Biashara yoyote inapaswa kukua zaidi kadiri muda unavyokwenda. Na kuna njia nyingi za kuikuza biashara, mojawapo ikiwa ni kuongeza mtaji wa biashara hiyo. Na pia kwenye kuongeza mtaji, kuna njia nyingi za kuweza kufanya hivyo, unaweza kutumia faida unayoipata, na pia unaweza kuomba mkopo kwenye taasisi za kifedha kama benki.

Unapokwenda kuomba mkopo wa kibiashara benki, benki haikujui wewe wala biashara yako, na hivyo inahitaji kupata taarifa za maendeleo ya biashara yako ili kujua kama kweli unafaa kupewa mkopo unaotaka na kama ukipewa unaweza kuurudisha. Hivyo benki itataka kujiridhisha kama kweli biashara yako inakwenda vizuri. Pamoja na kwamba utajieleza na kueleza mipango yako, kuna kipimo kimoja ambacho benki itatumia kupima uhai wa biashara yako. kipimo hiki ni taarifa za kibenki kwa miezi sita iliyopita.

Taarifa hii inaonesha mzunguko wa fedha kwenye biashara yako kupitia kwenye akaunti ya biashara yako, na siyo akaunti yako binafsi. Hivyo ni muhimu sana kwa kila biashara kuwa na akaunti ya benki ya biashara. Hata kama biashara yako ni ndogo, unahitaji kuwa na akaunti tofauti ya biashara benki. Usichanganye fedha za biashara kwenye akaunti yako binafsi. utakapohitaji kuonesha maendeleo ya biashara yako, moja ya vipimo muhimu ni taarifa za akaunti ya biashara.

Kuwa na akaunti hii ya biashara kwenye benki ni hatua ya kwanza na muhimu sana katika kuiweka biashara yako kwenye nafasi nzuri ya kukopeshwa. Ila kuwa tuna hii akaunti hakutoshi, bado kuna mambo mengine unahitaji kuzingatia, na hapa tutayajadili yale muhimu zaidi.

Weka utaratibu wa wateja wako kukulipa kupitia akaunti ya benki. Kulingana na biashara yako ilivyo, unaweza kuweka utaratibu mzuri wa kuwawezesha wateja wako kulipa kwa njia ya benki. Na kwa maendeleo ya sasa siyo lazima waende benki, bali wanaweza kulipa hata kwa njia ya mitandao ya simu. Kwa njia hii utarahisisha mzunguko wa fedha kwenye biashara yako na pia utaondoa hatari ya vitendo vya kihalifu. Kama wateja wako wanalipia kiasi kikubwa, unakuwa kwenye hatari ya kuvamiwa na majambazi na kuibiwa fedha za mauzo, hasa kama wanaona unauza sana. Na hili pia litakusaidia wewe kuweka taarifa zako za kibenki vizuri.

Kitu kingine muhimu sana kufanya ni kupeleka mapato ya kila siku benki. Kila siku yale mapato unayopata yapeleke benki. Hii itaboresha taarifa zako za kibenki na wakati huo pia itakuondolea hatari ya vitendo vya kihalifu. Kukaa na fedha taslimu kwa kiasi kikubwa kwenye biashara yako, unajiweka kwenye hatari ya kuvamiwa na kuibiwa fedha hizo. Lakini unapoziweka benki, hata kama utapata uvamizi, hutapoteza kiasi kikubwa cha fedha zako. Na kwa kufanya hivi unaweza taarifa zako vizuri, kama kila siku unaweka fedha kwenye akaunti ya biashara yako, siku utakapoomba mkopo wataangalia taarifa zako za kifedha na hizi ndio zitaamua ni kiasi gani cha mkopo unaweza kupewa na benki. Kama umekuwa unaweka kiasi kikubwa cha fedha hii inaongeza kiasi cha mkopo unachoweza kupewa kwenye benki.

Kitu cha mwisho kuzingatia ni kuwalipa wale wanaokudai kupitia benki na unapokuwa na akaunti ya biashara unaweza kutumia hundi katika malipo. Unapolipa kwa hundi au kwa njia nyingine ya kibenki kama kuhamisha fedha, inaweka taarifa zako za mzunguko wa fedha kwenye biashara vizuri. Na pia inaimarisha usalama wa fedha zako kuliko wewe kwenda kutoa kiasi kikubwa cha fedha na kumpelekea yule unayekwenda kumlipa.

Kama mpaka sasa biashara yako haina akaunti ya benki ya kibiashara ni muhimu ufanye hivyo sasa kwa sababu unajinyima mengi. Na pia kama una akaunti ya kibiashara na umekuwa huitumii kama ambavyo tumeona hapo juu anza kuitumia vizuri akaunti yako ili uweze kupata faida hiyo ya mkopo na pia kuwa na usalama mzuri wa fedha zako. Nakutakia kila la kheri.