uweze kuwa bora zaidi.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba kufanya kwa mazoea ndiyo adui mkubwa wa mafanikio yangu. Ili kuondokana na mazoea nitajijengea utaratibu wa kujifukuza mimi mwenyewe, kwa kujiuliza iwapo nitafukuzwa kwenye hiki ninachofanya sasa, atakayepewa nafasi hii atafanya kwa utofauti gani? Kisha nitafanyia kazi majibu ninayopata.
NENO LA LEO.
Jifukuze wewe mwenyewe kabla hujafukuzwa na wengine. Kwenye jambo lolote unalofanya jiulize swali hili muhimu sana; ikiwa utafukuzwa kwenye hiko ambacho unafanya, iwe ni biashara, kazi au hata ndoa, je yule atakayepewa nafasi yako ataboresha vipi utendaji wake? Fanyia kazi majibu utakayopata na hakuna yeyote atakayeweza kukufukuza.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.