Ukifanya biashara unapata uhuru na unaweza kutengeneza faida nzuri na kukuza biashara yako zaidi. Lakini siyo mara zote utatengeneza faidia kupitia biashara yako.
Ukiweka juhudi kubwa kwenye kazi yako, na kuifanya kwa moyo na kujitoa utapata matokeo bora na kuongeza thamani ya kile unachotoa na kile unachopokea pia. Lakini siyo mara zote majibu yatakuja kama unavyotegemea.
Juhudi zozote unazofanya kwenye kazi, biashara na maisha yako kwa ujumla zinaweza kuzaa matunda bora sana, lakini siyo mara zote. Kuna wakati utafanya kila unachotakiwa kufanya lakini usipate yale matokeo uliyotegemea kupata.
Lakini bado unahitaji uendelee kufanya. Kwa sababu gani uendelee kufanya?
Kwa sababu kadiri unavyofanya mara nyingi, ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi ya kupata matokeo bora. Hakuna juhudi unazoweka zinapotea, usipozifaidi sasa, jua utazifaidi sana baadaye.
Hivyo hata kama unafanya kila ambacho unajua ni sahihi, lakini bado hupati majibu uliyotegemea, usiache kufanya, kwa sababu kadiri unavyofanya mara nyingi ndivyo unavyotengeneza nafasi za wewe kushinda zaidi.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba siyo mara zote nitapata kile ninachotegemea kupata licha ya kufanya kila ninachotakiwa kufanya. Ninaweza kuweka juhudi kubwa lakini bado nisipate matokeo bora. Sitakatishwa tamaa na hili kwa sababu najua juhudi zangu hazipotei, nitanufaika nazo kwa ubora zaidi baadaye.
NENO LA LEO.
Huwezi kupata kile unachotegemea kupata mara zote. Kuna wakati utafanya kila unachotakiwa kufanya, lakini usipate yale matokeo uliyotegemea kupata. Usikatishwe tamaa kwenye nyakati kama hizi, badala yake endelea kuweka juhudi na utapata matokeo bora zaidi huko mbeleni. Hakuna juhudi yoyote unayoweka inapotea.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.